MDAHALO WA MAENDELEO NGARA:- Soma Yaliyojiri kwenye mdahalo uliohusu mada ya ukosefu wa ajira na umasikini kwa vijana wilayani Ngara mkoani Kagera Agosti 15,2014. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Saturday, August 16, 2014

MDAHALO WA MAENDELEO NGARA:- Soma Yaliyojiri kwenye mdahalo uliohusu mada ya ukosefu wa ajira na umasikini kwa vijana wilayani Ngara mkoani Kagera Agosti 15,2014.

Mdahalo huo ulioandaliwa na chuo cha mafunzo ya taaluma ya madini cha SEHKASA kilichopo wilayani Ngara umefanyikia katika ukumbi wa City Life Ngara leo tarehe 15/08/2015 kuanzia saa saba mchana hadi saa kumi na mbili jioni. Wadau mbalimbali wa maendeleo wilayani Ngara wametoa hoja zao juu ya mada hiyo.

Mdahalo huo ulioendeshwa na Ndugu Venant Verdian kama mwenyekiti ulikuwa na wachangia mada wakuu wanne ambao ni Dr. Gresmus Sebuyoya, Mr. Alex Gashaza, Bi. Heren na Mr. Issa Samma. 

Aidha walikuwepo wachokonoa mada ambao ni Mr. Josias Charles ( mwanachuo wa chuo kikuu cha Dodoma) , Mr. Falisi Addy Mohammed (mwenyekiti wa vijana wa CCM wa wilaya) , Dr. Peter Bujali ( kutoka Human Development Trust) na Mr. Brayan.

Pia mdahalo huo ulimwarika mkurugenzi wa wilaya ya Ngara ambapo amewakirishwa na Mr. Osward Rujuba. Aidha hadhira ya mdahalo huo ilikuwa na wanachuo na wale waliohitimu vyuo vikuu mbalimbali hapa nchini, wanachuo wa chuo cha madini SEKHASA, wanafunzi kutoka RHEC Secondari, walimu kutoka shule mbalimbali, waandishi wa habari  na wadau mbalimbali wa maendeleo yaani wajasiriamali.

Mdahalo huo uliolenga zaidi ukosefu wa  ajira kwa vijana na jinsi gani ya kutatua tatizo hilo na la umasikini wilayani Ngara ulianza kwa utambulisho na kufatiwa na risala fupi ya chuo kikuu cha SEKHASA ambapo risala hiyo imeeleza kwamba chuo hicho kimesajiriwa na veta hivyo kinatoa elimu hiyo kwa wakazi wa Ngara na wengine kutoka nje ya wilaya hii. 

Aidha risala imeeleza kuwa chuo kinatoa course nne mpaka sasa juu ya elimu ya madini na mafanikio ya chuo hicho ni kwamba namba ya wanachuo imeongezeka kulinganisha na kipindi cha nyuma na kimefanikiwa kutoa wahitimu 20 mwaka huu. 

Katika risala hiyo imeeleza kwamba changamoto kubwa ni wakazi wa Ngara hawaendi kusoma katika chuo hicho ili kujipanua kielimu na kupata fursa ya ajira ambapo mpaka sasa ni mhitimu mmoja tu kutoka Ngara aliyehitimu katika chuo hicho.





Mdahalo 

Mdahalo umeanza kwa watoa mada wakuu wanne kuchangia kama ifuatavyo:-

Dr. Gresmus Sebuyoya

Ameanza kwa kutaja aina mbili za umasikini ambazo ni umasikini wa kupindukia na ule umasikini wa kawaida wa kukosa mahitaji muhimu. 

Amesema hali ya umasikini wilayani Ngara na kokote nchini kunasababishwa na mgawanyo wa miundombinu na maliasili usiokuwa na usawa (unequal distribution of resources) ambapo ametolea mfano hospitali kuu zote zipo eneo moja wilaya nzima. 

