Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amestushwa na kuhuzunishwa na ajali kubwa iliyotokea usiku wa Jumamosi, Machi
29, 2014, katika Mkoa wa Pwani ikihusisha magari matano na kusababisha vifo vya
watu 21 na majeruhi 11.
Rais Kikwete amevielezea vifo hivyo kuwa siyo vya lazima na ni upotevu wa
bure wa maisha ya Watanzania.
Katika salamu za rambirambi ambazo amemtumia Mkuu wa Mkoa wa Pwani,
Mheshimiwa Mwantumu Bakari Mahiza, Rais Kikwete amesema: “Nimeshtushwa
na kusikitishwa na taarifa ya ajali iliyohusisha magari matano na iliyotokea
jana usiku katika Kijiji cha Kibupa, kilichoko kati ya Ikwiriri na Kibiti,
Wilaya ya Rufiji, Mkoa wa Pwani, ambako maisha ya Watanzania wenzetu 19
yamepotea na wengine 11 kujeruhiwa.”
“Kufuatia ajali hiyo, nakutumia wewe Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mheshimiwa
Mwamtumu Bakari Mahiza salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kuomboleza
vifo vya Watanzania wenzetu hao. Nimefadhaishwa mno na ajali hiyo ambako pia
wenzetu wengine 11wameumia.”
“Aidha, kupitia kwako, nawatumia ndugu, jamaa na marafiki ambao
wamepoteza wapendwa wao katika ajali hiyo. Naelewa machungu yao katika kipindi
hiki na niko nao katika kuomboleza upotevu huu mkubwa wa maisha ya wenzetu.
Msiba wao ni msiba wangu na machungu yao ni machungu yangu. Nawaombea subira na
uvumilivu katika kipindi hiki kigumu na naungana nao kumwomba Mwenyezi Mungu,
Mwingi wa Rehema, aziweke peponi roho za marehemu.”
Rais pia amewapa pole wote walioumia katika ajali hiyo mbaya akisema:
“Mkuu wa Mkoa nakuomba pia uwafikishie pole zangu nyingi wote ambao wameumia
katika ajali hiyo. Nawaombea Baraka za Mwenyezi Mungu ili wapone haraka
na wapate tena nafasi ya kuendelea na shughuli za kuboresha maisha yao.”
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
30 Machi,2014.
>>>Awali ajali hiyo ilihusisha magari mawili, Toyota Hiace (T 948 CUX),
iliyokuwa ikitokea Ikwiriri kuelekea Rufiji ambalo lilikwenda kukwaruzana na
Lori(T 132 AFJ) kwa nyumba, ambalo lilikuwa limeharibika na kusimama barbarani.
Alisema baada ya kulikwaruza roli hilo, mlango wa Hiace uling'oka na
kubaki kwenye roli ambapo gari hiyo lilipoteza mwelekeo na kwenda kugongana uso
kwa uso na gari nyingine aina ya Canter(T 774 CJW) na kupinduka.
"Katika ajali hii, watu 14 walifariki dunia papo hapo, wakati polisi
na baadhi ya wananchi wakiendelea kuwaokoa majeruhi ili wakimbizwe hospitali,
likatokea basi la kampuni ya Mining (President)( T 242 BXA), kuwakanyaga watu
waliokuwa wakitoa msaada na kuwaua ndio maana idadi ya waliokufa imefikia 21.
"Basi hili lilikuwa linatoka Lindi kuelekea Dar es Salaam...polisi
walifanya jitihada za kulisimamisha lakini dereva wake alikataa kusimama na
kwenda kukanyaga watu lakini tayari tumemkamata, majeruhi mmoja amehamishiwa
Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam," alisema Kamanda Matei.
Kamanda Matei alisema, basi hilo linashikiliwa polisi ambapo uchunguzi
ukikamilika, dereva wake atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka.
Aliwataja waliokufa ni Sixtus Ally Mtanga(32) na Nassoro Mohamed
Kajani(20) wakazi wa Ikwiriri, Juma Said Kitambulilo(30) na Salum Goma Makonde
(50), Ustaadhi Kalilambwe(34) na Shafil Kip (30), Wasabi Sabil(45), Ramadhani
Ally (23)wote wakazi wa Mbagala.
Shabani Bakari(30) Kondakta wa Hiace, mkazi wa Kibiti, Masud Abulal (27),
mkazi wa Mkuranga, Ammi Mpemba (30)na Madadi Hassan Mangasongo (45) wakazi wa
Jaribu na Japhet Ponsian (24), mkazi wa Dar es Salaam.
Pia yupo Said Ally China (21) mkazi wa Kimanzichana, mkazi wa Jaribu,
Abdalahaman Yusuph Kihemke(45), mkazi wa Kongowe na Fikiri Said Sauze, mkazi wa
Vikindu.
Wengine ni Nywari Mshigani mkazi wa Dar es Salaam, Hassan Wasabi (18),
mkazi wa Kibiti na Seleman Mcharazi (47) mwingine aliyejulikana kwa jina moja
la Mustafa, wote wakazi wa Mbagala na maiti ya mwanamke haijafahamika jina
lake.
Waliojeruhiwa katika ajali hiyo ni Frank Sixmundi (31), dereva wa gari la
Maliasili Kibiti ambaye alifika eneo ili kutoa msaada kwa majeruhi ambaye
ameumia kichwani, Mohamed Salehe (49) na Charles Rogasani (23), wote wakazi wa
Kibiti na Mohamed Mengine (42), mkazi wa Dar es Salaam.
Wengine ni Mniko Magige Mango (54) na Abdalah Issa (25) wakazi wa
Mkuranga, Khalid Salum (32), mkazi wa Dar es Salaam, Ahmad Yusuph (23), mkazi
wa Kigamboni na Shomari Yusuph (42), mkazi wa Mburahati. Majeruhi wamelazwa
katika hospitali za Ikwiriri, Misheni ya Mchukwi na wengine hospitali ya Taifa
Muhimbili.






No comments:
Post a Comment