Kweli ni
zaidi ya mateso! Ukisema we unaumwa lakini unapata usingizi, kumbe hujawaona
wagonjwa wenyewe! Mtoto Neema Joseph (2) anateseka kwa ugonjwa wa jicho
ambalo limefumuka na kutoka nje huku likitoa harufu kali na maumivu yasiyo na
mfano.
Mtoto huyo
anayelia wakati wote kutokana na maumivu, anaishi na mama yake mzazi, Annastazia
Yohana (28) kwenye Kijiji cha Bugomba, Kata ya Bulungwa wilayani Kahama,
Shinyanga.
Akizungumza
na Uwazi huku akimwaga machozi kwa uzito wa tatizo la mwanaye, mama Neema
alisema hali yake ya maisha kiuchumi ni mbaya, hasa kufuatia kufiwa na
mumewe, Josephat miezi tisa baada ya kujifungua mtoto huyo huku akiwa analea
watoto wenginewawili.
SIKIA KILIO CHA MAMA NEEMA.
“Tangu mume wangu afariki dunia nimekuwa na maisha ya shida, sina msaada kwani hakuna ndugu wa mume wala wangu wenye hali nzuri ya maisha na walio tayari kunisaidia kubeba mzigo wa maisha yangu.
|
Annastazia Yohana Mama wa mtoto Neema
akijitahidi kumbembeleza bila mafanikio.
|
“Hili tatizo
la jicho la mwanangu lilianza mwezi mmoja uliopita (Februari) ambapo lilianza
kwa kuwa jekundu huku likibubujika machozi mara kwa mara.
“Alikuwa
akilifikicha kila wakati kitendo kilichoniasharia kuwa mwanangu anapata mateso.
Ndipo siku moja nilimpeleka Kituo cha Afya cha Kata.
Walimchunguza
na kumpatia matibabu, lakini hali ndiyo ilizidi kuwa mbaya,” alisema mama
Neema.
Alisema jicho lilianza kutokeza kwa nje na kutoa mwonekano wa kutisha. Baadhi ya watu walimshauri ampeleke mtoto huyo kwenye Hospitali ya Nkinga.
“Nilipopata
ushauri huo huku nikioneshwa mmoja wa wanakijiji ambaye mwanae alitibiwa huko,
nilimfuata mama yangu mzazi na kumuomba aniangalizie wanangu wawili ambao mpaka
sasa anao.
“Niliuza chakula changu chote cha akiba ili kupata pesa ya nauli na matibabu,” alisema mama wa mtoto huyo.
HOSPITALI
KUBWA NDIYO WANAWEZA
Mama Neema aliendelea kuweka wazi kwamba, madaktari wa Hospitali ya Nkinga walimfanyia uchunguzi mtoto wake na kusema tatizo lake linaweza kutibiwa Hospitali ya
Kilimanjaro
Christian Medical Center (KCMC) iliyopo Moshi, mkoani Kilimanjaro. Alisema kwa
kauli hiyo, alilazimika kurejea nyumbani na mwanae kwa vile uwezo wa kufika
huko hakuwa nao.
ASAKA
FEDHA, AENDA KUSAKA TIBA ZAIDI
Mama Neema aliendelea kusema: “Hali ya mtoto ikazidi kuwa mbaya zaidi. Sasa jicho lilizidi kutoka nje huku likiambatana na majimaji ya njano na harufu kali. Alikuwa akilia sana kwa maumivu.
“Ilibidi
nisake fedha, nikampeleka Kahama mjini kuomba msaada wa matibabu. Kule Kahama
nilikutana na wanawake watatu ambao walinieleza nifike uwanja wa michezo kuna
madaktari wa saratani walioletwa na Shirika la Huheso Foundation ambao
walinikabidhi kwa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama.”
|
Annastazia Yohana Mama wa mtoto Neema
akijitahidi kumbembeleza bila mafanikio.
|
MGANGA
WA WILAYA AZUNGUMZA
Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama, Helen Yesaya alikiri kumpokea mtoto huyo. Alisema alimpeleka kwa daktari wa macho ili kumfanyia uchunguzi zaidi wa kubaini kama tatizo la jicho hilo ni saratani au la!
“Hata hivyo,
kwa vyovyote itakavyokuwa ni budi mtoto huyu apelekwe Hospitali ya Rufaa ya
Bugando, Mwanza kwa ajili ya matibabu zaidi. Kama unavyomuona, jicho limeoza,
linatoa usaha, kwa kweli anahitaji kusaidiwa,” alisema Dokta Helen huku
akisikitika.
MAMA
TENA
Akizungumzia taarifa hizo, mama wa mtoto huyo alisema hali yake kiuchumi ni mbaya, uwezo wa kuishi jijini Mwanza wakati mwanae akiendelea na matibabu hana, hivyo anawaomba Watanzania wamchangie fedha ambazo anaamini zitakuwa msaada wa kupata tiba bora ya mtoto wake.
KUTOA
NI MOYO
Kwa yeyote aliyeguswa na tatizo la mtoto Neema anaweza kumsaidia kwa kuwasiliana na Shirika la Huheso Foundation la mjini Kahama kwa namba; 0753 444 840-Juma Mwesigwa, atawasiliana na Mama Neema.
Source:-Global Publishers.





No comments:
Post a Comment