Pia ameongela mgodi wa madini wa kabanga nickel kuwa upo haufanyi kazi hivyo unachangia umasikini wilayani Ngara, na zaidi ameongelea suala la matumizi ya mipaka yetu ili kuweza kuuza mazao nchi za jirani za Rwanda na Burundi ili kujipatia kipato cha kuinua wananchi kiuchumi wilayani humo. 

Akimalizia na changamoto zilizopo amesema ukosefu wa utawala bora ndio chanzo cha umasikini wilayani Ngara huku akitolea mfano hospitali za wilaya zinakosa dawa hivyo kusababisha hali ya hospitali binafsi au maduka ya madawa kuwa bora kwa huduma ya afya kuliko hospitali hizo.

Mr. Issa Samma

Amesema utendaji kazi mzuri ndo unachangia upatikanaji wa ajira ambapo amesema kuna ajira zisizokidhi matarajio, ajira rasmi na kutokuwa na ajira kabisa ambapo amesema mfumo wa elimu hapa nchini ndio unapelekea ukosefu wa ajira kwa vijana hivyo kama mfumo wa elimu utarekebishwa vijana watapata ajira. 

Pia ameongelea matumizi mabaya ya fedha za mikopo zinazoletwa ili kusaidia vijana kujiajiri ambapo amesema fedha hizo hziwafikii walengwa wilayani humo na kupelekea vijana wasio na kazi kuwa wengi. 

Aidha amesema serikali inafanya mchakato utakaowawezesha vijana kuchukua mikopo kwa kutumia vyeti vya vyuo vikuu. Pia ameshauri halimashauri kuangalia tatizo hili la ajira kwa vijana kwa jicho pana. 

Mwisho ameshauri vijana kuwa suluhisho la tatizo hili kwa sasa ni vijana kujikita kwenye ujasiriamali ili kujiajiri na kujikwamua kwenye wimbi la umasikini.

Bi. Hereni Adirian

Amesema bila vijana hakuna maendeleo hivyo ili kutokomeza umasikini wilayani Ngara lazima vijana waangaliwe maana ndio wazalishaji wakuu na wadau wa maendeleo. 

Aidha amesema ukosefu wa ajira kwa vijana kunasababishwa na kutokuwa na elimu rasmi na isiyo rasmi ambayo itawasaidia kujikwamua kiuchumi. 

Mfano amesema vijana wanaoishia kidato cha nne wanarudi vijijini na kuwa mzigo kwa wazazi hali inayopelekea ongezeko la umasikini wilayani humo. 

Ameshauri kwamba ili kuondokana na tatizo hili inatakiwa vyuo vya ufundi stadi viongezeke ndani ya wilaya ya Ngara.

Mr. Alex Gashaza

Ameanza kwa kusema kuwa kuna aina kuu mbili za ajira ambazo ni ajira rasmi na ajira zisizo rasmi(ujasiriamali). 

Hivyo vijana wote wasomi na wasio wasomi wana wajibu wa kujihusisha na ajira hizo ili kutokomeza umasikini wilayani Ngara. 

Amesema wilaya inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa ajira hivyo ili kuondokana na tatizo hilo  kasi ya uzalishaji inabidi iongezeke huku kukiwepo na ongezeko la viwanda ili kuwapatia vijana ajira. 

Pia amesema sekta ya kilimo na maliasili hazijatumiwa ipasavyo katika kuinua uchumi wa vijana wilayani Ngara. 

Aidha Gashaza amesema halimashauri ya wilaya ya Ngara imeandaa mpango wa agriculture profile utakaosaidia kuinua fursa za ajira kwa vijana wa wilaya hiyo.





Waliofata kuchangia ni wachokonoa mada mbapo wamechangia kama ifuatavyo:-

Mr. Godfrey Brayan

Amesema ukosefu wa ajira kwa vijana umesababishwa na ukosefu elimu bora ambapo amesema mfumo wa serikali umejikita sana kwenye siasa badala ya kuangalia hali ya wananchi. 

