Kwenye Hotuba ya Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni ya Wizara ya Habari,Utamaduni na Michezo aliyoiwasilisha
Bungeni May 29,2014 na Waziri Kivuli Bw.Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ alimtaja Zitto Z. Kabwe kama Mmiliki
wa Kampuni ya Leka Dutigite aliyofanya biashara isivyo halali na Mashirika ya
Umma ya NSSF na TANAPA.
Hivi ndivyo ilivyokuwa sehemu
ya hotuba hiyo.
Mheshimiwa Spika, Tarehe 13
Agosti, 2012, Msajili Msaidizi wa Makampuni katika Wakala wa Usajili wa
Makampuni na Leseni (BRELA) alitoa Hati ya Usajili (Certificate iof
Incorporation) kwa kampuni inayoitwa Leka Dutigite Limited.
Kwa mujibu wa
nyaraka za BRELA, Leka Dutigite Ltd. ina ofisi zake katika ghorofa ya kwanza ya
jengo la City House lililoko katika Mtaa wa Mkwepu, Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika,Katiba yaani
Memorandum and Articles of Association, ya kampuni ya Leka Dutigite Ltd.
iliyosajiliwa BRELA tarehe 13 Agosti, 2012 inaonyesha kwamba mwenye hisa nyingi
katika kampuni hiyo ni kampuni nyingine inayoitwa Gombe Advisors Ltd. ya Dar es
Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa za
kibenki ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu imezipata, mnamo
tarehe 10 Desemba, 2012, Hifadhi ya Taifa ya Saadani ilihamisha jumla ya
shilingi 12,200,000 kwenda kwenye akaunti na. 0150357447800 iliyoko CRDB Bank
tawi la Pugu Road, Dar es Salaam, inayomilikiwa na Leka Dutigite Ltd.
Hifadhi
ya Taifa ya Saadani inamilikiwa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), ambayo
ni shirika la umma. Siku moja baadae, fedha hizo zilitolewa kwa pesa taslimu
kutoka kwenye akaunti hiyo.
Baada ya hapo, kati ya tarehe
14 Januari na 7 Februari, 2013, akaunti ya Leka Dutigite Ltd. iliingiziwa jumla
ya shilingi 28,600,000.
Fedha hizi zote ziliingizwa kama fedha taslimu na mtu
aitwaye Mchange (shilingi 3,600,000 tarehe 14 Januari, 2013) na Leka Dutigite
(shilingi 25,000,000 tarehe 23 Januari na 7 Februari, 2013). Kufikia tarehe 7
Februari, 2013, fedha hizo zote zilikwishatolewa benki.
Mheshimiwa Spika, Tarehe 28
Februari, 2013, akaunti ya Leka Dutigite Ltd. iliingiziwa shilingi 32,367,000
na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF). Kwa mujibu wa taarifa za kibenki,
siku hiyo hiyo, fedha hizo zilitolewa kwenye akaunti hiyo.
Siku nne baadae,
yaani tarehe 4 Machi, 2013, NSSF ilifanya malipo mengine kwenye akaunti ya Leka
Dutigite Ltd., kwa mikupuo miwili, ya jumla ya shilingi 46,663,000.
Siku hiyo
hiyo, fedha hizo nazo zilitolewa kutoka kwenye akaunti hiyo kwa mikupuo miwili.
Kwa hiyo, katika kipindi cha miezi mitatu katika ya tarehe 10 Desemba, 2012 na
4 Machi, 2013, Leka Dutigite Ltd. ililipwa shilingi 119,930,000 kwa utaratibu
huo huo wa ingiza na toa fasta. Kati ya fedha hizo, shilingi 12,200,000
zililipwa na TANAPA na shilingi 79,027,000 zililipwa na NSSF.
Mheshimiwa Spika, Katika
mazingira ya kawaida, sio kitu cha ajabu kwa mashirika ya umma kama NSSF na
TANAPA kufanya biashara na watu au taasisi mbali mbali kama makampuni binafsi.
