|
Ofisi ya
Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imetangaza matokeo
ya awali ya uchaguzi wa Serikali za mitaa Uliofanyika Desemba 14,2014,nchi
nzima yanayoonyesha kuimarika kwa upinzani.
Mkurugenzi
wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Bw. Khalist Luanda alisema jana Desemba
17,2014,kwamba wakati Chama cha Mapinduzi - CCM ikifanikiwa kupata ushindi wa
jumla wa mitaa na vijiji 9,406, kwa pamoja vyama vingine vya upinzani,
vimegawana nafasi 3,211.
Kwa ushindi
huo ,upinzani umeongeza viti 1,981 ikilinganishwa na uchaguzi wa Serikali za
Mitaa uliopita mwaka 2009 ambao kwa ujumla, ulipata nafasi 1,230 za wenyeviti
wa mitaa na vijiji.
Kwa upande
wake, CCM imepoteza nafasi 2,636 za uenyekiti wa vijiji na mitaa ikilinganishwa
na uchaguzi wa mwaka 2009 ilipopata jumla ya viti 12,042.
Hata hivyo,
uchaguzi mwa mwaka huu (2014), umefanyika huku kukiwa na nyongeza ya mikoa,
wilaya, mitaa na vijiji katika baadhi ya maeneo nchini.
Akitangaza
matokeo hayo, Bw.Luanda alisema katika nafasi ya vijiji ambavyo matokeo yake
yamepokelewa ni jumla ya vijiji 9,047 ambapo CCM ilipata 7,290 sawa na asilimia
80.58, Chadema 1,248 sawa na asilimia 13.79 na TLP viwili sawa na asilimia
0.02.
Vyama vingine ni CUF vijiji 382 sawa na asilimia 4.22, NCCR-Mageuzi 14 sawa na
asilimia 0.15, NLD viwili sawa na asilimia 0.02 na ACT vinne sawa na asilimia
0.04.
Kwa upande wa mitaa 3,231, CCM ilipata 2,194 sawa na asilimia 67.90,
Chadema 828 sawa na asilimia 25.63, CUF 235 sawa na asilimia 7.27, NCCR
Mageuzi minane sawa na asilimia 0.25, TLP mmoja sawa na asilimia 0.03, NLD tisa
sawa na asilimia 0.28, UDP mmoja sawa na asilimia 0.03 na ACT mmoja sawa
na asilimia 0.03.
Akizungumzia upande wa vitongoji 42,824, alisema CCM ilipata 35,564 sawa na
asilimia 83.05, Chadema 5,970 sawa na asilimia 13.94, CUF 1,555 sawa na
asilimia 3.63, NCCR-Mageuzi 80 sawa na asilimia 0.19, TLP 11 sawa na asilimia
0.03, NLD kimoja sawa na asilimia 0.00, ACT 10 sawa na asilimia 0.02 na UDP 21
sawa na asilimia 0.05.
Matokeo hayo
yamejumuisha maeneo mengi ambayo CCM ilipita bila ya kupingwa.
Katika
matokeo hayo, CCM imeendelea kufanya vizuri katika mikoa ambayo imekuwa
ikitajwa kuwa ni ngome yake lakini kuna maeneo ambayo yalionekana kuyumba kwa
kuzolewa na upinzani.
Mfano wa
ngome ambazo CCM kimetikiswa zaidi ni Mkoa wa Dodoma katika wilaya za Kondoa na
Chemba ambako vyama vya CUF na Chadema vimefanya vizuri tofauti na uchaguzi
uliopita.
Kuhusu
nafasi ya mwenyekiti ambaye alisimikwa na wananchi kibabe katika Mkoa wa Arusha,
Luanda alisema TAMISEMI haitamtambua, bali atakuwa ni mwenyekiti wa kimila tu.
|
No comments:
Post a Comment