UCHUMI WETU:-Tazama Viwango vya Nauli za Mabasi mikoani zilivyoshuka. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Saturday, April 18, 2015

UCHUMI WETU:-Tazama Viwango vya Nauli za Mabasi mikoani zilivyoshuka.

MABASI.

Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini Tanzania (SUMATRA) imepunguza nauli za mabasi ya mikoani huku ikitangaza kubaki kama zilivyokuwa, zile za daladala baada ya ukokotoaji wake kuonyesha tofauti ndogo ya punguzo kulinganisha na viwango vya sasa.


Punguzo hilo lina maana kwamba nauli za mabasi kutoka Dar es Salaam – Arusha ni Sh 21,000 badala ya Sh 22,700; Dar es Salaam – Bukoba ni Sh 51,000 badala ya 55,100; Dar es Salaam–Kigoma ni Sh 57,000 badala ya 59,800; Dar es Salaam – Mtwara Sh 20,000 badala ya 21,500 na Dar es Salaam – Mbeya Sh28,500 badala ya 30,700.

Katika ukokotoaji wa nauli hizi, tumezingatia madaraja ya mabasi kama yalivyoelekezwa katika kanuni za huduma za abiria za 2014,” alisema Ngewe na kuongeza kuwa nauli za mabasi ya daraja la juu hazidhibitiwi.
Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Gilliard Ngewe alisema pamoja na kupungua kwa kiasi hicho, Bodi ya Wakurugenzi ya SUMATRA iliridhia kuwa nauli zinazotumika sasa ziendelee ili kupunguza usumbufu.

Uamuzi huu unatokana na punguzo lililokokotolewa kuwa dogo ikilinganishwa na viwango vilivyopo sasa. Iwapo vitapitishwa vitasababisha usumbufu katika malipo,” alisema Ngewe na kusisitiza kuwa nauli kwa wanafunzi itaendelea kuwa Sh200 kama ilivyo sasa.

Alisema SUMATRA ilipokea maombi mengi mwaka jana 2014 juu ya kushusha nauli za mabasi kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta na kuanza mchakato wa kuzipitia upya kwa kukusanya maoni ya wadau mbalimbali.

Alisema Machi 9, 2015 walipokea maombi ya kushusha nauli kutoka kwa Baraza la Ushauri na Watumiaji wa Huduma zinazodhibitiwa na Sumatra (SUMATRA - CCC), likitoa hoja ya kushuka kwa bei ya mafuta na kodi ya forodha kwa mabasi mapya yanayoingia nchini kutoka asilimia 25 hadi 10.

Bodi ya wakurugenzi ilibaini kuwa gharama za utoaji huduma za usafiri mijini zinapaswa kutazamwa kwa ujumla wake ikiwa ni pamoja na punguzo la bei ya mafuta ili kufikia viwango vya nauli inayostahili,” alisema mkurugenzi huyo.

VIONGOZI WA SUMATRA.

Kuhusu mabasi ya masafa marefu, Ngewe alisema bodi hiyo iliridhia kupunguza viwango vya nauli kutokana na sababu hizo za SUMATRA - CCC.

Alisema nauli mpya kwa abiria mmoja anayetumia basi la daraja la kawaida la chini imepungua kwa asilimia 7.8, wakati daraja la kati ikipungua kwa asilimia 5.81.

Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), Enea Mrutu alisema walishirikishwa na Sumatra lakini hawakukubaliana na wazo la kupunguza nauli kwa sababu ya gharama nyingine za uendeshaji.

Alisema wamiliki wa mabasi watakutana kesho kujadili nauli hizo na kuona kama punguzo hilo litaathiri shughuli zao au la... “Bado sijapata nauli mpya, nadhani hiyo pia itakuwa ajenda kwenye mkutano wetu. Tutatoa taarifa kwa kile tutakachokuwa tumeamua baada ya mkutano huo.”

Ukokotoaji huo ulibainisha nauli ya daladala kwa umbali wa kilomita 10 kuwa Sh 376 badala ya Sh 400; Sh 448 badala ya Sh 450 kwa kilomita 11–15, Sh 485 badala ya Sh 500 kwa kilomita 16–20, Sh 583 badala ya Sh 600 kwa kilomita 21–25 na Sh742 badala ya 750 kwa umbali wa kilomita 26–30.

Pata Picha, Habari za Kisiasa, Kijamii, Kiuchumi na Michezo kila stori inayonifikia wakati  wowote ukijiunga na mimi kwa kubonyeza…..FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad