![]() |
|
ALLIANCE
FOR CHANGE AND TRANSPARENCY
(ACT TANZANIA)
MABADILIKO
NA UWAZI
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Jumatatu,
03 Machi 2014, Dar es Salaam.
|
1. Utangulizi.
Ndugu wana habari,
Naomba nichukue fursa hii
kuwashukuru kwa kuitikia wito wa kuhudhuria mkutano wetu, ambao ni wa kwanza
tangu chama chetu kianzishwe. Tunatambua na kuheshimu kazi yenu kama mhimili wa
nne wa dola, na leo tunaomba kuzungumza na watanzania kupitia kwenu.
Lengo kuu la mkutano huu ni
kukitambulisha kwenu chama kipya cha siasa kinachoitwa Alliance for Change
Tanzania (ACT Tanzania) na kuwaombeni kukitambulisha chama hiki kwa watanzania
kupitia vyombo vyenu vya habari.
2. ACT Tanzania ni nini?
Ndugu Wanahabari,
ACT Tanzania ni kifupi cha
maneno: Alliance for Change and Transparency, yaaani Umoja wa Mabadiliko na
Uwazi. Ni chama kipya cha siasa kilichoanzishwa kwa lengo mahsusi la kuwaleta
pamoja watanzania wanaoamini kwamba nguvu ya pamoja inahitajika katika kuleta
mabadiliko ya kweli katika nchi hii, na kwamba uwazi na uadilifu ni tunu ambazo
taifa hili linazihitaji sana kwa sasa na baadaye.
3. Itikadi na Misingi ya ACT Tanzania.
ACT Tanzania ni chama kinachoaamini
katika demokrasia jamii na chenye shabaha kuu ya kupigania na kusimamia
mabadiliko na uwazi nchini Tanzania.
ACT-Tanzania inaamini kuwa mabadiliko
yoyote katika jamii lazima yainufaishe jamii husika, na kwamba wananchi wenyewe
ni lazima washiriki katika kuleta mabadiliko hayo kwa uwazi na uzalendo.
Mwongozo wa sera za ACT-Tanzania ni maendeleo shirikishi na kuhakikisha uwepo
wa uongozi adili katika ngazi zote.
ACT Tanzania inaongozwa na misingi
mikuu mitano ifuatayo:-
i) Uzalendo
ACT-Tanzania inaamini kwamba kila
mwananchi ana wajibu wa msingi kabisa wa kutoa mchango wake katika jamii na
Taifa kwa ajili ya kuhifadhi ustawi wa nchi kwa ajili ya kizazi cha leo na cha
baadaye.
Ili wananchi waweze kutoa mchango huu kwa dhati na kwa moyo, ni muhimu
mazingira yawepo ya kuhakikisha kwamba wananchi wanaipenda nchi yao. Kwa msingi
huu, ACT-Tanzania itajenga mazingira mwafaka ya wananchi kuipenda nchi yao ili
wajitoe kikamilifu katika kuijenga na kuilinda.
ACT-Tanzania itajenga mazingira
yatakayoongeza uzalendo wa wananchi kwa kuhakikisha uwepo wa uwazi, ulinzi na
utumiaji bora wa rasilimali za taifa na uadilifu wa viongozi.
ii) Usawa.
ACT-Tanzania inaamini katika usawa
katika yyanja zote.
Tunaamini kwamba mafanikio ya mtu mmoja mmoja na jamii kwa
ujumla yatatokana na bidii katika kazi. Kwahiyo, ACT Tanzania kitapigania
kuwepo usawa wa fursa na mazingira mazuri kwa wote katika kuhakikisha kwamba
kila mtu na kila kundi katika jamii linakuwa na fursa sawa ya kufanya kazi za
kujiajiri au kuajiriwa, na kwamba kipato kitokanacho na kazi halali ndicho
kitakuwa kipimo cha mchango wake katika jamii na taifa.
iii) Uadilifu.
Uadilifu katika maisha binafsi na
katika jamii utakuwa ndio msingi na mwongozo mkuu wa viongozi na wanachama wa
ACT-Tanzania. ACT-Tanzania inaamini kwamba uadilifu ndio msingi na nguzo kuu ya
mapambano dhidi ya rushwa na maovu mengine katika jamii.
iv) Uwazi na uwajibikaji.
ACT Tanzania inaamini katika uwazi
kwenye mambo yote ya kijamii na kitaifa. Hivyo basi viongozi na wanachama wa
ACT-Tanzania wana wajibu wa kupigania uwazi katika mambo yote wanayofanya kwa
ajili ya umma.
Sambamba na uwazi, ACT- Tanzania inaamini kwamba kila mwananchi
na kiongozi mwenye dhamana katika umma ana wajibu katika jamii na Taifa kwa
ujumla na ni jukumu lake kutekeleza wajibu huo bila kinyongo.
Aidha, mwanachama
na kiongozi atokanaye na ACT Tanzania anapaswa kuwajibika kwa maneno na matendo
yake katika utumishi au nje ya utumishi wa chama au taasisi yeyote ya umma.
ACT
Tanzania inaamini kwamba bidii katika kazi ndiyo njia pekee ya kujipatia
maendeleo.. Hivyo basi wajibu mkuu wa mwanachama wa ACT Tanzania utakuwa ni:-
BIDII KATIKA KAZI.
v) Demokrasia ya Kweli.
ACT-Tanzania inaamini demokrasia
ndiyo msingi wa kujenga fikra pevu na kueneza uhuru wa mtu, jamii na Taifa kwa
ujumla.
Hivyo basi, viongozi na wanachama wa ACT-Tanzania watapigania uwepo wa
demokrasia ya kweli katika kila ngazi, ndani na nje ya chama.
Kila jambo lenye
maslahi mapana katika chama na katika umma litaamuliwa kwa njia ya kidemokrasia
ya moja kwa moja au kupitia kwa wawakilishi waliochaguliwa.
4. Taarifa ya Kazi na mipango ya
mbele.
:- ACT Tanzania imekwisha kukamilisha rasimu ya awali ya
Katiba ambaye iliwezesha kupata usajili wa muda.
:- Zoezi la kuandikisha wanachama katika mikoa kwa ajili ya
kuomba usajili wa kudumu kwa mujibu wa sheria limekwishakamilika. Tumewapata
wanachama katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Hata hivyo,
tumechagua mikoa kumi ambayo tungependa msajili akahakiki kama sheria
inavyotaka.
:- Baada ya kukamilisha zoezi la kuandikisha wanachama, wiki
hii kabla ya Ijumaa tutapeleka fomu na mahitaji mengine husika kwa Msajili wa
vyama ili aweze kupanga ratiba ya zoezi la uhakiki.
:- Mara baada ya msajili kutoa usajili wa kudumu kwa muda
atakaopanga, tutafanya uchaguzi wa kwanza mkuu.
:- Kama itampendeza msajili akatupatia usajili wa kudumu
mapema, tunatarajia kushiriki kwa nguvu zote katika chaguzi zote ndogo
zitakazojitokeza, uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani.
5. Shukrani.
:- Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru waratibu wote wa
zoezi zima la uandikishaji wanachama waliojitolea kwenye mikoa na wilaya
mbalimbali katika kuhakikisha zoezi hili linafanikiwa kwa wakati
uliopangwa.
:- Natoa wito kwa wanachama na wapenzi wa chama popote walipo
waendelee kukichangia chama kwa nguvu zao, muda wao, taaluma zao na kwa kila
hali kadri uwezo unavyomruhsu kila moja wetu.
:- Nawashukuru sana wataalam na watafiti wetu mbalimbali ambao
wamekuwa wakijitolea kutumia utaalam wao kutushauri katika maeneo mbalimbali ya
utafiti, uongozi, sera, raslimali, usimamizi wa fedha, mawasiliano, sheria,
sayansi ya siasa, na kadhalika.
6. Wito kwa wanachama na watanzania.
Tunatoa wito kwa kila mwanachama,
mfuasi na mpenzi wa ACT-Tanzania popote walipo nchini kuhakikisha kwamba:-
:- wanazingatia misingi ya chama iliyoanishwa hapo juu katika
shughuli zao zote. Wakukumbuke kila mara kwamba lengo kuu la chama hiki ni
kupigania na kusimamia mabadiliko na uwazi katika kila ngazi.
Tungependa kila
shughuli ya chama iwe shirikishi na wazi kwa wanachama na wananchi kwa
ujumla.
:- Anafanya kazi kwa bidii katika kukijenga chama na kushiriki
maendeleo katika jamii aliyomo,
akizingatia kwamba chama hiki
kinaamini kwamba bidii katika kazi ndiyo njia pekee ya kujipatia maendeleo kwa
mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla.
Hivyo, kila mwanachama ahakikishe anatoa
mchango wake katika kukijenga chama na kuleta maendeleo katika jamii husika
aliyomo.
:- Tunawakaribisha watanzania wote popote walipo na wanaoamini
katika misingi tuliyoainisha hapo juu kujiunga na ACT Tanzania.
Kila mtanzania
anayejiunga na chama hiki akumbuke kuchukua wajibu wake katika kukijenga chama
popote pale alipo. Na akumbuke wajibu mkuu kwa mujibu wa chama hiki kuwa ni:-
BIDII KATIKA KAZI.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu
ibariki ACT-Tanzania, ahsanteni kwa kunisikiliza!
Kadawi Lucas Limbu,
Mwenyekiti wa Taifa
ACT Tanzania






No comments:
Post a Comment