|
Sehemu ya
wazee wa Mkoa Dar es Salaam wakishangilia kuunga mkono kufukuzwa kwa Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maenedeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka jana. Picha na
Venance Nestory .
Hotuba ya
Rais Jakaya Kikwete kuhusu utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusu kashfa ya
Akaunti ya Tegeta Escrow imepokewa kwa hisia tofauti na wasomi, wanasiasa na
wananchi wa kawaida, wengi wakionyesha kutoridhishwa na hatua alizochukua.
Akizungumza
kwa simu baada ya hotuba hiyo Jana Desemba 22,2014, Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe alisema:- kitendo chake cha kuwatetea waliohusika katika kashfa
hiyo ya uchotwaji wa Sh306 bilioni kitakigharimu chama chake cha CCM siku
chache zijazo.
Alisema
kuachwa kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu
Mkuu wa wizara hiyo, Eliakimu Maswi si cha kupongezwa kwa sababu viongozi hao
ndiyo wahusika wakuu wa kashfa hiyo.
“Ameonyesha
kuwa kazi iliyofanywa na Bunge, ikiwahusisha mawaziri aliowateua waliotumia
uchunguzi uliofanywa na vyombo vya Serikali ni bure kabisa. Hotuba yake ina
maana kuwa uchunguzi wa Ikulu ndiyo unaotakiwa kuaminika.”
Huku
akionyesha kukerwa na jinsi Rais Kikwete alivyokuwa akiyarudiarudia maazimio ya
Bunge, Mbowe alisema katika hotuba yake, Rais Kikwete amekiri kuwa miamala yote
ya fedha iliyofanyika katika benki ilikuwa halali, kitu ambacho si kweli.
“Profesa
Tibaijuka ametolewa kafara tu. Huyu alikuwa katika tawi tu la kashfa ya escrow,
wahusika wakuu walikuwa ni Muhongo na Maswi ila wameachwa. Rais anatetea watu
badala ya kuwachukulia hatua. Hakika anazidi kuchochea moto,” alisema.
Aliongeza,
“Tunaitakia CCM maisha marefu na Rais Kikwete ili siku moja waje waone jinsi
kauli ya Rais kuhusu escrow itakavyoitafuna CCM. Inakuwaje Rais anashindwa
kusoma hisia za Taifa juu ya jambo hili?”
Wakati Mbowe
akieleza hayo, wasomi mbalimbali nchini wamepongeza hatua iliyochukuliwa na
Rais Kikwete huku wakiwashauri viongozi waliotajwa katika maazimio ya Bunge
kwamba mamlaka za uteuzi ziwawajibishe, wajiuzulu wenyewe kabla ya majibu ya
uchunguzi dhidi yao hayajatoka.
Mwenyekiti
wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema kauli,- hotuba na hatua za Rais Kikwete ni
kuwapaka Watanzania mafuta kwa mgongo wa chupa.
“Kimaadili,
viongozi wote waliotajwa kuhusika kwenye sakata la escrow walipaswa kujiuzulu.
Rais alistahili kuwaagiza waachie ngazi na wasipofanya hivyo, awawajibishe.
Siyo kupaka watu mafuta kwa mgongo wa chupa kama alivyofanya kwenye hotuba
yake.”
Alisema
Taifa liko katika hali tete, huku wahisani wakisimamisha misaada ya
kimaendeleo, lakini Rais haonekani kuchukua hatua madhubuti siyo tu kurejesha
imani ya wananchi na wahisani kwa Serikali, bali kunusuru nchi.”
Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe alisema,-
“Nimemsikiliza Rais, ninachoweza kusema ni kwamba maazimio yale hayakuwa ya
Zitto Kabwe, PAC, CAG au PCCB. Yalikuwa ni ya Bunge zima. Bunge la vyama vyote
kikiwamo chama cha Rais Kikwete yaani CCM.
“Sisi kama
Bunge tulitoa maazimio yale kwa maridhiano, uzalendo na bila kutaka kumwonea
mtu yeyote. Suala hili sasa naliacha kwa wananchi. Bunge limefanya kazi yake na
Serikali ambayo ndiyo tulikuwa tunasubiri maamuzi yake imeamua hivyo. Wananchi
wataamua wenyewe,” alisema.
Mbunge wa
Kigoma Kusini (NCCR- Mageuzi), aliyeibua sakata la escrow bungeni, David
Kafulila alisema:- “Rais amekwepa majukumu yake katika kuwachukulia hatua
wahusika. Maazimio ya Bunge yalitaka mamlaka ya uteuzi ichukue hatua dhidi ya
mawaziri, yeye ndiye aliyewateua iweje amwache Profesa Muhongo?”
Alisema Rais
Kikwete alitengua uteuzi wa mawaziri waliong’olewa kutokana na kashfa ya
Operesheni Tokomeza na kuagiza uchunguzi ufanywe dhidi yao, huku akihoji iweje
kwa Profesa Muhongo uchunguzi ufanyike huku akiwa bado waziri.
“Rais
anasema fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow zilitolewa kwa amri ya Mahakama,
sasa iweje fedha zitolewe wakati bado kulikuwa na mvutano kati ya Tanesco na
IPTL, ambao katika hotuba yake pia amekiri kuwa ulikuwepo?” alisema.
Kafulila pia
aliponda kitendo cha Rais Kikwete kusema kutaifisha mitambo ya IPTL ni
kukimbiza wawekezaji, wakati tayari amekiri kuwa suala la IPTL na PAP lina
utata mkubwa.
Mhadhiri wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema:- “Rais amejitahidi
kufafanua suala hili, hasa juu ya fedha za escrow ni za Serikali au IPTL na
kuhakikisha utawala wa kisheria unafanya kazi ipasavyo kulingana na maazimio ya
Bunge.”
Kuhusu
Profesa Tibaijuka, Dk Bana alisema uamuzi uliochukuliwa dhidi yake ni sahihi
kwa sababu alipewa fedha kupitia akaunti yake binafsi na kwamba kitendo chake
cha kukanusha kuhusika na suala hilo kupitia vyombo vya habari pia kilimponza.
Profesa
Kitila Mkumbo wa UDSM alisema:- “Profesa Muhongo anatakiwa kuachia ngazi. Kauli
ya Rais kwamba ‘anamweka kiporo’ maana yake anamtaka ajiuzulu bila aibu kama
iliyomkuta Profesa Tibaijuka. Rais hakuyadharau maazimio ya Bunge kama viongozi
wengine walivyoyadharau. Wote waliotajwa katika ripoti ile wanatakiwa kuachia
ngazi na si kusubiri mpaka kutimuliwa.”
Profesa wa
Chuo Kikuu Ruaha, Gaudence Mpangala alisema:- “Maamuzi yake hayakutarajiwa na
wananchi, ripoti ya uchunguzi ya CAG imebainisha kuwa fedha za escrow ni za
umma, sasa kama ni za IPTL uchunguzi wa nini?”
|
No comments:
Post a Comment