|
Godfrey
Mgimwa na Robby Mgimwa wakionesha hati yao ya ubunge baada ya kukabidhiwa March 17,2014.
|
|
Mbunge
mteule wa jimbo la Kalenga Bw Mgimwa akionyesha dole
|
|
Sehemu ya
msafara wake Boda boda nao walikuwepo .
|
Akiwa
ameambatana na mkewe, Robby Mgimwa, Godfrey Mgimwa wa Chama cha Mapinduzi (CCM)
jana alitangazwa mshindi wa ubunge katika uchaguzi mdogo jimbo la Kalenga baada
ya kuvibwaga kwa kura za kishindo vyama vingine viwili vilivyoshiriki uchaguzi
huo.
Katika
uchaguzi huo uliofanyika Jumapili ya Machi 16, mwaka huu, Mgimwa alizoa kura
22, 962 ambazo ni sawa na asilimia 79.32 dhidi ya kura 5,853 sawa na asilimia
20 alizopata Grace Tendega wa Chadema na kura 150 sawa na asilimia 0.52
alizopata Richard Minja wa Chausta.
Msimamizi wa
uchaguzi huo Pudenciana Kisaka ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Iringa jana alimkabidhi Mgimwa hati yake ya kuchaguliwa kuwa mbunge
wa jimbo hilo.
Akizungumza na wanahabari baadaye Mgimwa
alisema anazikumbuka ahadi zote alizotoa kwa wananchi wa jimbo hilo wakati wa
kampeni zake na anajipanga kutekeleza moja baada ya nyingine.
“Kama
mnavyojua nyingi ya ahadi hizo zitatekelezwa kupitia Ilani yetu ya CCM;
nachowahakikishia wananchi wangu wawe na imani kwani mambo yatatekelezwa,”
alisema huku akiwashukuru wapiga kura wa jimbo hilo kwa kumpa ushindi wa
kishindo dhidi ya wapinzani wake.
Pamoja na
Chadema kuleta wabunge wake wote siku tatu kabla ya uchaguzi huo na kutumia
chopa kwenye kampeni zake kabla ya kuitumia kulinda kura siku ya uchaguzi,
Mgimwa alimgaragaza mgombea wa Chadema hata katika kata zilizokuwa zikielezwa
kuwa ni ngome ya chama hicho.
Kata hizo ni
pamoja na Ifunda ambayo Mgimwa alipata jumla ya kura 1,627 dhidi ya 601
alizopata mgombea wa CCM na 13 za mgombea wa Chausta.
Nyingine ni
Nzihi ambayo CCM ilipataa kura 1,793 dhidi ya 606 za Chadema na saba za
Chausta.
Katika kata
ya Magulilwa ambako mgombea wa Chadema ndiko anakotokea, Mgimwa alifanya vizuri
zaidi kwa kupata kura 2,065 dhidi ya kura 549 za Chadema.
Matokeo
ynayofana na hayo yalitokea pia katika kata zingine zote za jimbo hilo; wakati
Mgimwa akipata kati ya kura 1,500 na 3,000, mgombea wa Chadema alipata kati ya
kura 200 na 700 tu.
Huku baadhi
ya wafuasi wa chama hicho wakiangua kilio alisema; “Ninawashukuru makamanda
wenzangu na wanaharakati waliokuwa wanapigania haki Kalenga, wafuasi na
wanachama wa Chadema wote, nawapa pole na hongera kwa kuanza na kumaliza
uchaguzi huu uliokuwa na dosari nyingi,” alisema.
Alisema
maapambano ya ukombozi yana changamoto nyingi na kwamba huo ni mwanzo wa safari
ya mabadiliko makubwa nchini, pale walipokosea mbele ya safari watajipanga
upya.
|
Benson
Kigaila akisisitiza kuyakataa matokeo ya
uchaguzi huo wa Kalenga.
|
Katika
mkutano huo na wanahabaari, Mkurugenzi wa Oparesheni wa Chadema, Benson Kigaila
alisema Chadema haiyakubali matokeo hayo japokuwa haitakakata rufaa mahakamani
kuyapinga.
Alisema
daftari la wapiga kura lililotumika katika uchaguzi huo sio la mwaka 2010 bali
ni lile walilolilalamikia awali kufanyiwa marekebisho mwaka huu.
“Kuna wapiga
kura wengi waliondolewa katika daftari hilo lakini wengine wengi wapya
waliingizwa, tunao ushahidi tuliouwasilisha kwenye kikao tulichofanya na Tume
ya Taifa ya Uchaguzi,” alisema.
Alisema “ni
mwendawazimu pekee ndiye anayeweza kusema kwamba uchaguzi huu wa Kalenga
ulikuwa huru na wa haki, vinginevyo haki ya watanzania inaendelea kuporwa kwa
njia ya masunduku ya kura.”
Alisema yako
mambo ya kisheria yaliyojitokeza wakati wa zoezi la upigaji kura ambayo
watataka ufafanuzi wake kutoka kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa.
“Kuna gari
na watu wetu hawajulikani walipo mpaka sasa, kuna wafuasi wetu walikamatwa
wakapigwa na kuteswa baada ya kukamatwa na watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa
CCM, tunataka kujua wahusika wamechukuliwa hatua gani kwasababu wanafahamika,”
alisema.
Alisema yeye
na baadhi yaa viongozi wa chama hicho hawataondoka mjini Iringa mpaka
watakapopata majibu ya mambo wanayolalamikia.
Jimbo la
Chalinze
Kigaila
alisema wakimaliza kushughulikia changamoto zote zilizojitokeza wakati wa
uchaguzi huo, mapambano yao watayaelekeza katika uchaguzi mdogo jimbo la
Chalinze.
“Kule Chalinze
kampeni zimekwishaanza; tukitoka Iringa breki yetu ni Chalinze; tutapita kijiji
kwa kijiji kuwaeleza watanzania umuhimu wa kuichagua Chadema,” alisema.
Alisema
katika kampeni hiyo wimbo wao mkubwa utakuwa ni fursa sawa kwa watanzania wote
ili kuondokana na tabia inayojengekea ya watoto kurithi nafasi za uongozi za
wazazi wao.
“Wote tuna
haki sawa, Chadema tunataka kuona wakulima, walimu na watu wengine wa kawaida
wanapata fursa katika nchi hii badala ya kuendelea kutoa madaraka kwa watoto wa
wakubwa,” alisema.





No comments:
Post a Comment