Aliyekuwa
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba ameuliza
maswali saba ya msingi kwa wajumbe wa Bunge la Katiba wanaopinga Rasimu ya
Katiba iliyotolewa na Tume yake akitaka wawajibu wananchi ili kutuliza kiu yao.
Jaji Warioba
ambaye tangu awasilishe Rasimu ya Katiba Desemba 30, mwaka jana amegeuka kuwa
adui kwa watu wanaotaka muundo wa serikali mbili, aliuliza maswali hayo jana
katika uzinduzi wa ripoti ya utafiti wa Taasisi ya Twaweza kuhusu mchakato wa
Katiba.
Akizungumza
kwa ukali, Jaji Warioba alisema: “Kwanza, jibuni kwa nini mnapinga muundo wa
Muungano wakati walioupendekeza ni wananchi?
“Sheria
inasema uwepo wa Muungano na mapendekezo katika rasimu hayasemi Muungano
usiwepo. Kumbukeni kuwa wananchi walitakiwa kutoa mapendekezo ya namna ya
kuboresha Muungano.”
Katika swali
lake la pili:-, Warioba alisema kwa nini Tanganyika imevaa koti la Muungano? Kwa
kuwa katika ukusanyaji wa maoni wananchi walieleza kuwa Serikali ya Muungano ya
sasa siyo ya Muungano, ni ya Tanganyika.
Katika swali
la tatu :-,alisema wajumbe hao wanatakiwa kujibu maelezo ya wananchi ambao
waliieleza tume hiyo kuwa Katiba imevunjwa na madaraka ya rais yamechukuliwa na
sasa kuna marais wawili katika nchi moja.
“Tume
inapewa lawama kubwa, wajibuni wananchi hii tume ilitumwa na nani kukusanya
maoni ya wananchi? Waambieni ilikusanya maoni hayo kwa kutumia sheria ipi zaidi
ya ile ya Mabadiliko ya Katiba?” alisema Jaji Warioba katika swali lake la nne.
Katika swali
lake la tano:-, Warioba aliwataka wajumbe hao kutoa sababu za kumtuhumu kuwa
amependekeza muundo wa serikali tatu kwa sababu yeye pamoja na (Joseph Butiku)
walikuwa wajumbe wa Tume ya Jaji Kisanga na Jaji Nyalali ambazo nazo
zilipendekeza muundo wa serikali tatu, kitu ambacho alisema si kweli na
hawakuwahi kuwa mjumbe wa tume hizo.
Pia,
aliwataka wajumbe hao kujibu swali la sita, kwa nini hawataki kuzungumzia
yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na badala yake wanageuza rasimu hiyo kuwa
imeandikwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Katika swali
lake la saba:-, aliwataka wajumbe kujibu kwa nini wanaishutumu Tume ya Mabadiliko
ya Katiba kuwa imeingiza maoni yake, wakati ilikusanya maoni hayo kwa mujibu wa
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba?
Alisema
badala ya kujadili hoja za msingi, wajumbe wa Bunge hilo wamekuwa wakitoa lugha
za kejeli na matusi kwa baadhi ya watu (akiwamo na yeye), kitendo ambacho
alisema si sahihi na kinaweza kuligawa taifa kwa sababu yaliyomo katika Rasimu
ya Katiba yametokana na maoni ya wananchi.
Katika
uzinduzi huo walikuwepo baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo ambao ni Dk Hamisi
Kigwangalla aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Julius
Mtatiro, Maria Sarungi na aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Humphrey Polepole.
Amshukia Lukuvi.
Katika
maelezo yake, Jaji Warioba alieleza kushangazwa kwake na wajumbe kulitumia
Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kama mfano wa kuwashawishi Watanzania
kukubaliana na matakwa yao ya kutaka kupinga mfumo wa serikali tatu.
“Nchi hii
imekuwa na matatizo ya rushwa na ufisadi, lakini hakuna hata siku moja mtu
amesema jeshi linaweza kushika madaraka. Leo kwa sababu ya madaraka mnaingiza
jeshi na mchakato wa Katiba katika makundi.”
Licha ya
kutomtaja mlengwa, kauli hiyo ilionekana kumlenga Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera Uratibu na Bunge), William Lukuvi ambaye Aprili 13, mwaka huu
aliwataka wananchi kupinga muundo wa serikali tatu, akisema la sivyo jeshi
linaweza kuchukua madaraka.
