HISTORIA:- Marehemu Muhidin Gurumo “tunamuombea kwa Mungu kila heri huko aliko na ampumzishe kwa amani,” - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Monday, April 14, 2014

HISTORIA:- Marehemu Muhidin Gurumo “tunamuombea kwa Mungu kila heri huko aliko na ampumzishe kwa amani,”


Picha ya marehemu maalim Gurumo enzi za uhai wake akiwa na mkewe… Gwiji la muziki wa dansi Tanzania, Maalim Muhidin Gurumo amefariki jana (April 13,2014) mchana kwa maradhi ya moyo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili-Dar es Salaam.
Amezaliwa mkoa wa Pwani wilaya ya Kisarawe 1940. Elimu ya Msingi alisoma katika  Shule ya Pugu kuanzia darasa la kwanza mpaka la tatu, mwaka 1956, mjomba wake aliamua kumuamishia  Dar es Salaam ambako alisoma zaidi elimu ya dini 'Kuran', Mtaa wa Lindi, Ilala.

Gurumo aliyezaliwa mwaka 1940, alianza muziki mwaka 1960 katika bendi ya Kilimanjaro Chacha, mwaka 1962 akajiunga na Rufiji Jazz Band, kabla ya kutua Kilwa Jazz mwaka 1963.

Mwaka 1978 aliamia Mlimani Park Orchestra na mwaka 1985 alijiunga na  Bendi ya Orchestra Safari Sound (OSS- Ndekule)  lakini siku zote maisha yake yamekuwa Msondo ambayo ndiyo bendi iliyopitia majina ya Nuta, Juwata na Ottu.


Ndugu wa marehemu Gurumo
wakiwa katika picha ya pamoja,
kuanzia kushoto ni mtoto wake Mwalimu Muhidin,
 Mariamu Muhidin na Omari Muhidin
anayefuatia ni kaka wa marehemu
Bw.Ramadhani Mwishehe.
Tangu miaka ya 1960 kama ungethubutu kutamka humjui Gurumo, ungeonekana mshamba ambaye tasnia ya muziki umeipa kisogo,alikuwa staa mkubwa sana wa muziki kipindi hicho ingawa jina  lake limebaki juu kuanzia nyakati hizo mpaka sasa.

Ni kamanda hodari, aliyeifanya Bendi ya Msondo ‘Msondo Ngoma’ ipate heshima kubwa mpaka ikaitwa Baba ya Muziki Tanzania(Msondo na sasa Msondo Ngoma Music Band, bendi aliyodumu nayo hadi kifo chake licha ya kuchomoka mwaka 1978 kwenda kuanzisha DDC Mlimani Park ‘Sikinde).

Tungo zake nyingi ni lulu ambayo haitafutika kamwe. Kinachoumiza kwa sasa ni kuona Gurumo hawezi tena kusimama jukwaani.

Mzee huyo ndiye aliyeivusha Msondo  kupitia majina ya Nuta, Juwata,  na Ottu, ikiwa inamilikiwa na Chama cha Wafanyakazi.

Itambulike kuwa yeye akiwa na wenzake kama marehemu Shaaban Mhoja Kishiwa  maarufu kama ‘TX Moshi William’, Saidi Mabera, marehemu Suleiman Mbwembwe, Othuman Momba, Joseph Maina na wengineo, ndiyo waliounganisha nguvu na kuimiliki, baada ya chama cha wafanyakazi kujiondoa katika uendeshaji wa bendi.


Maalim Muhidin Gurumo ,
enzi za uhai wake.
Gwiji huyo wa muziki aliyeanza kuimba mwaka 1960, atakumbukwa na nyimbo zake zenye kubeba ujumbe kulingana na mazingira husika iwe siasa, uchumi na masuala ya kijamii.

Agosti mwaka jana, Mzee Gurumo alitangaza kustaafu muziki baada ya kuitumikia fani hiyo kwa miaka 53.

Alifanya hivyo kutokana na umri na afya yake kuzorota mara kwa mara kwa sababu ya maradhi.

Ameimba zaidi nyingi zikiwamo za Usimchezee Chatu, Selina piga moyo konde na nyinginezo nyingi, huku akiwa pia mwalimu wa wanamuziki wengi mahiri nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad