KUTOKA BUNGENI JANUARI 28,2015:- Ni kuhusu Kikao cha Bunge la Tanzania Kuvurugika kutokana na vurugu za baadhi ya Wabunge. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Wednesday, January 28, 2015

KUTOKA BUNGENI JANUARI 28,2015:- Ni kuhusu Kikao cha Bunge la Tanzania Kuvurugika kutokana na vurugu za baadhi ya Wabunge.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bi.Anna Makinda leo Januari 28,2015 amelazimika kuahirisha kikao cha Bunge kilichoanza jana Januari 27,2015, baada ya vurugu zilizotokea  baada ya kutolewa kwa hoja binafsi kutoka kwa Mbunge na Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi, Bw.James Mbatia kuhusu Jeshi la Polisi Nchini kumshambulia Profesa Ibrahimu Lipumba jana JANUARI 27,2015 akiwa kwenye Maandamano .

Akizungumza katika Bunge hilo, Bw.Mbatia amesema kuwa kitendo cha Polisi cha kuwapiga raia wasiokuwa na hatia, kuwazalilisha Waandishi wa Habari na kupiga mabomu ya machozi kiasi cha kuwafanya watoto wadogo kuhangaika hakikubaliki.
 
Amesema Polisi wakiendelea kuachwa kufanya vitu vya uvunjifu wa Amani, Serikali haitatawalika hivyo ili kurejesha amani na imani ya wananchi kwa Serikali yao ni vema shughuli zote za Bunge zikaahirishwa kupisha mjadala wa hoja hiyo binafsi kwa lengo la kuinusuru nchi.

"Nimesikitishwa sana, Lipumba amepigwa, watoto wamepigwa, waandishi wa habari wamepigwa, na Polisi wakasema wamepewa maagizo
 

"Prof Lipumba ni Mwenyekiti wa chama chenye wabunge zaidi ya 30 na Mwenyekiti wa chama kinachoshiriki serikali ya Zanzibar, sasa kama yeye anafanyiwa hivi itakuwaje Wananchi wa kawaida?
 
“Mheshimiwa Spika naliomba bunge lako liahirishe shughuli zake ili leo tuweze kujadili suala hili la uvunjifu wa amani uliofanywa na  jeshi letu la polisi jijini Dar es Salam jana, wao wanasema kuwa wamepewa amri kutoka ngazi za juu tunataka serikali ituambie ni nani anayetoa amri hizi za kupiga watu wasiokuwa na hatia yeyote, " amesema Mbatia.
 
Baada ya kuwasilisha hoja hiyo asilimia kubwa ya Wabunge walisimama juu ishara ya kuunga mkono hoja hiyo lakini Spika wa Bunge,Bi.Anna Makinda akawaomba wakae ili aweze kutoa ufafanuzi kwa mujibu wa kanuni.
 
Spika Makinda aliwaeleza Wabunge hao kuwa suala hilo ni nyeti kwa sababu ni la kiusalama, ili kupata ufafanuzi zaidi anaiagiza Serikali kufikisha Bungeni hapo majibu ya hoja hiyo kesho Januari 29,2015 ili wabunge waweze kujadili.
 
Baada ya maamuzi hayo ya Spika Makinda, kelele zikasikika Bungeni huku Wabunge wakitaka kufanyika kwa mjadala huo leo leo, ndipo Spika alipoamua kuahirisha Bunge hadi saa kumi jioni ambapo pia kutokana na hoja kutokamilika liliahirishwa mpaka kesho Januari 29,2015 saa Tatu asubuhi.

 Kiongozi huyo wa upinzani inadaiwa alifika eneo ambako maandamano yaliyopangwa kufanyika Jumanne Januari 27,2015,yalikuwa yamepigwa marufuku, ingawa uongozi wa chama cha CUF unadai Profesa Lipumba alikusudia kuwashawishi wafuasi wake watawanyike kutii amri ya polisi ndipo akashambuliwa.

Wakati huo huo Profesa Lipumba amefikishwa mahakamani mjini Dar Es Salaam ambako amesomewa mashtaka ya kufanya maandamano bila kuwa na kibali.

Hata hivyo kwa muda Profesa Lipumba alikimbizwa hospitalini baada ya afya yake kudhoofika, ikidaiwa ni sababu ya kupigwa na polisi.

Hata hivyo alirejeshwa mahakamani baada ya kupata nafuu, na kesi yake imeahirishwa na itatajwa tena mahakamani tarehe 26 Februari 2015.

Ameachiwa kwa dhamana ya watu wawili kwa kiasi cha shilingi milioni mbili kila mmoja.


UNGANANASI KATIKA  FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad