Kijana Ndaki
Samola akiwa amepandishwa ndani ya gari la Polisi kwa ajili ya kupelekwa kwa
wataalamu ili kufanyiwa uchunguzi kama ana matatizo ya akili ama la.
|
Katika hali
isiyokuwa ya kawaida mamia ya wananchi wa kijiji cha Ilebelebe kata ya Itilima
wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga wamefurika kushuhudia tukio la
kijana mmoja anayesadikiwa kuwa ni msukule aliyeibuka siku moja baada ya
kikongwe kuuawa kwa kucharangwa mapanga kwa imani za kishrikina kijijini
hapo.
Kijana huyo
aliyedai kuwa anaitwa Ndaki Samola alionekana jirani na nyumba ya
mwanamke Nyanzala Basu (65-70) aliyeuawa Mei 26 mwaka huu,saa moja na
nusu usiku baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana kisha kumcharanga
mapanga akiwa nyumbani kwake kisha kutokomea kusikojulikana.
Imeelezwa
kuwa siku ya mazishi ya Kikongwe huyo Mei 27 mwaka huu ndipo kijana
huyo anayedaiwa kuhifadhiwa na kikongwe huyo alikutwa na wananchi nyuma ya
nyumba ya kikongwe huyo saa tatu usiku akizunguka na kusikika akisema kaamua
kutoka nje baada ya kukosa chakula.
Kijana huyo
akizungumza bila ya kufafanua ni kipindi gani amekaa katika kijiji hicho alidai
alikuwa akiishi kwenye nyumba ya bati ya kikongwe huyo na wenzake wawili na
kwamba kutokana na njaa yake ndiyo kaamua kutoka.
Mwenyekiti
wa kijiji cha Ilebelebe Thomas Nkindo alisema tukio hilo limewashangaza
kwani kijana huyo hajawahi kuonekana kijijini hapo hata siku moja ,hali ambayo
imewapa wasiwasi wananchi kutokana na maneno aliyoeleza kwamba alikuwa kwenye
nyumba ya kikongwe huyo ambayo ilikuwa imefungwa kwa muda mrefu na haitumiki
“Baada ya
kuhojiwa na jeshi la jadi sungusungu kijana, alidai kilichomtoa ndani
ni njaa na kawaacha wenzake wawili mmoja akiwa ni mwanamke,na alikuja kwa
ajili ya kuoa na kufikishiwa kwenye nyumba hiyo ya tope ambayo imeezekwa kwa
bati iliyokuwa ikimilikiwa na marehemu”,alieeleza Nkindo.
Akifafanua
zaidi kuhusu tukio hilo afisa mtendaji wa kijiji cha Ilebelebe Emmanuel
Asili alisema marehemu Nyanzala Basu kabla ya kufikwa na mauti siku hiyo ya
tukio asubuhi alikuwa amealika wanawake, ambao walifanya kazi ya kumsaidia
kukata viazi maarufu kama michembe ndipo usiku huo huo alivamiwa na kuuawa
majira ya saa 1.30 wakati akimpatia mbwa wake chakula.
“Kilichotushtua
zaidi huyo kijana Ndaki alikuwa ananukia harufu ya nyama wakati tunamuona na
ukizingatia mchana kwenye mji huo ulipokuwa msiba walikuwa wamechinja
mbuzi,moja kwa moja wananchi walimtilia mashaka inawezekana akawa ni msukule
kwa kulinganisha na maelezo yake “alisema Asili.
“Kutokana na
mashaka hayo tulitoa taarifa kwa jeshi la polisi huku tukimhifadhi kijana kwa
muda katika ofisi yangu uangalizi zaidi na polisi walipofika walizungumza na
wananchi na kuamuru mlango wa nyumba hiyo uvunjwe ili kuona kilichomo ndani
wakakuta beseni,ndoo na bati lililochakaa”,alieeleza afisa mtendaji wa kijiji.
Akizungumza
na wananchi mkuu wa kituo cha polisi wilaya ya Kishapu ASP Samwel Kijenga
aliwataka kutoa ushirikiano ili kuwabaini watu waliosababisha mauaji hayo ya
kinyama huku akiwataka kuondoa wasiwasi kuhusu nyumba waliyokuwa wakihofia
kwani wameangalia hawajaona kitu hivyo waendelee na shughuli za maendeleo.
Hata hivyo
wakati kijana huyo akiwa tayari amepandishwa ndani ya gari la polisi kwa ajili
ya kupelekwa kufanyiwa uchunguzi kama ana matatizo ya akili,alitokea mwanamme
aliyejitambulisha kwa jina la Nyalali Chaba mkazi wa kijiji cha Ikoma wilayani
Kishapu na kudai kuwa anamfahamu ni mdogo wake anasumbuliwa na tatizo la akili
ndipo polisi wakamkabidhi kwa maandishi.
Kamanda wa
jeshi la polisi mkoani Shinyanga SACP Evarist Mangalla amethibitisha kutokea
kwa tukio hilo la mauaji ya kikongwe na tayari watu wanne wanashikiliwa
kwa ajili ya mahojiano zaidi wakati wakiendelea na upelelezi.
Habari Na:-Kadama
Malunde wa Malunde1 Blog-Kishapu
No comments:
Post a Comment