Ukweli ni kwamba, kwa upande wa malipo yaliyofanywa na TANAPA, Kambi Rasmi ya
Upinzani ya Bunge lako tukufu imeweza kupata nakala ya mkataba unaohusu Maandalizi
ya Filamu (Documentary) kwa Ajili ya Kuhamasisha Shughuli za Utalii katika
Hifadhi ya Taifa ya Saadani kwa Kutumia Wasanii Kutoka Kigoma.
Mkataba huo
umesainiwa tarehe 5 Desemba, 2012, kati ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani na Leka
Dutigite Ltd. na una thamani ya shilingi 12,200,000, kiasi kile kile
kilicholipwa na Hifadhi hiyo.
Hata hivyo, Mheshimiwa Spika,
mazingira ya malipo haya sio ya kawaida. Hii ni kwa sababu ya uwepo wa kampuni
ya Gombe Advisors Ltd. Kwa mujibu wa nyaraka za BRELA, kampuni hii ilisajiliwa
tarehe 24 Novemba, 2011.
Kwa mujibu wa nyaraka hizo, ofisi za Gombe Advisors
Ltd. ziko kwenye jengo la City House, Mtaa wa Mkwepu, Dar es Salaam, ziliko
ofisi za Leka Dutigite Ltd. Kwa mujibu wa nyaraka hizo, wakurugenzi wa Gombe
Advisors Ltd. ni Zitto Zuberi Kabwe ambaye kazi yake inatajwa kuwa ‘mchumi’, na
Raphael Ongangi ambaye anatajwa kuwa ‘mchambuzi wa fedha na vitega uchumi’
(Financial and Investment Analyst).
Bwana Ongangi aliwahi kutajwa na gazeti la
kila wiki la —– la tarehe 26 Desemba 2013 kuwa ni mmoja wa washauri wa Zitto
Zuberi Kabwe na anasemekana kuwa msaidizi wake.
Mheshimiwa Spika, Zitto
Zuberi Kabwe sio ‘mchumi’ anayetajwa katika nyaraka za BRELA zinazoihusu
kampuni ya Gombe Advisors Ltd. pekee, bali pia ni Mbunge, tangu mwaka 2005, wa
Bunge lako tukufu.
Kama Mbunge, Mheshimiwa Zitto Kabwe ni ‘kiongozi wa umma’
kwa mujibu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, 1995. Sheria hii inawalazimu
viongozi wa umma, wanapokuwa madarakani, kuwa “waadilifu, wenye huruma,
utulivu, umakini na watakaoendeleza viwango vya juu vya maadili ili kujenga na
kuendeleza imani ya umma kwa uadilifu wa Serikali.”
Aidha, viongozi wa umma “…
watawajibika kutekeleza wajibu wao kwa umma na kuendesha shughuli zao binafsi
kwa namna ambayo itaonekana na kuthibitika kuwa ni wazi kwa umma na
haitatosheleza kwao kutekeleza wajibu wao kwa kufuata sheria tu.” Vile vile,
kuhusiana na maslahi binafsi, Sheria hii inaelekeza kwamba “… viongozi wa umma
hawatakuwa na maslahi binafsi ambayo yanaweza kuathiriwa na maamuzi ya serikali
wanayoshiriki katika kuyafanya.
Mwisho,kuhusiana na maslahi
ya umma, viongozi wa umma wanatakiwa, pale wanapochaguliwa au kuteuliwa,
kupanga masuala yao “kwa namna itakayozuia migongano ya maslahi ya wazi,
iliyojificha au inayoonekana kuwepo na pale ambapo migongano hiyo inatokea kati
ya maslahi binafsi na maslahi ya umma basi itatatuliwa kwa kuangalia zaidi
maslahi ya umma.” Kwa kadri ya ufahamu wa Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako
tukufu, Mheshimiwa Zitto Kabwe hajawahi kutangaza maslahi aliyonayo kwenye
mikataba ya Gombe Advisors Ltd. na Leka Dutigite Ltd. na NSSF na TANAPA.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa
Zitto Zuberi Kabwe sio tu ni Mbunge anayebanwa na masharti ya Sheria ya Maadili
ya Viongozi wa Umma, bali pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Fedha za Serikali (PAC).
