Pamoja na hayo nia kubwa ya elimu hii ni kumwendeleza mtu ambaye hakubahatika kupata elimu ya Msingi.
Kwa Tanzania inaelezwa kuwa mkakati huu ulianza mara baada ya nchi kupata
uhuru Mwaka 1961 ambapo suala hili lilipewa kipaumbele lengo likiwa ni
kupambana na ujinga, Maradhi na Umaskini.
Taarifa zinaeleza kuwa mpango huu ulifanikiwa kwa asilimia kubwa
kupunguza idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika wakati wa Serikali ya awamu
ya Kwanza lakini kwasasa inaonekana idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika imeongezeka
kwa kasi.
Wakati wa Serikali ya awamu ya kwanza chini ya hayati Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere idadi ya walimu katika Shule za Msingi na Sekondari
ilitosheleza ambapo ilipelekea walimu hao kuweza kufundisha Elimu ya watu
wazima.
Kutokana na hali ngumu ya Uchumi kwa sasa na ongezeko la
uandikishaji wanafunzi wa Shule za
Msingi kuwa mkubwa kumekuwepo na upungufu mkubwa wa walimu na hivyo kushindwa
kufundisha katika madarasa ya elimu ya watu wazima na hivyo madarasa mengi ya
elimu ya watu wazima kukosa wawezeshaji.
Kaimu Afisa elimu ya watu wazima katika halmashauri ya manispaa ya Musoma
mkoani Mara , Mwalimu Fibe Okelo alisema kwasasa elimu ya watu wazima ni kama
vile imepuuzwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Alisema mwaka 1964 katika mpango wa miaka 5, 10 hadi 20 msisitizo ulikuwa
elimu kwa wote na Mwaka 1970 Msisitizo wa elimu ya watu wazima ulitangazwa na
Mwalimu Nyerere kuwa suala la kuelimisha watu wazima lilikuwa ni jukumu la kila
Mtanzania aliyekuwa anajua kusoma na kuandika tofauti na ilivyosasa.
"Nyakati za Mwalimu kulikuwa na msisitizo mkubwa sana katika suala
la elimu ya watu wazima jambo ambalo kila mtanzania aliliona kama linamhusu
tofauti na leo kila mtu na mambo yake" alisema Afisa huyo.
Mwalimu Okelo anaendelea kuelezea kuwa juhudi hizo wakati wa mwalimu
ziliweza kupunguza idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika kuwa asilimia 6.7
Mwaka 1967 huku Mwaka 1980 idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika ilianza
kuongezeka kutokana na vita ya Kagera ambapo idadi iliongezeka hadi kufikia
asilimia 9.6 huku kwa sasa idadi hiyo ikiwa imeongezeka hadi kufikia asilimia
31.
Kwa sasa hali ngumu ya Maisha na kiuchumi
imeweza kuzalisha kundi lingine la vijana la wasiojua kusoma na kuandika
kutokana na kukosa nafasi ya kuandikishwa darasa la kwanza.
Aidha afisa elimu huyo watu wazima alieleza kuwa kwasasa takwimu za watu
wasiojua kusoma na kuandika katika wilaya ya Butiama ni pamoja ana ME 89,396
huku KE 103,501 huku idadi ya watu wasiojua kusoma,kuandika na kuhesabu ikiwa
ni asilimia 82 na idadi ya wanakisomo ikiwa ni 3,575.
Akielezea kuhusu sera ya elimu ya watu wazima,Mwalimu Okelo alisema kuwa
Sera ya Kisomo chenye Manufaa (KCM) haiwezi kufanikiwa kutokana na viongozi
kutotoa kipaumbele katika elimu hiyo bali kwa sasa limebaki jina la kuwepo kwa
elimu ya watu wazima (EWW).
Alisema kutokuwepo kwa bajeti ya kutosha katika kuendesha Madarasa na
idara hiyo ni tatizo katika mustakabali wa elimu hiyo kwani viongozi wetu
hawaoni kama kuna umuhimu katika elimu hiyo.
"Itakuwa kazi sana kufanikiwa katika Elimu ya watu wazima na hii ni
kutokana na viongozi kutotekeleza sera ya Elimu ya watu wazima,tunapanga bajeti
lakini bajeti hailetwi sasa hapo sisi tutafanya nini" alisema Mwalimu
Okelo.
Alisema EWW si mfumo rasmi kama ulivyo mfumo wa elimu wa Moja kwa moja
hapa kuna madarasa ambayo wahusika huzalisha na hiyo ndiyo tafsiri sahihi ya
EWW kuwa ni kisomo chenye Manufaa.
