Matukio ya
ukatili yameendelea kuibuka nchini baada ya kugundulika kwa mtoto mwenye umri
wa miaka sita katika Kijiji cha Bwizanduru Kata ya Maruku Wilaya ya Bukoba
Vijijini akiwa amefungiwa ndani kwa miezi saba huku makalio yake yakiwa
yamechanika kutokana na adhabu ya viboko.
Mtoto huyo
aitwaye Erick Emmanuel anatembea kwa shida huku akiwa na makovu mengi mwilini
na sehemu ya makalio yake kuharibika vibaya. Amekuwa akipewa adhabu hiyo na
baba yake mzazi.
Kwa mujibu
wa majirani wa mtoto huyo ambaye anaishi na mama yake wa kambo aitwaye Fidea
Emmanuel, anayedaiwa kumtesa mtoto huyo ni baba yake mzazi aliyejulikana kwa
jina la Emmanuel Justinian.
Chanzo cha
mateso hayo inadaiwa kuwa mtoto huyo hujisaidia ndani na hivyo baba yake mzazi
kuamua kumfungia kwa kipindi chote cha miezi saba bila kutoka nje huku kila
siku mtoto huyo akipata adhabu kali ya viboko.
Mama wa
kambo wa mtoto huyo Fidea Emmanuel aliiambia Mwananchi kuwa mume wake alikuwa
akimpa adhabu mtoto huyo mara kwa mara hasa alipojisaidia au kukojoa ndani kwa
kutumia fimbo ya mti wa m’buni.
Hata hivyo
mama huyo wa kambo na Erick alisema kutokana na hali mbaya ya mtoto huyo
iliyotokana na adhabu ya viboko,amekuwa akimtibu kwa kutumia dawa za mitishamba
bila ya kufanyiwa vipimo au kupelekwa hospitalini.
Pia, mtoto
huyo anaonekana kuwa na michirizi mikubwa katika sehemu ya kifua na tumbo
pamoja na makovu makubwa mwilini mwake, alama ambazo zinahusishwa na viboko
alivyokuwa akicharazwa na baba yake mzazi.
Naye,
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Maiga Audax Bayon, alisema kuwa ilikuwa ni vigumu
kumuona mtoto huyo kwa kuwa kila aliyemuulizia aliambiwa yuko ndani akijifunza
kusoma na watoto wengine jambo ambalo halikuwa kweli.
Mama mzazi
wa mtoto huyo Aneth Brand ambaye anaishi Kijiji cha Bugabo wilayani humo
alisema miezi saba iliyopita alimpeleka mtoto huyo kwa baba yake na kudai
hakuwa na matatizo makubwa yanayomkabili mtoto wake, lakini sasa ana matatizo
ikiwamo upungufu wa damu.
Akizungumzia
tukio hilo Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Bwizanduru, Edward Mwemezi alisema
pamoja na mtoto huyo kufanyiwa ukatili mkubwa kwa muda mrefu alisema familia
ilijitahidi kuficha taarifa hizo hata kwa majirani.
Alisema
baada ya kuendelea kuenea kwa uvumi wa kuwepo kwa mtoto aliyefungiwa kwa
muda mrefu na kupewa mateso katika familia hiyo waliamua kufuatilia
na tayari mtuhumiwa amewekwa chini ya ulinzi kwa ajili ya hatua zaidi za
kisheria.
Habari na:-Gazeti la Mwananchi June 26,2014.
No comments:
Post a Comment