Pia ameongelea suala la vijana kujikita zaidi kwenye mitandao ya kijamii mfano facebook kuwa kumewapelekea kubweteka hivyo kushindwa kujihusisha na uzalishaji mfano kilimo. 

Aidha amesema vijana wanachagua kazi hali inayopelekea wengi kukosa ajira na pia wale walioajiriwa hawajitumi kazini huku akiongelea kuwa suala la michezo wilayani Ngara limesahaulika na pia haliendeshwi ili kuwasaidia vijana kujiajiri kupitia michezo mbalimbali.

Mr. Josias Charles

Amesema tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana linasababishwa na vijana wenyewe kutegemea serikali kuwainua kiuchumi na hivyo kutojihusisha na ujasiriamali. 

Pia ameongelea kuwa huduma za kijamii bado ni changamoto hasa maeneo mbalimbali ya wilaya hii hivyo inakuwa vigumu kutatua taizo la umasikini wilayani humo.

Mr. Falisi Addy

Amesema tiba ya umasikini na ukosefu wa ajira kwa vijana wilayani Ngara ni kumubana Mkurugenzi wa wilaya ili aweze kuwaeleza vijana fursa mbalimbali za ajira. 

Amesema kuwa vijana wengi wanakosa ajira sababu hawajui fursa za ajira hali inayosababishwa na halimashauri y awilaya. 

Pia amesema ili kuondoa tatizo la ajira na umasikini kwa vijana succos ya vijina ina hitajika ambapo amesema kuwa kuna asilimia tano ya mapato ya wilaya ambayo halimashauri inatakiwa ikusanye na kuwapatia vijana lakini bado kwa wilaya ya Ngara hilo halijafanyika kuwasaidia vijana wa wilaya hiyo na haijurikani hiyo 5% inafanya shughuli gani kama haiwasaidii vijana wa wilaya husika.

Baadhi ya wachangiaji kutoka kwenye hadhira

Mr. Ezra Essau (mhitimu wa shahada ya sociologia na kazi za jamii kutoka chuo kikuu cha Mwenge)

Amesema tatizo la ajira kwa vijana linasababishwa na vijana wa wilaya ya Ngara kutegemea zaidi ajira rasmi (white collar jobs) na kutojihusisha na ujasiriamali. 

Akitolea mfano wa kikundi cha vijana wa kabanga cha matunda ambacho ni kikundi cha wajasiriamali wanaotegemea kilimo ameongelea jinsi kilivyoendelea hadi kuanzisha succos ya kukopesha mikopo ya fedha kwa watu mbalimbali ambapo leo hii hata wasomi wanakopa mikopo kwenye kikundi hicho cha vijana wakulima wa kawaida. 

Hivyo amesisitiza kuwa mabadiliko yanaanzia kwa mtu mmoja mmoja na baadae kwenda hadi kundi kubwa hivyo kila kijana anapaswa kubuni mbinu ya kujiajiri ili kujikwamua kiuchumi. 

Akiongelea mfumo wa demokrasia Tanzania amesema siasa imechangia kuua maendeleo ya nchi hii ambapo viongozi tulionao kwa sasa wana uzalendo wa vyama na sio uzalendo wa nchi. 

Pia amegusia suala la powertiller moja lililoletwa wilayani Ngara ili kuinua kilimo cha mpunga huku akihoji je powertiler moja litatosheleza wakulima wote? Na je hivi kweli wakulima wote wataweza kuja kujifunza kutumia powertiller hilo moja lililopo halimashauri kutoka sehemu mbalimbali za wilaya? Na je, wakijifunza watapataje powertiller la kuendeleza kilimo kwa yale waliojifunza? 