Kwa mujibu wa kipengele cha 12 cha Nyongeza ya Nane ya
Kanuni za Kudumu za Bunge lako tukufu, mojawapo ya majukumu ya PAC ni
kushughulikia maeneo yenye matatizo sugu ya matumizi mabaya ya fedha za umma
katika Wizara na Mashirika ya Umma yaliyoainishwa katika taarifa ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
NSSF na TANAPA ni baadhi tu ya Mashirika ya
Umma yaliyo chini ya usimamizi wa kibunge wa PAC.
Kwa maana hiyo, Mheshimiwa
Spika, Mheshimiwa Zitto Kabwe, kwa kutumia makampuni yake ya Leka Dutigite Ltd.
na Gombe Advisors Ltd., amefanya biashara na TANAPA, shirika la umma
analolisimamia kama Mbunge na Mwenyekiti wa PAC.
Mheshimiwa Zitto Kabwe na wanamuziki
washirika wake, kwa kutumia makampuni ya Gombe Advisors Ltd. na Leka Dutigite
Ltd., wamelipwa fedha za umma za TANAPA na NSSF.
Kambi Rasmi ya Upinzani
inaitaka Serikali kutoa maelezo juu ya madai ya ukiukwaji wa Sheria uliofanywa
na viongozi wa umma na mashirika ya umma katika kashfa hii.
Pamoja na maelezo
yatayotolewa , Kambi Rasmi ya Upinzani inataka Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalum juu ya matumizi ya fedha zilizotolewa na
TANAPA na NSSF; msukumo uliofanya fedha hizo zitolewe na matumizi ya fedha hizo
kwa kuzingatia masharti yanayosimamia fedha za umma na utawala bora katika
usimamizi wa fedha za umma.
Aidha, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU) ifanye uchunguzi juu ya malipo na matumizi husika kwa kurejea
masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Sheria nyingine
zinazohusika.
Kwa upande mwingine, kwa kuwa suala hili linahusu mbunge na
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge inayohusika na usimamizi wa fedha za umma, Kamati
ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge nayo ifanye uchunguzi wake juu ya madai ya
masharti ya Katiba ya Nchi, Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge na
Kanuni za Bunge juu ya maadili ya kiongozi wa umma ikiwemo yahusuyo utangazaji
wa maslahi.
Mheshimiwa Spika; Mwisho,
Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu inatoa rai kwa wanamuziki na
wasanii wengine wote nchini kuwa waangalifu na watu wanaotaka kutumia umaarufu
wao kama wanamuziki na wasanii kwa lengo la kufanikisha dili za kifisadi.
Bila
kuchukua tahadhari ya kutosha, wasanii hao wanaweza kujikuta wakipoteza sifa na
umaarufu wao ambao wameujenga kwa jitihada zao wenyewe.
Maelezo yangu kuhusu kazi za
Kigoma AllStars/LEKADUTIGITE kwa NSSF na TANAPA.
Tarehe 29 Mei, 2014
Msemaji wa Kambi ya Upinzani kuhusu Habari, Michezo, Vijana na Utamaduni
amenituhumu kuhusika na kinachoitwa ufisadi katika Shirika la TANAPA na NSSF.
Nasikitika kwamba katika hali
niliyonayo ya kumwuguza mama yangu naingizwa kwenye siasa za majitaka. Kwa sasa
nitatoa maelezo kwa ufupi ili kuondoa upotoshaji.
Kampuni ya LekaDutigite
inamilikiwa na wasanii 15 ambapo kila mmoja ana hisa 5% ambazo niliwalipia ili
waweze kushirikiana katika kazi zao.
