Anavyotusimulia Agnes, "Wazazi wangu walinikalisha
na kuniarifu kuwa sikua jukumu lao tena. Walitaka nijitenge nao na kuanza
maisha kivyangu.Mambo yalikwenda haraka kinyume na matarajio yangu wakati
mwanamme huyo ambaye simfahamu alilipa mahari kwa wazazi wangu.”
“Sikua na usemi
wowote kwenye jambo hilo,” Agnes alisema haya akiwa na simanzi tele na
kububujikwa na machozi."Sikuchagua kuishi hivi na sina raha"
Agnes alikubali kuzungumza nasi mradi tusimtambulishe.
Aidha BBC iliweza kuzungumza naye kwani mumewe hakuwepo.
Tulipopatana naye, alikuwa anatekeleza majukumu yake ya
kila siku, kuosha vyombo, kufanya usafi kwa ujumla na hatimaye kujiandaa
kutayarisha chajio.
Alionekana mwenye wasiwasi na masikitiko, na haikuwa
vigumu kubainisha kuwa alionekana kukata tamaa- visigino vyake vilikuwa
vimepasuka, na vipodozi vyake kufifia.
Kuozwa mapema na kwa lazima ni jambo la kawaida huko
Zambia, lakini utamaduni huu si wa ki-Afrka tu, bali ni tatizo la kimataifa .
Inakadiriwa kuwa wasichana milioni 14 wanalazimishwa
kuoleka kabla ya kufika miaka 18, kila mwaka. Kuamrishwa kuoleka wakiwa na umri
mdogo hukatiza utoto wao ghafla.
.....Umaskini ndio sababu kubwa ya wasichana kuolewa Mapema.....
|
Agnes anajaribu kwa udi na uvumba kuhepa mfumo huu mpya
wa maisha, lakini ana hofu kuwa wazazi wake watamkana iwapo atakwepa ndoa yake.
Umasikini na tamaduni huchangia pakubwa mila hizi ambazo
ni maarufu sana huko mashambani.
Wapinzani wa mila hizi wanadai kuwa wazazi huona mabinti
zao kama jinsi ya kupata fedha na mali.
Chief Chamuka VI wa Zambia, na mavazi yake ya kiasili –
vazi jekundu na kofia nyekundu ilyopambwa kwa manyoya- alihutubia wanakijiji
kuhusu hatari na athari za kuoza watoto mapema, na kuwataka wasichana wachanga
kuzingatia umuhimu wa masomo na kuenda shuleni.
“Kama chifu, nimechukua msimamo kuwa hakuna mzazi
atakayeamuru binti wa chini ya miaka 18 kuolewa. Yeyote akiukaye sheria hii
ataadhibiwa vikali.” Chifu alisema.
Viongozi wa kitamaduni wanaopigia debe kuolewa kwa
wasichana wachanga, hujawa na hamaki wanapoona wenzao wakibadilisha msimamo wao
na kupinga kuozwa kwa mabinti wachanga.
.....Chifu Chamuka amesema utamaduni wa ndoa za mapema
hazitakubaliwa. ....
|
Aghalabu, wanaopinga tamaduni hizi huchukuliwa kukiuka
mila zilizotumika tangu jadi na vizazi vilivyopita, lakini chifu hakulegeza
msimamo wake.
"Nahisi kuwa katika jamii kuna mila zilizo nzuri na
zingine mbovu- jambo hili lazima likome,” chifu alisema.
'Athari za kudumu'
Wanaolazimishwa kuoleka mapema huhisi athari hizo kwenye
maisha yao ya baadaye.
Beatrice Chikwekwe aliolewa akiwa 15, sasa ana umri wa
miaka 32.
"Nilijawa na hofu na kuchanganyikiwa siku yangu ya
harusi, hata sikuwa na fahamu ya nilichokua nikifanya,” Beatrice alisema.
“Nilipata mimba mwaka huo huo na nikapata matatizo nilipokuwa najifungua.
Karibu nipoteze maisha yangu”
Bi Chikwekwe sasa anasoma mwaka wake wa mwisho katika
chuo cha kilimo, baada ya kupoteza muda mwingi. Akilinganishwa na wengi ana
bahati kubwa kwani ni nadra kupata hatima kama ya Beatrice- nafasi ya kwenda
shule.
'Kuolewa kwa watoto Zambia.'
Ndoa za Mapema.
- 40% ya wasichana wanaoleka wakiwa miaka 18 au chini ya miaka 18- hii ni mojawapo ya asilimia kubwa Zaidi ulimwenguni.
- 9% wanaolewa wakiwa umri wa miaka 15 au chini ya miaka 15.
- Wasichana wasioelimika sana huwa na uwezekano mkubwa wa kuolewa mapema.
- Wasichana wanaozaliwa katika familia fukara huwa na uwezekano mara tano Zaidi kuolewa mapema, inapolinganishwa na wasichana wa familia tajiri.
- Kuolewa mapema ni maarufu sana mashinani au vijijini.
- Kundi la wanaharakati la “Wasichana sio mabi harusi,” (au Girls Not Brides kwa kimombo) linasema kuwa kuozwa kwa watoto huwanasa mabinti na familia zao kwenye “mzunguko wa ufukara.”
“Wasichana wanaooleka mapema hawapati elimu na nafasi za
kujikuza kiuchumu hivyo basi hukosa uwezo wa kuinua jamii zao kutoka kwa
umaskini,” kundi hili lilisema kwenye taarifa.
Graca Machel, mkewe hayati Nelson Mandela na mmojawapo wa
wanaharakati waliarifu BBC kuwa Mila hubuniwa na binadamu na zilizo hatari na
zenye athari mbaya lazima zibadilishwe. “Kama wazazi hatuna haki ya kulazimisha
watoto wetu kuchukua uamuzi flani,” Graca alisema.
Tunapaswa kubadili mtazamo wa familia na jamii kwa
wasichana na kuchukulia mtoto wa kike kama binadamu aliye na maazimio na
matarajio, na aliye ana uwezo wa kufuzu kama awezavyo mtoto wa kiume.
Inakadiriwa kuwa wasichana wanopata mimba kabla ya
kufikisha umri wa miaka 14 wana uwezekano mara tano Zaidi kufariki
wanapojifungua.
....Jamii zimeanza kuelimishwa kuhusu madhara ya ndao za
Mapema....
|
Tukirejea Chibombo, shirika la ufadhili ‘Plan
International Zambia’ linashirikiana na viongozi wa kitamaduni, serikali na
vikundi vinginevyo ili kunusuru wasichana kama Agnes kutoka kwa ndoa za
kulazimishwa.
Kwa mujibu wa msemaji wa shirka hilo, panapo ufukara
watoto huwa kwenye hatari ya kunyanyaswa. Tunafanya juhudi kuelimisha jamii
kuhusu haki za watoto na haki hizo zinazofaa kuheshimiwa.
Kwa sauti ya kutetemeka Agnes anahitimisha manung’uniko
yake.
"Saa zingine ni vigumu kutofuata masharti ya wazazi
wetu kwani ni ukosefu wa heshima, lakini hatuwezi kuruhusu watufanyie uamuzi
ambao una athari mbaya kwetu,” alisema.
"Lilikuwa azimio langu nimalize shule na kuwa muuguzi
lakini nadhani matarajio hayo hayatatimia kwani mume wangu hatoniruhusu
niendeleze masomo yangu.”
Utafiti
Na:-BBC Swahili.
No comments:
Post a Comment