TANZIA:- Undani wa Kifo cha Mbunge JOHN KOMBA Aliefariki Dunia leo Februari 28,2015. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Saturday, February 28, 2015

TANZIA:- Undani wa Kifo cha Mbunge JOHN KOMBA Aliefariki Dunia leo Februari 28,2015.

Picha ya kwanza ya Marehemu komba mara baada ya kufariki dunia.

 Mbunge wa Mbinga Magharibi ,na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM,Mh. Kapteni John Komba amefariki Dunia leo Februari 28,2015 saa 10 jioni katika Hosptali ya TMJ Mikocheni,Jijini Dar es Salaam. 

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amethibitisha kutokea kwa kifo hicho, hata hivyo hakuwa tayari kuelezea kwa undani kwa madai kuwa taarifa hizo zimemfikia sasa hivi.

Kwa Mujibu wa mtoto wa Marehemu Bw. Jerry Komba amesema kifo cha marehemu baba yake kimetokana na ugonjwa wa kisukari ambapo amedai kuwa sukari ilishuka ghafla akiwa nyumbani kwake Mbezi Beach, Dar es salaam.

"Ni kweli mzee amefariki dakika 50 zilizopita, alikuwa nyumbani amekaa lakini sukari ilishuka ghafla na baadaye kidogo alifariki" amesema Jerry Komba mtoto wa marehemu.
Marehemu Kapteni Komba.

Katibu wa mbunge huyo Bwana Gasper Tumaini amesema kuwa mbunge huyo alikimbizwa katika hospitali ya TMJ ambapo ndipo mauti yamemkuta.

Aidha Bwana Gaspaer Tumaini ameongeza kuwa mwili wa marehemu umehamishiwa katika hosptali ya Lugalo jijini Dar es salaam ambapo ratiba ya Mazishi bado haijafahamika.
...Komba enzi za uhai wake.

Kapteni Komba ambaye pia ni Mkurugugenzi wa Kikundi cha Maigizo cha Tanzania One Theatre (TOT),  ambacho kina kikundi cha taarabu na bendi  inayokwenda na mtindo wa Achimenengule, amekuwa akikisaidia sana chama chake, Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kampeni zake wakati wa uchaguzi kwa kutunga nyimbo za kuhamasisha wapiga kura na kushiriki kupiga live kwenye majukwaa ya kisiasa.

Enzi za uhai wake alitamani  sana na kufanya juhudi kubwa ili mtindo wa Achimenengule uwe wa kitaifa lakini ikashindikana,  na badala yake Watanzania sasa tuna muziki wa Mduara ambao umekuwa kama mtindo wa muziki wetu kwa sababu zifuatazo.

Kwanza, ni mtindo halisi wa Kitanzania uliochipuka kutoka mahadhi ya kimwambao ya Tanzania. Pili, ndiyo mtindo pekee uliowahi kutumiwa na bendi nyingi baada ya kuasisiwa na ‘mabingwa’ wa muziki wetu, wana Njenje, The Kilimanjaro Band.

Baada ya bendi hiyo kuuasisi, mtindo huo, tayari umepigwa na bendi kama TOT Plus, Chuchu Sound, Pamo Sound, Inafrika Band, wana mipasho kadhaa na mwanamuziki mahiri lakini asiyethamini kiwango chake kikubwa cha muziki, Bob Haisa.

Sababu ya tatu ni kwamba mtindo huo umekuwa wa kupigwa na bendi nyingi, vikundi vingi na wanamuziki wengi si kwa kulazimisha bali kwa mapenzi tu ya mashabiki wa muziki wa Tanzania.

Kapteni Komba awali alikuwa mwalimu wa shule ya msingi kabla ya kuingia jeshini na kuwa kiongozi wa kikundi cha maonesho cha jeshi na baadaye Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi akamshawishi aachane na jeshi na kujiunga na CCM wakati wa mfumo wa vyama mingi ulipoingizwa mwaka 1992.

“Mzee Mwinyi ndiye aliyenifanya niache jeshi wakati huo nikiwa na cheo cha ukapteni. Aliniomba nikisaidie chama kwa kuanzisha kikundi ambacho lengo lake lilikuwa kukipigia debe CCM,” aliwahi kusema hivyo Kapteni Komba.

Ameshiriki kampenzi za marais Ally Hassan Mwinyi, Benjamin William Mkapa na aliye madarakani hivi sasa, Jakaya Mrisho Kikwete. Alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi hadi kifo kinamchukua.

Licha ya siasa Kapteni Komba alikuwa anamiliki shule na pia alikuwa na biashara kadhaa.

Mwaka 2012 Komba aliwahi kupelekwa India kwa matibabu ambapo alifanyiwa upasuaji wa nyonga baada ya kupata ugonjwa uliosababisha mifupa kusagana sehemu hiyo ya nyonga.

Baada ya kurejea nchini alisema upasuaji huo ulichukua saa tano na ulifanyika katika Hospitali ya Apollo, India na alikanusha kuwa alikuwa na ugonjwa wa figo.Ugonjwa uliomuua haujajulikana ila mtandao huu unafuatilia kila hatua na utakujuza.

Marehemu Komba ameacha mjane, Bi Salome, ambaye ni mwalimu kitaalumu na watoto kadhaa. Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi- ameen!


UNGANA  NASI KATIKA  FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad