|
MWANANCHI
Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat
Gwajima jana April 05,2015 alihubiri akiwa katika kiti cha magurudumu na kusema
hawezi kuwatupa Mbunge Edward Lowassa na Dk Wilbrod
Slaa kwa kuwa ni marafiki zake wa siku nyingi.
Gwajima alisema kumekuwa uvumi kwamba kuhojiwa kwake na polisi
kulitokana na kuwakaribisha wanasiasa hao kanisani kwake kwa nyakati tofauti na
kuzungumza na waumini wake.
Askofu huyo amesema alifahamiana na Lowassa
tangu mwaka 1996 na alifahamiana na Dk Slaa tangu
mwaka 1994 kabla hajagombea nafasi ya Urais kupitia CHADEMA, baada ya hapo
urafiki wao walikuwa kama familia.
“Hawawezi
kunichagulia marafiki, hawa ni watu wangu wa karibu hata kabla hawajawa na
ndoto za kugombea urais, nitaendelea kuwa nao karibu,”—Askofu Gwajima.
“Polisi
walinihoji mambo mengi binafsi yanayonihusu mimi na hayakuhusiana kabisa na
Pengo, maswali ya Pengo yalikuwa machache sana,”—Askofu
Gwajima.
Hata hivyo, Gwajima alisema
hana ugomvi na polisi wala Serikali kwa kuwa amekuwa akitoa ushirikiano kwa
vyombo hivyo.
NIPASHE
Askari wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Sikonge
mkoani Tabora, PC Charles amejiua kwa kujipiga risasi, baadhi
ya wananchi wanaoishi jirani na kituo hicho cha polisi walisema tukio hilo
lilitokea Aprili 4 mwaka huu saa 1:00 usiku kituoni hapo.
“Suala hili
limetushangaza, kwani sisi tulikuwa nyumbani. Ghafla tulisikia mlio wa bunduki
katika kituo cha polisi. Tulipofika, tulimkuta askari huyo akiwa amekufa kwa
kujipiga risasi,” alisema Lazaro ambaye ni moja wa
mashuhuda.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Suzana
Kaganda alithibitisha kujiua kwa askari huyo; “Ni kweli askari huyo amejiua kwa kujipiga risasi wakati akiwa
kituoni majira ya saa 1:00 usiku,” alisema Kamanda Kaganda.
Kamanda huyo alisema hakuna ujumbe wowote
ulioachwa na askari huyo kuelezea sababu za kujiua na kuwataka askari wote
kutatua matatizo yao kupitia viongozi wao badala ya kujichukulia sheria
mkononi.
Alisema uchunguzi unaendelea ili kubaini
chanzo cha askari huyo kujiua.
MWANANCHI
Mtoto Abdul Mohamedi ambaye ni
mlemavu wa viungo, amelazimika kuishi darini kwa miezi minne mfululizo kukwepa
kudhuriwa na mafuriko kutokana mvua kubwa zinazoendelea kunyesha Mtwara.
Bibi wa mtoto huyo Zainabu Lipuga
alisema jana kuwa alimpandisha darini mjukuu wake Novemba mwaka jana baada ya
mafuriko yaliyotekea kipindi hicho.
“Nilipoona mvua
zinanyesha nikaona bora nimnusuru mjukuu wangu asisombwe na mafuriko kwa vile
sina nguvu za kuweza kumpandisha na kumteremsha mara kwa mara,”
alisema Lipuga
Bibi huyo amesema baba wa mtoto hajulikani
alipo na jukumu la kumlea limeachwa mikononi mwake bila msaada.
Zaidi ya nyumba 200 zilizingirwa na maji
kutokana na mvua kusababisha hasara kwa wananchi ikiwemo kuharibika mali zao
zikiwamo nguo na vyakula.
MTANZANIA
Sakata la kufungiwa kwa miaka miwili kwa
shindamo la Miss Tanzania limechukua sura mpya baada ya Wizara ya Habari Vijana
Utamaduni na Michezo kulirudisha suala hilo BASATA kwa kuandika barua ya kuomba
msamaha.
“Tumeandika barua
kuomba msamaha BASATA kama tulivyoelekezwa kutoka Wizarani, hivyo tunasubiri
majibu..”—alisema Hidan Rico, Ofisa Habari wa Miss
Tanzania.
Kampuni ya Lino International Agency
ilikata rufaa ya kufungiwa kufanya mashindano hayo ya Miss Tanzania ambayo wao
ndio walikuwa waandaaji.
Gazeti la TANZANIA DAIMA walifanya jitihada
za kuwapata wahusika wa BASATA wazungumzie kuhusu suala la kuandikiwa barua
lakini hakuna mhusika yoyote aliyepatikana.
NIPASHE
Zaidi ya watu 1,600 hawana makazi
kutokana na mvua kubwa iliyonyesha Wilaya ya Busega, Simiyu pamoja na
kuambatana na upepo mkali ambao umeangusha nyumba hizo.
Mmoja wa mashuhuda ambaye pia ni mmoja wa
waathirika wa janga hilo amesema kuwa mvua hiyo ilianza kunyesha kidogo kidogo
na baadaye ikaongezeka pamoja na upepo mkali ambao ulipelekea nyumba kuanza
kuanguka.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa ya Wilaya
ambaye ni Mkuu wa Wilaya hiyo pia, Paul Mzindakaya amesema
tayari ameagiza wananchi waliokumbwa na maafa hayo kuorodhesha ili wapatiwe
msaada pamoja na kuwahimiza waishio mabondeni kuhama ili kujiepusha na maafa.
Watu hao waliokosa makazi wameathirika pia
kutokana na kukosa chakula na mavazi baada ya mvua kusomba kila kitu.
Source:-Magazetini Tanzania.
Pata
Picha, Habari za Kisiasa, Kijamii, Kiuchumi na Michezo kila tukio/stori
inayonifikia wakati wowote ukijiunga na mimi kwa kubonyeza…..FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.
|
No comments:
Post a Comment