![]() |
|
Mwenyekiti
wa Bodi ya TRL,Bw.Severin Kaombwe alisema mpango huo huenda ukaanza baada ya
mwaka 2015 kutoka na mkakati uliopo kwenye Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa
(BRN).
|
Kampuni ya
Reli Tanzania (TRL) inatarajiwa kupata ushindani baada ya Serikali kuamua
kuruhusu wawekezaji wa sekta binafsi kutumia Reli ya Kati.
Uamuzi huo
wa Serikali huenda ukaongeza ufanisi kwa shirika hilo ambalo kwa miaka mingi
limekuwa likikumbwa na matatizo ya kiufanisi.
Baada ya
kuanzishwa mwaka 2007, TRL ilikumbwa na misukosuko baada ya mwekezaji Rites
kutoka India kushindwa kulisimamia kikamilifu na kusababisha hasara ya
mabilioni. Kabla ya TRL reli ya kati ilikuwa chini ya Shirika la Reli (TRC)
ambalo nalo halikuwa na ufanisi.
Akizungumza
katika ufunguzi wa warsha ya kuijengea uwezo TRL iliyofanyika Dar es Salaam
jana(April 22,2014) , Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaaban Mwinjaka
alisema kampuni binafsi zitaruhusiwa kuingiza treni zitakazotumia reli hiyo kwa
kulipa ushuru kwa Serikali.
Kutokana
na mabadiliko hayo, Dk Mwinjaka alisema Serikali imeanza kuiandaa TRL kupambana
na ushindani utakaotolewa na kampuni hizo binafsi.
“Katika
hii warsha tunawaandaa kujua kwamba utafikia wakati wanahitaji kujitegemea. Kwa
misingi hiyo basi, tumepata wataalamu kutoka ndani na nje kuweka mawazo yao
pamoja kujua ni namna gani mabadiliko hayo yatafanyika,” alisema Dk Mwinjaka.
Alipoulizwa
kuwa uamuzi huo utaanza kutekelezwa lini, Mwinjaka alisema baada ya TRL
kujengewa uwezo wa kuwa na mabehewa, injini na watumishi wa kutosha ili kuweka
uwanja mzuri wa ushindani.
Hata
hivyo, Mwenyekiti wa Bodi ya TRL, Severin Kaombwe alisema mpango huo huenda
ukaanza baada ya mwaka 2015 kutoka na mkakati uliopo kwenye Mpango wa Matokeo
Makubwa Sasa (BRN).
“Kwa sasa
tumeshaagiza vichwa (injini) 21 na takriban mabehewa 200 ambayo yanatarajiwa
kufika ndani ya Agosti mwaka huu,” alisema Dk Mwinjaka huku akisisitiza kwamba
mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa BRN.
Alisema
injini na mabehewa hayo yana uwezo wa kurekebishwa kupita kwenye reli zote; za
kawaida (ya kati) na ile ya kisasa inayotarajiwa kujengwa.
“Serikali
imeamua kununua aina hiyo ya vifaa ili shughuli za usafirishaji wa mizigo
kupitia reli ya kati ziendelee bila kuathiriwa wakati wa kujenga reli hiyo mpya
na baada ya kukamilika tutarekebisha ili kupita njia mpya.”
Reli mpya
ya kisasa inatarajiwa kugharimu takriban Dola za Marekani 6 bilioni (Sh9.6
trilioni) zinazofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Dk
Mwinjaka alisema ujenzi utaanza baada ya kukamilika hatua za kumpata mkandarasi
Desemba mwaka huu, shughuli inayosimamiwa na AfDB yenyewe.
“Tulishafanya
upembuzi yakinifu na sasa tunasubiri kumpata mshauri elekezi anayetafutwa na
AfdB, ambaye atamteua mkandarasi mwenye uwezo wa kujenga reli hiyo,” alisema.
Reli hiyo
itaanzia Dar es Salaam - Isaka hadi Kigali, Rwanda; pia itaendelea kuanzia Keza
wilayani Ngara hadi Gitega na Musongati, Burundi.
Mbali na
nchi hizo mbili, pia Serikali mapema mwaka jana ilisaini mkataba na Serikali ya
Uganda kuanza kutumia reli ya kati kusafirisha mizigo kutoka Dar es Salaam
mpaka Kampala na Dk Mwinjaka alisema tayari injini tano na mabehewa 60
yameshanunuliwa kwa ajili ya mradi huo.
Mkurugenzi
Mtendaji wa TRL, Kipallo Kisamfu alisema kampuni yake inajiandaa kwa mabadiliko
hayo na baada ya miaka mitatu itakuwa na uwezo wa kusafirisha tani milioni tatu
za mizigo kwa mwaka kutoka 200,000 za sasa.
“Tumejipanga
pia kuongeza rasilimali watu kwa asilimia 30 kila mwaka mpaka tutakapofikia
lengo. Kwa sasa tunao wafanyakazi 2,900 na tunagemea sana Chuo cha Reli
kuzalisha wataalamu hao,” alisema Kisamfu.
Awali,
Kaombwe alisema kampuni hiyo itakuwa ya kibiashara zaidi na itaruhusiwa kukopa
kutoka katika vyanzo mbalimbali vya fedha.
Habari
Na:-Mwananchi.






No comments:
Post a Comment