Akiwa katika
Kanisa la Methodist, Jimbo la Dodoma alipokuwa mgeni rasmi akimwakilisha Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda, Lukuvi alisema muundo huo ukipita, nchi itatawaliwa na
jeshi kwa kuwa Serikali ya Muungano itashindwa kuwalipa mishahara wanajeshi.
Kauli kama
hiyo pia iliwahi kutolewa na Rais Jakaya Kikwete wakati akizindua Bunge Maalumu
la Katiba mjini Dodoma.
“Msiliingize
jeshi katika siasa za makundi na inakuwa mbaya zaidi kama mkienda katika
makanisa na kutoa kauli za namna hii,” alisema Warioba na kuongeza:-
“Umoja wetu,
amani na utulivu kwa kiwango kikubwa mhimili wake ni viongozi wa dini. Wamekuwa
wakihubiri umoja, amani na mshikamano, hivyo tusiingize siasa za makundi kwenye
makanisa na misikiti.”
Jaji Warioba
aliwataka wajumbe wa Bunge hilo kukumbuka wajibu wao wa kuwaunganisha wananchi
na kuwataka waachane na kauli za kejeli, kuudhi na matusi kwani zinaweza kuleta
mgawanyiko na mpasuko nchini.
“Nimekuwa
mtumishi wa umma kwa muda mrefu lakini sijawahi kuona taasisi yenye uzalendo wa
hali ya juu kama JWTZ,” alisema Warioba.
Warioba
ambaye amewahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania,
kuanzia mwaka 1985 hadi 1990, alisema: “Katika ziara zangu mikoani nilikuwa
nikikutana na wanajeshi na kunieleza matatizo yao. Licha ya wakati huo serikali
za mataifa mengine zilikuwa zikipinduliwa na jeshi, hapa kwetu ilikuwa tofauti,
walikuwa na uzalendo wa hali ya juu licha ya kuwa hali yetu kiuchumi ilikuwa
mbaya,” alisema.
Alisema
wakati huo wanajeshi walikuwa wakivaa sare zilizochakaa na viatu vilivyopasuka,
lakini hawakufikiria kuipindua Serikali.
Alisema hata
katika vita dhidi ya Uganda, wanajeshi wa Tanzania walishinda kwa sababu ya
uzalendo na siyo vifaa vya kisasa vya kivita... “Inashangaza kuona watu
wanatolea mfano mmoja tu wa kama wanajeshi wasipolipwa; kwa nini wasiseme
mawaziri au watumishi wa serikali wasipolipwa?”
Alisema
kauli hiyo ni sawa na kuwaeleza wananchi kuwa jeshi ni baya na kama ikipita
Katiba isiyoendana na matakwa ya walio wengi jeshi litachukua nchi.
Alisema
wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba ikikusanya maoni ya wananchi, wanajeshi na
viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini walijikita zaidi kutoa maoni ya
kuimarishwa kwa ulinzi na usalama na siyo mambo mengine.
“Tatizo
ambalo walitueleza ni kuchoshwa na kitendo cha kupiga mizinga 21 kwa Amri Jeshi
Mkuu wakiwa Dar es Salaam na wakiwa Zanzibar. Walisema kwa nidhamu ya jeshi,
Amri Jeshi Mkuu ni mmoja tu. Nadhani mngewaondolea kero hiyo na si mambo
mengine,” alisisitiza.
Kigwangalla.
Kwa upande
wake, Dk Kigwangalla alisema kama tatizo ni Muungano ni vyema suala hilo
likarejeshwa upya kwa wananchi ili watoe maoni yao kwa sababu mchakato huo sasa
umehamia katika muundo wa Muungano pekee.
“Mchakato
huu si wa kuifufua Tanganyika na kuvunja mkataba wa Muungano na siyo wa
kubadili muundo wa utawala. Mambo haya yalihitaji mchakato unaojitegemea,”
alisema.
Alisema tume
zote zilizotoa mapendekezo ya Serikali tatu zilikuwa na asilimia ndogo ya watu
waliounga mkono kama ilivyo kwa Tume ya Jaji Warioba.
Habari Na:-Mwananchi.
No comments:
Post a Comment