Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema amesema Rais Jakaya Kikwete hana uwezo kisheria wa kuwafukuza au kutengua uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.
Jaji Werema
alisema Sheria namba 8 ya Mabadiliko ya Katiba ya 2011, ipo kimya kuhusu suala
hilo na kwamba kwa maana hiyo Rais hana mamlaka ya kutengua hata ubunge wa wale
aliowateua kupitia kundi la wajumbe 201.
“Umesoma
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba? Kaisome maana ili mtu afukuzwe ubunge lazima
apungukiwe sifa za nafasi hiyo, lakini kama sheria iko kimya maana yake ni
kwamba hana (Rais) uwezo wa kuwafukuza,” alisema Jaji Werema.
Jaji Werema
alikuwa akijibu maswali ya gazeti la Mwananchi, kuhusu hatima ya wajumbe ambao ni
wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambao Jumatano (April 16,2014) jioni
waliondoka bungeni kwa madai ya kutoridhishwa na uendeshaji wa Bunge Maalumu.
Wajumbe
waliotoka nje ni wanaotokana na vyama vya CUF, Chadema, NCCR Mageuzi, NRA, NLD
na baadhi kutoka kundi la 201.
Alhamisi asubuhi, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu,
Samuel Sitta alisema utafiti uliofanywa na ofisi yake ulibaini kuwa katika
kundi la 201, ni wajumbe 25 tu ambao walitoka nje pamoja na Ukawa.
Baada ya
wajumbe hao kutoka nje, Mjumbe wa Bunge hilo, Mwigulu Nchemba ambaye ni Naibu
Katibu Mkuu wa CCM Bara, aliomba mwongozo akihoji iwapo Ofisi ya Mwenyekiti wa
Bunge Maalumu haiwezi kumwandikia Rais Kikwete ili ateungue uteuzi wa wajumbe katika
kundi la 201 ambao waliungana na Ukawa kususia vikao.
“Ningependa
Rais atengue hadhi zao ili kuingiza watu wengine ambao wako tayari kufanya kazi
hata bure, sisi tunalipwa fedha nyingi, lakini tunaleta mzaha, watu hawana
maji, dawa, madawati, ada za elimu ya juu watu wamekosa, hizi fedha zingetumika
huko,” alisema Nchemba mwenye wadhifa mwingine wa Naibu Waziri wa Fedha.
Matakwa ya
Sheria.
Jaji Werema
alisema: “Ili mtu aondolewe katika nafasi yake ni lazima akose sifa za kuwa
mjumbe, mathalan kuugua ugonjwa wa akili au kichaa, kuumwa muda mrefu kiasi cha
kushindwa kutimiza majukumu yake na kadhalika, lakini sifa hizo kama hazipo
kwenye sheria sasa unaanzia wapi?”
Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba ya 2011 pamoja na marekebisho yake ya 2012 na 2013 inawataja
Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi kuwa Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kwa mujibu wa nafasi zao.
Kadhalika
sheria hiyo inampa Rais mamlaka ya kufanya uteuzi wa wajumbe 201 kutoka makundi
mbalimbali, lakini haitaji sifa wanazopaswa kuwa nazo wajumbe hao.
Jaji Werema
alisema hata kama sheria ingekuwa inaruhusu kufukuzwa au kusitishwa kwa ujumbe
wa wabunge hao, hakuna sababu ya msingi ya kuwachukulia hatua hiyo.
Habari Na:- Mwananchi
No comments:
Post a Comment