Hisa 25% zilizobakia zinamilikiwa na
kampuni ya Gombe Advisors ambayo ni kampuni isiyofanya faida (Company limited
by guarantee) na haina maslahi yeyote ya kibiashara (not for profit company).
Hivyo Mimi binafsi sina maslahi yeyote ya kifedha zaidi ya kuwasaidia wasanii
hawa katika kazi zao mbalimbali.
Wasanii wa Kigoma AllStars
wamefanya kazi na TANAPA na NSSF, kazi ambazo zinajulikana na zipo.
Kwa upande
wa TANAPA wasanii hawa waliandaa kazi ya kuitangaza Hifadhi ya Saadani na
walilipwa.
Kwa upande wa NSSF wasanii hao walitunga wimbo na video yake na
wimbo huo unatumika katika Shirika hilo.
Vile vile walifanya matamasha
mbalimbali ya kuhamasisha watu kujiunga na NSSF. Wasanii wa Kigoma All Stars
wote ni wanachama wa Mfuko huo.
Katika kazi zote hizi Mimi
binafsi sijafaidika kwa namna yeyote ile kifedha.
Kauli yeyote ya kujaribu
kuonyesha kazi hizi za wasanii ni ufisadi ni kauli za kusikitisha na kukatisha
tamaa kwa mtu ambaye anajaribu kusaidia wasanii kufaidika na kazi zao za sanaa.
Katika kazi zote hizi Mimi
binafsi sijafaidika kwa namna yeyote ile kifedha. Kauli yeyote ya kujaribu
kuonyesha kazi hizi za wasanii ni ufisadi ni kauli za kusikitisha na kukatisha
tamaa kwa mtu ambaye anajaribu kusaidia wasanii kufaidika na kazi zao za sanaa.
Toka mwaka 2012 nilipoanza
kujitokeza kusemea wasanii watu kadhaa wenye maslahi na tasnia hii wamekuwa
wakinikatisha tamaa na hata wengine kuona nimewaingilia kazi zao.
Hivi sasa wasanii wa Kigoma
AllStars ni wanahisa katika kampuni ya PERA Africa limited ili kufaidika na
biashara ya miito ya simu.
Yote haya nilifanya kwa uchungu nilionao kwa vijana
wetu na sio kwa kutaka kufaidika kifedha. Nimeumizwa sana na tuhuma hizi za
kuokoteza okoteza.
Inaniumiza zaidi kutokana na
ukweli kwamba ninamwuguza mama yangu mzazi, kipindi ninachohitaji kutiwa moyo
na kuombewa hata na maadui zangu kisiasa.
Kipindi ambacho mama yangu yupo
mahututi, tena mjumbe wa kamati kuu ya chama ambacho watoa tuhuma wanatoka,
pole ninayopewa ndio hiyo. Hakuna namna ya kukosa ubinaadamu zaidi ya hivi.
Najua wajibu wangu ni
kusimamia Mashirika ya Umma na nikiwa mpigania uwajibikaji nipo makini sana
kuhakikisha sina mgongano wa maslahi katika mambo yangu.
Ndio maana sina
biashara yeyote ile ili kuhakikisha natimiza wajibu wangu kwa uadilifu mkubwa.
Napata ‘moral authority’ ya kutaka uwajibikaji kwa sababu nafanya kazi zangu
kwa misingi hiyo ‘at arms length’.
Hivyo ninataka mara moja CAG
afanye ukaguzi wa kazi za wasanii hao kwenye NSSF na TANAPA. Pia achunguze kama
Gombe Advisors ( company limited by guarantee) ina maslahi yeyote ya kifedha
katika kazi hizo za wasanii. Nataka pia Shirika la NSSF na TANAPA waweke wazi
mchakato wa kazi zao na wasanii hawa kupitia LEKADUTIGITE Limited.
Zitto Kabwe
Mei 29, 2014
Dar Es Salaam.
No comments:
Post a Comment