Idadi kubwa ya Watanzania ni watoto huku mikoa ya Simiyu, Rukwa na Geita .....'' - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Friday, March 14, 2014

Idadi kubwa ya Watanzania ni watoto huku mikoa ya Simiyu, Rukwa na Geita .....''


Idadi kubwa ya watu nchini ni watoto wenye umri wa chini ya miaka 15 na vijana huku mikoa ya Simiyu, Rukwa na Geita ikitajwa kuwa zaidi ya nusu ya watu wake, ni watoto.

Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dk Albina Chuwa alimweleza hayo Rais Jakaya Mrisho Kikwete jana Ikulu wakati akimkabidhi vitabu na majedwali yenye matokeo na machapisho ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012.

Alisema asilimia 44 ya watu wote hapa nchini Tanzania, ni watoto wenye umri chini ya miaka 15.

Alisema utafiti wa Mama na Mtoto wa Mwaka 2010, unaonesha kuwa kiwango cha uzazi ni wastani wa watoto 5.4 kwa kila mama mwenye umri wa kuzaa ambao ni miaka 15 hadi 49.

Sera ya Vijana Tanzania ya Mwaka 2007 inatambua vijana kuwa ni watu wote wenye umri wa kati ya miaka 15 na 35, ambao kulingana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 ni asilimia 34.7 ya watu wote nchini.

Kulingana na Takwimu, idadi ya watu Tanzania imeongezeka zaidi ya mara tatu kutoka watu milioni 12.3 kwa mwaka 1967 hadi watu milioni 44.9 mwaka 2012.

Takwimu hizo zinaonesha Mkoa wa Dar es Salaam una asilimia kubwa ya vijana wakati Mkoa wa Singida, ukiwa na asilimia ndogo zaidi. 

Kulingana na takwimu, zaidi ya nusu ambayo ni asilimia 52.2 ya watu wote nchini, wako katika umri wa kufanya kazi huku Dar es Salaam ikiongoza.

Mkoa wa Simiyu uko chini zaidi kwa kuwa na asilimia 45.5 ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi. 

Katika takwimu hizo, zaidi ya nusu ya watu katika mikoa ya Simiyu, Rukwa na Geita ni watoto wenye umri wa chini ya miaka 15.

Takwimu zinaonesha asilimia 5.6 ya watu nchini ni wazee na takwimu hizi zinaonesha kuwa wazee kwa asilimia kubwa wako katika mikoa ya Kilimanjaro, Mtwara, Lindi na Pwani.

Asilimia ndogo zaidi ya wazee iko katika mikoa ya Dar es Salaam na Mjini Magharibi.
Kwa mujibu wa Sera ya Wazee Tanzania, mzee ni mtu mwenye umri wa miaka 60 au zaidi.

Aidha takwimu zinazidi kuonesha kuwa asilimia ya watu wanaoishi mijini imeongezeka zaidi ya mara tano, ambapo ni asilimia 6.4 mwaka 1967 na kufikia asilimia 29.6 kwa mwaka 2012.

Jiji la Dar es Salaam lina asilimia 10 ya watu wote Tanzania Bara wakati Mjini Magharibi ina asilimia 46 ya watu wote wa Zanzibar.

Sensa pia imeonesha wanawake ni wengi zaidi , kwa asilimia 51 ukilinganisha na wanaume ambao ni asilimia 49 kama ilivyo katika nchi nyingi Afrika. 

Mkoa wa Manyara unaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanaume na Njombe una idadi ndogo zaidi ya wanaume.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad