BBC Idhaa ya Ulimwengu, imezindua ofisi zake
jijini Dar es Salaam. Ofisi za Dar es Salaam zina studio ambazo zinatumika
kuandaa matangazo maarufu ya redio ya asubuhi, Amka na BBC, na pia kuendesha
tovuti ya bbcswahili.com.
Katika kuadhimisha uzinduzi huo, vipindi
vingine viwili vya BBC Idhaa ya Kiswahili, Dira ya Dunia ya redio na ya TV
vitaandaliwa kutoka Dar es Salaam katika siku hiyo ya Jumatatu Agosti 11.
Ufunguzi wa ofisi za Dar es Salaam ni matokeo
ya mikakati ya BBC Idhaa ya Ulimwengu ya kuhamisha uandaaji wa vipindi vya
redio na tovuti kutoka London kwenda Afrika Mashariki.
Ofisi mpya ina vifaa vya kisasa vinavyoweza
kutayarisha vipindi vya redio, TV na huduma za habari kwa njia ya simu za
mkononi. Amka na BBC, kipindi cha nusu saa ambacho hutangazwa Jumatatu hadi
Ijumaa humulika matukio na taarifa zitakazojiri katika siku, sasa kitaandaliwa
Dar es Salaam na watayarishaji na watangazaji 15.
Ofisi mpya pia zina watayarishaji wanaoandaa
taarifa mbalimbali za kanda ya Afrika Mashariki na Kati kwa ajili ya vipindi
vya TV vya Focus on Africa na Dira ya Dunia. Mkuu wa Habari wa BBC Idhaa ya
Ulimwengu Nikki Clarke amesema:
"Uzinduzi wa ofisi zetu za Dar es
Salaam ni hatua kubwa katika safari yetu iliyoanza muda mrefu kidogo, katika
kuwapa wanachotaka wasikilizaji katika nchi zinazozungumza Kiswahili, na ambao
husikiliza BBC wanapotaka kupata taarifa wanazoziamini na zenye uhakika.
Takriban watu milioni 12.4 - ambao ni kama nusu ya idadi ya watu wazima nchini
Tanzania, husikiliza matangazo ya redio ya BBC kila wiki.
Na sasa moja ya kipindi maarufu cha BBC, Amka
na BBC, kimekuja karibu zaidi na wasikilizaji." Ofisi ya Dar es Salaam,
ina studio mbili za redio ambazo zinaweza kutumika na hadi watu sita kwa wakati
mmoja, na hivyo ni muafaka kabisa kwa kipindi kichangamfu cha Amka na BBC kwa
ajili ya mijadala na mahojiano ya kuvutia.
Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Ali Saleh
anasema : "Ofisi mpya zinatoa nafasi bora kabisa kwa watayarishaji wa BBC
nchini Tanzania kuimarisha ukusanyaji wa habari na kutoa taarifa kutoka katika
eneo la Afrika Mashariki na Kati.
Amka na BBC itakuwa na uwezo mkubwa zaidi
kutoa taarifa na habari mchanganyiko, za Afrika Mashariki na pia za dunia,
pamoja na mahojiano ya moja kwa moja na watu mbalimbali, lakini pia makala na
habari za kijamii." Idhaa ya Kiswahili ya BBC imekuwa kitovu cha hatua ya
BBC Idhaa ya Ulimwengu ya kuimarisha kuwepo kwake katika sekta ya habari barani
Afrika.
Baada ya ufunguzi wa ofisi ya Nairobi mwaka
1998, BBC Idhaa ya Ulimwengu ilikuwa shirika la kwanza la habari la kimataifa
kuwa na kituo cha uandaaji habari barani Afrika. Mwaka 2006 Amka na BBC
ilihamishwa kutoka London kwenda Nairobi, na BBC Idhaa ya Ulimwengu, kwa mara
nyingine tena ikawa shirika la kwanza la kimataifa la habari kuandaa na
kutangaza vipindi kutoka barani Afrika.
Katika hatua ya kuhamisha utayarisaji wa
vipindi na taarifa za kwenye tovuti, kipindi maarufu cha jioni cha redio, Dira
ya Dunia sasa kinatayarishwa Nairobi. Mwisho// Kwa taarifa zaidi wasiliana na
afisa wa idara ya mawasiliano ya BBC Idhaa ya Ulimwengu - Lala Najafova,
lala.najafova@bbc.co.uk.
Kwa wahariri: BBC Idhaa ya Ulimwengu ni
shirika la utangazaji la kimataifa lenye idhaa nyingi za lugha mbalimbali
zinazotoa huduma ya matangazo ya redio, TV, kwenye mtandao wa internet na pia
simu za mkononi. BBC Idhaa ya Ulimwengu hutumia njia mbalimbali kuwafikia
wasikilizaji wake wapatao milioni 191 duniani kote. BBC huwafikia watu milioni
265 duniani kote kila wiki kwa huduma zake kutoka BBC Idhaa ya Ulimwengu, BBC
News TV na bbc.com.
|
No comments:
Post a Comment