Mbali na kutokuwepo kwa bajeti lakini pia hakuna vitabu ambavyo
vinaendana na sera yenyewe katika kutoa elimu ya watu wazima.Madarasa rasmi na
hivyo kusababisha kutoa elimu hiyo katika mfumo usio sahihi.
Katika hatua nyingine imeonekana kuwepo kwa uzembe wa viongozi katika
kusimamia na kuhimiza sera ya elimu ya watu wazima kutekelezwa kutokana na
kutokuwepo kwa hamasa kwao,mfano katika wilaya Mwenyekiti wa kuhamasisha elimu
ya watu wazima ni Mkuu wa wilaya akisaidia na Mkurugenzi lakini viongozi hao
pamoja na kuwepo kwa jukumu kubwa katika kufanikisha suala hilo hakuna msumo
wowote wanaoutoa katika Jamii au vikao vya Madiwani.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma Bw Musiranga Muhabi alisema tatizo kubwa ambalo linasababisha
kutofanikiwa katika utekelezaji wa elimu ya watu wazima ni ukosefu wa Bajeti
ambao umekuwa tatizo kubwa katika halmashauri.
Alisema mara nyingi bajeti ya elimu ya watu wazima inaunganishwa katika
idara ya elimu hivyo fedha zinapokuja huunganishwa katika mfumo wa elimu ulio
rasmi kutokana na mahitaji yake hivyo nadhani ingekuwa bora kama serikali
ingetenga idara ya elimu ya watu wazima ambayo inajitegemea.
"Kufanikiwa bado nji tatizo kutona na bajeti kuwa ndogo mimi nadhani
kama kweli tunataka kufanikiwa katika suala hili ni bora kitengo hiki
kingejitegemea ili kuleta ufanisi mkubwa" alisema kaimu Mkurugenzi huyo.
Baadhi ya watu waliosoma elimu ya watu wazima nyakati za serikali ya
awamu ya kwanza walisema kwa sasa elimu ya watu wazima ipo kwa sababu isije
kuonekana imekufa mikononi mwa watu lakini hakuna ambaye anajali eneo hilo.
Mzee Nyanjofu Majaaliwa alisema kuwa kama sio kisomo hicho leo hasingejua
kusoma na kuandika lakini kulingana na sera nzuri iliyokuwepo waliweza
kufanikiwa hadi kufikia kufanya kazi kwenye Makampuni wakati huo.
Naye Mwalimu Mstaafu Juma Nyasoro ambaye aliwahi kufundisha madarasa ya
Elimu ya watu wazima alisema kuwa wakati wa Serikali ya awamu ya kwanza hayati
walimu Nyerere aligundua watanzania hawajui kusoma wala kuandika hivyo hatua za
haraka zilihitajika.
Alisema kuwa hata walimu waliokuwa wanajitolea kufundisha Madarasa hayo
walikuwa na moyo tofauti na leo walimu wengi wametanguliza Masilahi mbele bila
kuangalia athari ambazo jamii inazipata.
"Sisi tulikuwa na moyo wa kujitolea katika kuhakikisha watanzania
wanaondokana na tatizo la kutojua kusoma na kuandika tofauti na leo kila mwali
mu anatnguliza pesa kwanza" alisema Mwalim huyo Mstaafu.
Katika hatua hiyo Mwalimu huyo Mstaafu alisema kuwa bila kuwepo na
msukumo kutoka idara huska elimu ya watu wazima itabaki jina huku akieleza kuwa
hajui kama madarasa hayo bado yapo.
Nao baadhi ya wananchi mbalimbali walipata nafasi ya kuhojiwa na mwandishi
wa Makala hii walisema kuwa itakuwa kazi kukuza eneo hilo kutokana na Serikali
kutoiona kama ina manufaa katika jamii,mmoja wa mwananchi aliyejitambulisha kwa
jina la Ally Ramadhani Mkazi wa manispaa ya Musoma alisema kuwa si rahisi
kufanikiwa katika eneo hilo kwasasa kutokana na hali ya uchumi ilivyo lakini
viongozi kutotoa msukumo katika elimu hiyo.
Alisema kuwa Mamlaka huska zinapaswa kuweka bajeti ambazo zitasaidia
katika kukuza na kuendeleza elimu ya watu wazima ili kionekana kuwa na Manufaa
tofauti na sasa ambapo idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika inaongezeka na
hasa kundi la vijana.






No comments:
Post a Comment