 |
UTAPIAMLO
unaosababishwa na ukosefu wa lishe bora na matunzo sahihi unaendelea kuwa
sababu ya watoto kudumaa na kutishia maisha yao.
Wakati nchi
yetu kupitia mikakati mbalimbali ikiendelea kupambana na tatizo hilo, Shirika
la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) linabainisha kuwa tayari nchi 63 duniani
zinazoendelea zimefikia malengo ya Milenia katika vita dhidi ya utapiamlo mkali
ifikapo mwaka 2015.
Waziri wa
Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, anatahadharisha kuwa ni jambo
la fedheha kubwa kwa nchi yetu kuendelea kukabiliwa na tatizo la udumavu
unaosababishwa na ukosefu wa lishe bora na matunzo sahihi wakati kimsingi
hatuna tatizo kubwa la chakula.
Kadhalika
anasema ni jambo lisilovumilika kuendelea kupoteza maisha ya watoto 130 kila
siku nchini kutokana na kukosa lishe bora.
Anasema lishe duni inaathiri kwa
kiasi kikubwa ukuaji wa kiakili wa watoto na hivyo kupunguza uwezo wa kufanya
vizuri shuleni, hali ambayo pia inapunguza ufanisi katika maisha ya utu uzima
wake.
Waziri Chiza
anayasema haya katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Mkoa wa
Katavi, Dk Rajab Rutengwe, katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Chakula
Duniani yaliyofanyika kitaifa Oktoba 16 mwaka huu katika Mji wa Mpanda.
Anakumbusha
kuwa wakati tunapoadhimisha Siku ya Chakula Duniani, hatuna budi kujikumbusha
kuwa madhara makubwa yanaweza kutokea katika ukuaji wa kimwili na kiakili kwa
mtoto ikiwa lishe bora haitazingatiwa.
Kwamba tangu
mimba inapotungwa mjamzito anatakiwa apate lishe bora na baadaye mama na
mwanawe waendelee kupata lishe bora hadi mtoto anapotomiza angalau umri wa
miaka miwili.
“Hivyo ni
jambo la msingi kwetu sote tukaelewa kuwa tunapoongeza uzalishaji wa mazao ya
chakula na biashara, hatuna budi kuweka mkazo mkubwa katika kuboresha lishe ya
familia zetu. Itakuwa haiingii akilini iwapo ongezeko la uzalishaji haliwezi
kwenda sambamba na upunguzaji wa tatizo la utapiamlo na kudumaa kwa watoto,”
anasisitiza.
|
Karibu kwenye familia
ya Makonda Blog na uzipokee Picha/Habari zote kwa kutumiwa Mchana /Usiku
baada tu ya kujiunga kwa kubonyeza hapa mtu wangu >>>BONYEZA
HAPA.>>>Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.
Copy n Win at:
http://bit.ly/copyandwin
No comments:
Post a Comment