UCHAGUZI (TAMISEMI) DESEMBA 14 na 21,2014:-Taswira ya Matokeo ya Jumla huku chama kipya cha ACT-Tanzania kikijitahidi kuliko hata baadhi ya Vyama vikongwe. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Thursday, December 25, 2014

UCHAGUZI (TAMISEMI) DESEMBA 14 na 21,2014:-Taswira ya Matokeo ya Jumla huku chama kipya cha ACT-Tanzania kikijitahidi kuliko hata baadhi ya Vyama vikongwe.


Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), imetangaza matokeo ya jumla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Desemba 14 na 21,2014 yakionyesha kuwa uungwaji mkono wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika maeneo ya mijini umeporomoka kwa kasi.

Katika uchaguzi huo, chama kipya cha ACT-Tanzania kimechomoza na kuviacha baadhi ya vyama vikongwe ambavyo havikupata hata nafasi ya ujumbe. 

Akisoma matokeo hayo jana,Desemba 24,2014 Mkurugenzi wa Uchaguzi wa TAMISEMI, Bw. Khalist Luanda alisema matokeo hayo yamekamilika kwa asilimia 99 kutokana na baadhi ya maeneo kutofanya uchaguzi kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo wagombea kufungua kesi mahakamani na baadhi ya wagombea kufariki dunia kabla ya uchaguzi.


Jumla ya vyama 15 vilishiriki uchaguzi huo vikiwamo CCM, Chadema, CUF, NCCR - Mageuzi, TLP, NLD, ACT, UDP na APPT- Maendeleo. Vingine ni Chauma, NRA, UMD na vitatu ambavyo havikuambulia kiti hata kimoja vya DP, Tadea na ADC.

MATOKEO.

Pamoja na CCM kuendelea kuongoza kwa ujumla, chama hicho kimeonekana kupoteza viti mijini na vijijini na kimeporomoka zaidi mijini.

Katika maeneo ya vijiji na vitongoji, chama hicho kimepata ushindi wa asilimia 79.81 (vijiji) na 79.83 katika vitongoji, wakati kwenye mitaa ambayo ipo sehemu za mijini kimeshuka zaidi na kupata asilimia 66.66.

Matokeo hayo yakilinganishwa na yale ya mwaka 1999, chama hicho kimepata asilimia 89.2 katika mitaa, asilimia 91 katika vitongoji na asilimia 91.6 katika vijiji.

MATOKEO YA VIJIJINI.

Idadi ya vijiji vyote Tanzania Bara vilivyotarajiwa kufanya uchaguzi ni 12,443 lakini umefanyika katika vijiji 11,750.


Matokeo ya vyama pamoja na asilimia katika mabano ni CCM 9,378 (79.8), Chadema 1,754 (14.9), CUF 516 (4.4), NCCR Mageuzi 67 (0.6) na TLP 10 (0.09).


Vingine ni UDP 14, ACT 8 (0.07), NLD 2 (0.02), (0.12) na NRA 1 (0.0001).

UCHAGUZI WA VITONGOJI. 

Jumla ya vitongoji vilivyotarajiwa ni 64,616 lakini vilivyopiga kura 60,688 huku CCM ikiendelea kuongoza kwa kupata vitongoji 48,447 (79.8), Chadema 9,145 (15.1), CUF 2,561(4.2), NCCR Mageuzi 339 (0. 6), ACT 72 (0.12, TLP 55 (0.1), UDP 54 (0.1), NLD 2 (0.02).

MATOKEO YA MITAA. 

Mitaa yote 3,875 nchini ilifanya uchaguzi na kukamilika kwa asilimia 100 huku CCM ikipata asilimia 66.66 baada ya kupata mitaa 2,583, ikifuatiwa na Chadema iliyopata mitaa 980 (25.3), CUF 266 (6.9), NCCR Mageuzi 28 (0.7), TLP 1 (0.03), ACT 12 (0.31), UDP 3 (0.08), NRA 1 (0.03) na UMD 1(0.03).

UKAWA YACHANUA .

Kwa matokeo hayo, inaonyesha kuwa vyama vinavyounda Ukawa vimeongeza nguvu katika maeneo mengi hasa mijini ambako kwa pamoja vimepata wenyeviti 1,275 ikiwa ni sawa na asilimia 32.18 ya mitaa yote.

Katika maeneo ya vijiji Ukawa wamepata jumla ya vijiji 2,339 ambayo ni asilimia 19.91 wakati kwenye vitongoji waliambulia 12,047 sawa na asilimia 19.87.

WAJUMBE VITI MAALUMU. 

Kwa upande wa wajumbe wa viti maalumu ambao safari hii wamepigiwa kura badala ya kutokana na uwiano wa kura, CCM ilipata asilimia 80.24, Chadema (14.8), CUF asilimia (4.31), NCCR asilimia (0.48), ACT (0.08) huku APPT Maendeleo, Chauma na NRA vyote vikipata mjumbe mmoja kila kimoja sawa na asilimia 0.0001.

UNGANANASI KATIKA  FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad