Nesi wa
kituo cha afya cha Katoro, wilaya Geita mkoani Geita, Leah Mganga( 33) mkazi wa
katoro, anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa tuhuma za mauaji ya kichanga.
|
Tukio hilo
la kushangaza limetokea Julai 21,2014, majira ya saa tisa
usiku, wakati mama mmoja aitwaye Mariam Gekera (23) mkazi wa
Nyarugusu, alipofikishwa katika kituo hicho kwa ajili kujifungua na kisha
kupokelewa na nesi huyo ambaye alikuwa zamu kwa ajili ya kumhudumia.
Akizungumza
na waandishi wa habari kituoni hapo huku akibubujikwa na machozi ,mzazi huyo
alisema kuwa pamoja na kupokelewa na nesi huyo na kupimwa na
kuambiwa mimba imefikia kuzaliwa lakini huduma za kumsaidia ili ajifungue
salama zilianza kusuasua .
Mama huyo
alisema alifanikiwa kujifungua japo kwa shida yeye mwenyewe mtoto akiwa mzima
na analia, lakini kwa bahati mbaya damu zilimrukia nesi huyo kitendo ambacho
kilimkera nesi na kuanza kutoa matusi kwa mzazi huyo.
Kufuatia
hali hiyo nesi alikwenda kubadilisha vazi na kurudi na kubeba kichanga na
kuondoka nacho huku mzazi akiuliza mtoto anapelekwa wapi.
“Muda
mfupi nesi alirudi akiwa amekibeba kichanga hicho kwa mikono miwili na kusema “kichanga
chako ni kilo tatu na ni kivulana lakini kimekufa”.alisema mama huyo
Kwa upande
wake,Nesi Leah Mganga alisema taarifa zilizotolewa na mzazi huyo si za kweli na
kuongeza kuwa yeye alitoa msaada kama kawaida na baada ya kurukiwa alikwenda
kubadilisha vazi jingine na aliporudi alikuta kichanga kimekufa.
Mganga mfawidhi
wa kituo hicho Dk. Alex Bundala alikiri kuwepo kwa tukio hilo kwenye kikao cha
wajumbe wa serikali ya kijiji walichokuwa wamekiitisha mapema asubuhi ya Julai
22,2014,kwa ajili ya kuzungumzia tukio hilo.
Mwenyekiti
wa kijiji hicho Joel Mazemle pamoja na uongozi wake wamelaani kitendo
kilichofanywa na nesi na kuiomba serikali kuchukua hatua kali dhidi ya
mtuhumiwa huyo kwani ni vitendo vingi viovu vinavyofanywa na manesi
hao katika kituo hicho.
Jeshi la
polisi mkoani Geita limethibitisha kutokea kwa tukio na kusema mtuhumiwa
anashikiliwa kwa uchunguzi zaidi.
Na Valence
Robert-Geita.
No comments:
Post a Comment