Katibu Muenezi wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Juma 'Gadafi' akizungumza katika
mkutano na waandishi wa habari ofisi kwake leo August 22,2015 asubuhi, kuhusu
kukamilika kwa maandalizi ya uzinduzi wa mkutano wa kampeni za uchaguzi
mkuu wa chama hicho utaofanyika kesho August 23,2015 viwanja vya Jangwani jijini Dar es
Salaam.
Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
Picha zikichukuliwa.
Na Dotto Mwaibale
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es
Salaam kimetangaza ratiba ya uzinduzi wa kampeni za uchaguzi wa chama
hicho utakaofanyika viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam.
Katibu Muenezi wa chama hicho Mkoa wa
Dar es Salaam, Ramadhan Juma 'Gadafi' akizungumza na waandishi wa habari
ofisi kwake Dar es Salaam leo August 22,2015 asubuhi, alisema maandalizi yote ya
uzinduzi huo tayari yamekamilika.
"Maandalizi yote tayari yamekamilika na
leo jukwaa kubwa la kukaa viongozi linafungwa na tunategemea kuwa na
watu wengi katika uzinduzi huo" alisema Gadafi.
Gadafi alisema kuanzia saa tatu asubuhi
watu kutoka sehemu mbalimbali na wapenzi wa chama hicho wataanza
kuwasili katika viwanja hivyo ambapo viongozi wastaafu wa chama na
serikali na wale waliopo kazini watafuatia na kisha watawasili mgombea
nafasi ya urais kupitia CCM Dk.John Magufuli na mgombea mwenza wake
Samia Hassan Suluhu na baadae Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete.
Alisema katika uzinduzi huo wageni
mbalimbali wamealikwa kutoka mikoa ya jirani na mabalozi kadhaa
wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.
Gadafi alisema kuwa wakati wa uzinduzi
wa kampeni hizo viongozi wa chama hicho wakiwemo mgombea urais
Dk.Magufuli na mgombea mwenza wake watahutubia wanachama kuelezea sera
za chama hicho na utekelezaji wa ilani ya CCM kuelekea uchaguzi mkuu.
Gadafi alitumia nafasi hiyo kuwaomba
wananchi, wanaccm na makundi mengine kufika katika uzinduzi huo ambapo
kutakuwepo na vikundi mbalimbali vya burudani na kufanyika kwa dua za
madhehebu yote za kukiombea chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu kama
inavyofanyika vipindi vyote wanapo zindua kampeni za uchaguzi mkuu.
Katika hatua nyingine Gadafi amekemea
vikali vitendo vya udhalilishaji kwa wanachama wake vya kuzomewa na
kuchaniwa nguzo zao wanapopita maeneo ya Kariakoo na Mwenge.
Alisema kila mwana chama yeyote wa chama
cha siasa ana haki ya kuvaa nguo za chama chake hivyo kuwazomea
wanachama wao ni kukiuka sheria ya nchi na inaweza kuleta ugomvi pale
upande wa pili utakapoamua nao kujibu mapigo.
"Napenda kuiomba serikali ya mkoa wa Dar
es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Suleiman Kova kukomesha
vitendo hivyo dhidi ya wanachama wetu na kama wanaona tunawakera
wasubiri majibu yao baada ya uchaguzi kwani CCM itachukua ushindi mapema
huku wakibaki wakishangaa" alisema Gadafi.
No comments:
Post a Comment