Taarifa ya
Tume hiyo kwa umma wa Watanzania, iliyosambazwa jana kwenye vyombo vya habari,
ilisema hatua hiyo ya kutoa ufafanuzi katika baadhi ya maeneo imetokana na kile
kinachoelezwa na Tume hiyo kuwa shauku kubwa ya wananchi kutaka ufafanuzi wa
mambo mbalimbali kuhusu Rasimu ya Katiba baada ya hotuba ya Rais Kikwete.
Kwa mujibu
wa taarifa hiyo, ufafanuzi huo umetokana na kikao cha tathmini kilichofanywa na
wajumbe wa iliyokuwa Tume hiyo ya Warioba, kilichofanyika Jumatatu wiki hii ya
Machi 24, mwaka huu jijini Dar es Salaam, baada Tume kuhitimisha kazi yake
hiyo.
Maeneo
ambayo Tume hiyo imeyafanyia ufafanuzi ni pamoja na Usanifu wa Katiba; Malengo
muhimu na mwelekeo wa shughuli za Serikali na sera za kitaifa (Dira); Nchi
mbili, Serikali mbili; Mamlaka ya Rais; Orodha ya mambo ya Muungano; Katiba na
Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mamlaka ya Mahakama ya Rufani na
takwimu kuhusu maoni ya wananchi juu ya muundo wa Muungano.Ufafanuzi kamili ni
kama ifuatavyo:-
UTANGULIZI.
Tume ya
Mabadiliko ya Katiba katika kutekeleza majukumu iliyopewa imetoa taarifa ya
Tume yenye viambatisho vingi na vyenye maelezo ya kina kuhusu mchakato wa
kuratibu, kukusanya, kuchambua maoni ya wananchi na kuandaa ripoti.
Baada ya
kukamilisha kazi hiyo, Tume iliwasilisha Rasimu ya Katiba katika Bunge Maalumu
la Katiba Machi 18, mwaka huu. Pamoja na Rasimu hiyo, Tume iliwasilisha Randama
ya Rasimu ya Katiba na Bango kitita la Randama ya Rasimu ya Katiba ambayo
ilitoa maelezo ya kila Ibara ya Rasimu ikitoa maudhui, madhumuni na lengo
pamoja na sababu za mapendekezo ya kila Ibara.
Tangu
kuwasilishwa kwa Rasimu na vyaraka zilizoambatana nayo katika Bunge Maalumu la
Katiba, kumejitokeza tafsiri tofauti kuhusu baadhi ya mapendekezo yaliyomo
kwenye Rasimu ya Katiba na baadhi ya taarifa zilizoambatana na Ripoti ya Tume.
Katika maeneo ambayo kumekuwepo na tafsiri tofauti tofauti, ufafanuzi wa kina
umetolewa kwenye Randama na bango kitita ya Randama ya Rasimu ya Katiba.
Kutokana na
hali hiyo, Tume ya Mabadiliko ya Katiba, katika kikao chake cha tathmini ya
kuhitimisha kazi kilichofanyika Machi 24, mwaka huu, jijini Dar es Salaam,
imeamua kutoa maelezo ya ziada ya ufafanuzi kama ifutavyo:-
NCHI MBILI
SERIKALI MBILI.
Tangu Mwaka
1984 hatua ambazo zimechukuliwa na serikali zote mbili za Muungano na Zanzibar
zimeifanya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka kuwa Nchi Moja yenye Serikali
mbili na kuwa Nchi mbili zenye Serikali mbili. Kwa maana nyingine Masharti
yaliyomo katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano yanaelekeza kwamba Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ni Nchi moja yenye Serikali mbili- Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kufuatia Mabadiliko
ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984, Zanzibar imetamka ni Nchi tofauti na
ilivyokuwa imetamka kwamba ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano kabla ya Mabadiliko
hayo.
Wakati
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni Nchi moja, Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania lilikuwa na Mamlaka ya Kutunga Sheria juu ya Mambo ya
Muungano kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yote, sasa uwezo huo umewekewa
mipaka na Katiba ya Zanzibar Katika Ibara ya 132 ambayo inaelekeza kwamba
Sheria iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kabla ya
kuanza kutumika Zanzibar ipelekwe kwenye Baraza la Wawakilishi na kupata ridhaa
ya kutumika Zanzibar .
Zipo Sheria zilizotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania zilipokosa ridhaa ya Baraza la Wawakilishi zilirejeshwa katika
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kufanyiwa marekebisho ili kukidhi
maelekezo ya Baraza la Wawakilishi, kwa mfano, Sheria ya Haki za Binadamu na
Utawala Bora (Commission for Human Rights and Good Governance Act) na Sheria ya
Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu (Deep Sea Fishing Authority Act)
MAMLAKA YA
RAIS.
Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 imempa Rais wa Jamhuri ya
Muungano mamlaka ya kuigawa Jamhuri ya Muungano katika maeneo ya kiutawala
katika Mikoa na Wilaya. Hata hivyo, Marekebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya
Mwaka 1984 yanampa Rais wa Zanzibar Mamlaka kama hayo ya kuigawa Zanzibar bila
kufanya marekebisho stahiki ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 1977. Kwa
mantiki hiyo mamlaka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano yamepungua na kubaki kwa
Tanzania Bara tu.
MAMLAKA YA
MAHAKAMA YA RUFANI.
Katiba ya
Muungano ya 1977 imetoa mamlaka ya kusikiliza rufaa nchi nzima. Lakini Zanzibar
imezuia Mahakama hiyo kusikiliza rufaa kutoka Mahakama za Kadhi, kutafsiri
Katiba ya Zanzibar na rufaa kuhusu mashauri ya haki za binadamu.
Kwa kifupi:
Waasisi
walituachia mambo 21 (ukiacha usajili wa vyama) kwenye orodha ya Muungano.
Katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita yamepunguzwa. Mambo yote yaliwekwa
kwa utaratibu uliowekwa na Katiba lakini yameondolewa kinyume na Katiba.
Sehemu
zote mbili ziliamua kuachia baadhi ya mambo yake kuwa chini ya Serikali ya
Muungano, sasa sehemu moja inaondoa mambo yake. Kwa hiyo serikali ya Muungano
itakuwa inashughulikia zaidi mambo ya upande mmoja.
Waasisi
walituachia Bunge lenye madaraka nchi nzima. Sasa ni lazima lipate idhini ya
Baraza la Wawakilishi.
Waasisi
waliacha Rais akiwa na madaraka kamili. Madaraka hayo yamepunguzwa bila kufuata
utaratibu wa Katiba.
Waasisi
walituachia Mahakama ya rufani yenye madaraka kamili. Madaraka haya
yamepunguzwa.
Waasisi
waliunganisha nchi mbili ikawa moja. Sasa tunazo nchi mbili.
Hii ndiyo
inafanya wananchi wa Tanzania Bara waamini Zanzibar ni huru katika mambo yao.
Wanaona ina mamlaka kamili kushughulikia mambo yake na imechukua rasilimali
zake.
Serikali ya Muungano imebaki na mamlaka na rasilimali za Tanzania Bara.
Wabunge wa Zanzibar wanashiriki kuamua mambo ya Tanzania Bara lakini wabunge wa
Tanzania Bara hawana nafasi ya kushiriki katika kuamua mambo ya Zanzibar.
Tume iliona
ni vigumu kwa Zanzibar kurudi kwa hiyari kwenye hali ya awali, yaani kurudisha
mambo yote yaliyotolewa kwenye orodha ya Muungano, kurudisha madaraka ya Rais
na kufuta kipingere cha nchi mbili kwenye Katiba yake.
Tume iliona kwamba
pamoja na mambo haya kufanywa kinyume na Katiba ya Muungano hali ibaki hivyo
hivyo. Lakini kwa kufanya hivyo basi malalamiko ya Tanzania Bara nayo
yasipuuzwe. Hivyo Tume nayo ikapendekeza Serikali ya Tanganyika iundwe.
HITIMISHO.
Tume
inapenda kuwashukuru wananchi wote kwa shauku kubwa ya kutaka ufafanuzi wa
mambo mbalimbali kuhusu Rasimu ya Katiba.






No comments:
Post a Comment