Bibi mmoja raia
wa Nigeria, Olabisi Ibidun Cole (65) amevunja rekodi ya umri wa watu
wanaokamatwa wakiwa na dawa za kulevya katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere (JNIA).
Cole
alikamatwa Jumatatu akiwa amemeza kete 82 aina ya heroini zilizokuwa zimefungwa
kwenye karatasi zinazofanana na ganda la sigara, ambazo si rahisi kuonekana
katika mitambo.
Habari
zilizopatikana na kuthibitishwa na Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za
Kulevya, Alfred Nzowa zimesema pamoja na mbinu zake na kujiamini, mwanamke huyo
alikamatwa kutokana na ushirikiano wa vitengo mbalimbali vya uwanja wa ndege.
Kamanda wa
Polisi wa Uwanja wa Ndege, Hamisi Selemani alisema mwanamke huyo alikamatwa Mei
19, mwaka huu saa tisa alasiri akijiandaa kwenda Paris, Ufaransa kwa ndege ya
Shirika la Ndege la Ethiopia.
Selemani
alisema raia huyo aliwasili nchini Mei 15, mwaka huu na alikaa muda wote bila
ya kuwa na shughuli yoyote, jambo ambalo lilitiliwa shaka na kumkamata.
“Huyu
mwanamke achana naye, akisimama mbele yako huwezi ukaamini kwa jinsi
anavyojiamini. Alikuwa na mbinu mpya ya kufunga hizo kete. Kila moja ilifungwa
kwa karatasi inayofanana na ganda la sigara,” alisema Selemani.
Alisema
mwanamke huyo alitumia mbinu hiyo ili asigundulike wakati akikaguliwa kwa
mitambo maalumu inayogundua dawa za kulevya.
Taarifa
zaidi zinasema kuwa kutokana na mbinu yake ya ufungaji wa kete, mwanamke huyo
alikuwa tayari amevuka hatua ya kwanza ya ukaguzi.
Nzowa
alisema baada ya kumhoji, mtuhumiwa huyo alidai kuwa aliingia nchini kwa ajili
ya kutafuta soko la kuuza vipodozi na nguo.
“Wakati
tukiendelea kumhoji, Kikosi Kazi cha Kuthibiti Dawa za Kulevya kilibaini na
kugundua kuwa alikuwa amemeza dawa za kulevya.
“Huyu ni
mzee, lakini tumeshangaa kuona bado ana nguvu za kutosha na tulishangaa baada
ya kutoa kete 20 kwa mara moja katika awamu ya kwanza, jambo hili si rahisi
kutokana na umri wake,” alisema Nzowa.
Mtuhumiwa
huyo aliyekuwa na hati ya kusafiria ya Nigeria, anaendelea kuhojiwa na
upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani.
Habari
Na:-Mwananchi.
No comments:
Post a Comment