TANZANIA:- Watu 7 wauawa kufuatia imani za kishirikina wilayani Kasulu mkoani Kigoma. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Friday, October 10, 2014

TANZANIA:- Watu 7 wauawa kufuatia imani za kishirikina wilayani Kasulu mkoani Kigoma.

Watu saba wameuawa kinyama na nyumba zaidi ya 20 kuchomwa moto kwenye kijiji cha Murufiti, wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, nchini Tanzania, baada ya kundi la watu kuwavamia, kuua na kuchoma moto miili yao kwasababu za kishirikina. 

Utakumbuka, Rais wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye amekua akiwataka raia wake kuzingatia amani na usalama, lakini katika baadhi ya mikoa raia wamekua wakiwaua wenzao kwa imani za kishirikina.

Habari zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma,Mohamed Jafari, zinasema vurugu hizo zilitokea juzi October 08,2014,usiku na watu waliouawa, walikuwa wakituhumiwa kujihusisha na ushirikina.

Kufuatia hali hiyo watu 18 akiwemo Mwenyekiti wa Kijiji cha Murufiti, Evarist Kuhaya (56) wanashikiliwa na Polisi. 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kigoma, Mohamed Jafari alitaja waliouawa kuwa ni John Muvumba (68), Elizabeth Kaje (55), Vincent Ntiyaba (42), Herman Ndabiloye (78), Redampta Mdogo (60) na Ramadhani Kalaliza (70).

Alisema nyumba 20 zimeharibiwa ambazo kati yake, 18 zimechomwa moto na kuteketea na zilizobaki, zimebomolewa.

 Tunaendelea na msako mkali wa kutafuta wengine ambao walihusika na tukio hili na kati yao yumo mganga wa jadi, Faustino Ruchagula ambaye taarifa zinaonesha alihusika katika masuala ya kupiga ramli hivyo kuchochea hasira za wauaji,” alisema Kamanda Mohamed.

Waandishi wa habari waliofika eneo la tukio, walishuhudia taharuki katika kijiji hicho kutokana na watu wenye umri mkubwa kukikimbia kwa hofu ya kushambuliwa kama wenzao waliopoteza maisha.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Murufiti, Ogeni Gaspar alisema kuwa kabla ya mauaji, watu waliotekeleza unyama huo walipiga mbiu kukusanya wananchi. Kwa mujibu wa ofisa huyo, watu waliokusanyika walipeana maelekezo ya kutekeleza jambo hilo.

Alieleza kwamba kutokana na hali hiyo alilazimika kutoa taarifa Polisi lakini walichelewa na wakati wanawasili kijijini hapo walikuta maafa yameshatokea.

Mtendaji huyo wa Kijiji alisema tukio hilo si la kwanza kwani mwanzoni mwa mwaka huu, mzee mmoja ambaye hakutaka kumtaja jina lake alifukuzwa kijijini
 hapo na nyumba yake kuchomwa baada ya kuhusishwa na vitendo vya ushirikina.

Lakini hakuna jambo lisilokuwa na chanzo, nina uhakika kuwa waliofanya tukio lile la awali ndio wanahusika na uchochezi wa tukio hili la juzi kwa sababu tayari wameshabainishwa na wanajamii lakini majina yao yamehifadhiwa,” alisema.

Akizungumzia tukio hilo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Murufiti, Filbert Mkwangu alisema licha ya baadhi ya watu kukikimbia kijiji hicho, pia hali ya mahudhurio shuleni kwake imeshuka jambo alilosema linaweza kuathiri taaluma kwa wanafunzi.
Karibu kwenye familia ya Makonda Blog na uzipokee Picha/Habari zote kwa kutumiwa Mchana /Usiku baada tu ya kujiunga kwa kubonyeza hapa mtu wangu >>>BONYEZA HAPA.>>>Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad