|
Na Kadama
Malunde, Shinyanga.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mwili wa Benadetha Steven (35), aliyefariki
dunia juzi January 03,2015, umefanyiwa matambiko ya kimila baada ya kupasuliwa na wembe ukiwa
kaburini na kuingiziwa kuku ndani ya tumbo lake ikiwa ni ishara ya kuondoa
mkosi.
Tukio hilo lilitokea juzi katika Mtaa wa Mapinduzi wakati waombolezaji wakiwa
hatua ya mwisho ya kumzika marehemu.
Lakini ghafla alijitokeza ndugu wa marehemu mwanamke kuwazuia waombolezaji,huku mwenyewe akiingia kaburini na
kufungua sanduku na kuanza kuchana tumbo la marehemu aliyekuwa akisumbuliwa kwa
muda mrefu na uvimbe tumboni.
Mashuhuda wa tukio hilo, walisema mwanamke huyo ambaye hakutaka kujitambulisha
jina kabila la Mkurya, aliupasua mwili wa marehemu kwa kutumia wembe kisha
kuchinja kifaranga cha kuku na kuumwagia damu baadaye kufunika jeneza na
kuruhusu maziko.
Walisema kabla ya tukio hilo, kulitokea mabishano kati ya waombolezaji na ndugu
wakitaka matambiko hayo yafanyike Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga alikokuwa
akitibiwa.
“Mgogoro ulianzia nyumbani hata kabla ya kwenda makaburini, wakati mazishi
yanaendelea ndipo ndugu mmoja wa marehemu akaingia kaburini akiwa amevaa mipira
ya mkononi (glovu), akiwa na wembe na boksi dogo lililokuwa na kifaranga cha
kuku na kuzuia waombolezaji wasitupe udongo kaburini.
“Ndugu huyo wa marehemu mwenye jinsia ya kike, aliingia kaburini baada ya
mchungaji kumaliza ibada ya mazishi na kuruhusu mwili wa marehemu ufukiwe ndipo
akaanza kuuchana kwa wembe, akachinja kuku kisha kummwagia damu na kumwingiza
kuku huyo kwenye tumbo la marehemu, akafunika jeneza na ndugu wakaendelea na
mazishi,” alieleza mmoja wa mashuhuda, Sijali Jumanne.
Jumanne
alisema ndugu wa marehemu waliamua kufanya hivyo wakiamini wanaondoa mkosi ili
kifo kama hicho kinachotokana na uvimbe tumboni kisitokee tena kwenye ukoo wao.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mapinduzi, Ayubu Daniel, alikiri kuwapo kwa tukio hilo na
kuongeza kuwa baada ya tukio alitoa taarifa polisi ambapo ndugu hao
wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi.
Hata hivyo, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ndala, Dickson Venance, alisema marehemu
alikuwa mgonjwa kwa muda mrefu na kwamba siku moja kabla ya mazishi kulikuwa na
mgogoro juu ya mazishi ya mwanamke huyo ambaye aliolewa bila kulipiwa mahari.
“Kabla ya mazishi nilisuluhisha mgogoro, ndugu wa marehemu walikuwa wanataka
mahari ya Sh milioni moja, kukawa na mvutano, wakakubaliana Sh 100,000, ndugu
wa mwanaume wakachangishana wakakubaliana kuzika, sikuwepo wakati wa mazishi
lakini nashangaa leo yamekuwa hayo,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha, amethibitisha tukio hilo
na kusema uchunguzi unafanyika.
|
No comments:
Post a Comment