Zaid amesema powertiller hilo limeletwa ili kiotewa na nyasi pale halimashauri na sio kusaidia wananchi. Zaidi amesema kuwa kama kijana wa Ngara aliyepata elimu ya jamii atajipanga ili kutumia fursa ya vipindi kupitia redio kwizera ili kuelimisha jamii yake juu ya mambo mabalimbali yanayokwamisha maendeleo wilaya Ngara.

Mr. Chegere

Huyu ni mratibu wa mikopo kwa vijana wilayani Ngara, amesema mwaka huu amezunguka na mkuu wa wilaya maeneo yote ya wilaya kuhamasisha vijana kuhusu mikopo lakini cha kusikitisha hakuna aliyejitokeza kuchukua mikopo. 

Baadae ilitolewa milioni 200 na serikali baada ya kupitishwa kwa bunge la bajeti mjini Dodoma ndipo uhamasishaji ulianza upya na vikundi 30 vilipatikana kuchukua mikopo hiyo. 

Amesema usajiri wa vikundi unaendelea kwenye ofisi ya mikopo iliyopo eneo la community center mjini Ngara. 

Ili kupata mkopo lazima kikundi kiwe na vijana wenye idadi ya kuanzia watano kwenda juu na pia kikundi hicho sharti kiwe kinajihusisha na uzalishaji mali na kisajiliwe na wilaya ambapo mdhamini mkuu ni mtendaji wa kata wanakotoka wanakikundi hicho. 

Katika mkopo huo hakuna mdhamana wa nyumba wa mali yoyote na usajiri ni bure hivyo vijana wanakaribishwa kuchukua mikopo ofisi hapo.

Aliyehitimisha mdahalo ni muwakilishi wa mkurugenzi wa wilaya ya Ngara

Afisa elimu wa wilaya Ndugu Osward Rujumba

Ameanza kwa kusema kuwa hakuja kujibu maswali ya mdahalo bali amekuja kuchangia mada ya mdahalo hivyo japo mambo mengi yapo kisiasa ila changamoto zilizopo ni jukumu lake na wananchi wote kuzitatua. 

Amesema Ngara tuna vyuo vya ufundi mfano Remela na Sehkasa ila vijana hawaendi kusoma ili kujipatia ujuzi wa kuwainua kiuchumi. 

Pia amesema ili kuboresha elimu ya sayansi wilayani Ngara kuna mpango wa kuhakikisha kila shule inakuwa na maabara ili wanafunzi wajifunze kwa vitendo. 

Aidha amesema suala la asilimia tano (5%) inayotolewa kwa vijana kutoka halimashauri atalipeleka kwa mkurugenzi maana yeye hana majibu yake. 

Na pia akijibu hoja ya mchangiaji kutoka hadhira aliyehoji juu ya kutokuwepo kwa mashamba darasa wilayani Ngara amesema mashamba darasa yapo ila hana takwimu kamili yapo wapi na ni mangapi. 

Na mwisho amesema suala la kuanzisha taasisi binafsi litasaidia kukwamua vijana katika tatizo la umasikini.

Mwisho 

Waliohudhuria wamewaomba waandaaji kuwa mdahalo huu usiwe mwisho leo bali uandaliwe kila mwaka na pia waliohudhuria wawe mabalozi wa kuhamasisha na wengine kushiriki midahalo mbalimbali. 

Hali halisi ni leo ambapo vijana waliojitokeza kwenye mdahalo ni wachache sana hivyo ni vigumu jamii ya Ngara kubadilika kama hakutakuwa na msukumo wa mtu binafsi kuruhusu mabadiliko ya maendeleo.

Imechapishwa na (Mwana wa Makonda na  Ezra Essau )

UKIONA TUKIO LOLOTE LINATOKEA USISITE KUTUTUMIA PICHA KUPITIA WhatsApp:- 0789-925-630.
 
 
Like ukurasa wetu wa facebook  ili habari ziwe zinakuijia punde tu zinapoweka kwenye mtandao huu BONYEZA HAPA

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad