VPL 2013/2014:- Azam FC hiyoo kwenye Ubingwa wa Ligi Kuu Soka Bara kwa mara ya kwanza. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Monday, March 31, 2014

VPL 2013/2014:- Azam FC hiyoo kwenye Ubingwa wa Ligi Kuu Soka Bara kwa mara ya kwanza.



Kikosi cha Azam FC…ambacho kina Uwezekano wa kuandika historia ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Vodacom Tanzania Bara kwa mara ya kwanza upo karibu, kufuatia kufanikiwa kuifunga Simba SC kwa mabao 2-1 na kuongoza msimamo wa ligi hiyo kwa tofauti ya pointi saba dhidi ya Yanga SC.

Azam FC ambayo haijapoteza mechi yoyote msimu huu, imeonyesha kweli imejipanga baada ya kutoa kipigo hicho kwa Simba ambayo mwaka huu imekuwa ikipepesuka, hivyo kufikisha pointi 53 huku Yanga SC ikishika nafasi ya pili ikiwa na pointi 46.

Mechi hiyo ya Azam FC iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, jana (March 30,2014) jijini Dar es Salaam ilishuhudia Azam FC ikipata bao lake la kwanza kupitia kwa Hamis Mcha katika dakika ya 16 baada ya mabeki wa Simba SC, Joseph Owino na Donald Musoti kujichanganya.

Simba SC ilisawazisha kupitia kwa Owino katika dakika ya 45 kwa kichwa kutokana na mpira wa faulo uliopigwa na Wiliam Lucian.

John Bocco ambaye alikuwa nje muda mrefu kutokana na majeraha, ameonyesha kurejea kwa kasi baada ya kutupia bao la pili kwa Azam  FC katika dakika 56 kutokana na shuti kali la Kipre Tchetche kugonga mwamba na kurejea uwanjani.

Simba SC ilionyesha kuamka katika dakika za mwisho za kipindi cha pili lakini bado mambo yakawa magumu kwao.


Mashabiki wa Yanga SC ambao wengi wao walikuwa wakiipa nguvu Simba ili iifunge Azam kwenye Uwanja wa Taifa, walifanya hivyo ili Azam ipunguzwe kasi kwa kuwa timu hiyo pamoja na Yanga ndizo zinazowania nafasi ya kuwa bingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na ni tukio la kushangaza, ambalo pengine lilionekana ni kama mchezo wa kuigiza, mashabiki wa Yanga, jana Jumapili waliamua kufunika kombe baada ya kuishabikia Simba kwa nguvu zote huku baadhi yao wakiwa na bendera za Msimbazi.
Nao Mabingwa watetezi wa Ligi kuu soka Vodacom Tanzania bara,Yanga SC sasa wapo hatarini kuukosa Ubingwa wa Ligi- hiyo inafuatia Mbeya City kuilaza Prisons bao 1-0 jioni ya leo Uwanja wa Sokoine, Mbeya na kurejea rasmi kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.


Baadhi ya wachezaji wa Mbeya City wakishangilia ushindi…baada ya kutoa kipigo cha bao 1-0 kwa wapinzani wao wa mji mmoja, Tanzania Prisons katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, jana March 30,2014.
Bao pekee la Mbeya City katika mchezo huo wa jana (March 30,3014) limefungwa na Paul Nonga dakika ya kwanza tu ya mchezo na sasa timu hiyo ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya inatimiza pointi 45 baada ya kucheza mechi 23.

Yanga SC baada ya kufungwa na Mgambo JKT mabao 2-1 Uwanja wa Mkwakwani, Tanga inabaki na pointi zake 46 za mechi 22, wakati Azam FC ipo kileleni kwa pointi 53 za mechi 23 baada ya kuifunga Simba SC mabao 2-1 Jana March 30,3014.


Ikiwa sasa inaizidi pointi moja tu Mbeya City, Yanga SC inarejea Dar es Salaam kucheza na JKT Ruvu na baadaye Kagera Sugar kabla ya kucheza na JKT Oljoro na Simba SC.

Matokeo mengine ya Ligi kuu Jana(March 30,3014), Kagera Sugar imelazimishwa sare ya bila kufungana na Ruvu Shooting, Mtibwa Sugar imeifunga mabao 3-1 Coastal Union na JKT Ruvu imeichapa 3-1 Rhino Rangers.


RATIBA YA MECHI ZIJAZO LIGI KUU VODACOM TANZANIA 2013/2014.
 
Jumamosi Aprili 5,2014.

Kagera Sugar v Simba
Ashanti United v Mbeya City

Jumapili Aprili 6,2014.

Coastal Union v Mgambo JKT
JKT Oljoro v Tanzania Prisons
Rhino Rangers v Mtibwa Sugar
Ruvu Shooting v Azam FC
Yanga v JKT Ruvu

Jumatano Aprili 9,2014.

Yanga v Kagera Sugar

**RATIBA INAWEZA KUBADILIKA

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad