Watu zaidi
ya 30 wanashikiliwa na Polisi wilayani Muleba , Mkoa wa Kagera, wakituhumiwa
kufanya vurugu na uharibifu wa mali, chanzo kikiwa kifo cha mfanyakazi wa ndani
aliyefia mkoani Arusha.
Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Kagera, George Mayunga alisema vurugu hizo zilitokea baada ya
mwili wa mtoto huyo, Asera Tryphone (16) kufikishwa katika Kijiji cha Bukono
kilichoko Kata ya Muleba.
Kwa mujibu
wa kamanda, binti huyo alikuwa akifanya kazi za ndani mkoani Arusha, akaugua
ghafla na kulazwa katika Hospitali ya Mount Meru kabla ya kukutwa na mauti,
Juni 12 mwaka huu.
Mwajiri
wake, Valentina Maxmilian, alisafirisha mwili huo na baada ya kuufikisha
kijijini hapo, inadaiwa wazazi wa marehemu walikuwa wamepata taarifa tofauti
kwamba mtoto wao alifariki dunia kutokana na kipigo na mateso.
Aidha,
taarifa zilizokuwa zimeenea kijijini hapo ni kwamba, baadhi ya viungo vya
mwili, hususani sehemu za siri, mkono na mguu, vilikuwa vimekatwa jambo
lililohusishwa na ushirikina. Kamanda alisema wazazi walitaka mwili huo
ufanyiwe uchunguzi kabla ya kuupokea.
Waliamua
kupiga simu Kituo cha Polisi cha Muleba, na Polisi ilitaka kuongozana na ndugu
hao hadi Kituo cha Afya cha Kaigara kwa ajili ya uchunguzi.
Hata hivyo
wanafamilia waligoma na kutaka polisi wafanye uchunguzi wa mwili huo nyumbani jambo
ambalo halikuafikiwa.
Baada ya
polisi kuondoka eneo hilo, inadaiwa wanafamilia walimbeba maiti na kumtelekeza
katika barabara iliyoko karibu na Kituo cha Polisi Muleba.
Polisi
walichukua mwili na kuupeleka Kituo cha Afya cha Kaigara.
Polisi walishauri
ndugu hao kusubiri mganga aliyekuwa zamu aufanyie mwili uchunguzi wa kitaalamu
jambo ambalo waliafiki.
Wakati
wakisubiri uchunguzi, wananchi walihamasishana tena na kuvunja mlango wa chumba
cha kuhifadhia maiti ambapo polisi waliamua kutumia nguvu na kupiga mabomu ya
machozi kuwatawanya wananchi hao.
Amesema baada ya kutuliza ghasia, uchunguzi wa mwili
ulifanyika na ndugu wakaridhika na kwenda kuzika ingawa inadaiwa wapo baadhi ya
watu waliokuwa wakishawishi wazazi wa marehemu wasikubali.
Miongoni mwa
wanaoendelea kuhojiwa, yumo Veronica; anayedaiwa kumwomba mtoto huyo akafanye
kazi kwa mwanawe.
Pia Polisi
imesema inaendelea kufanya uchunguzi wa kina mkoani Arusha alikofia mtoto huyo
na pia kuchunguza nyumbani kwao.
No comments:
Post a Comment