Katika kuelekea uchaguzi mkuu huo
niliitisha mkutano na waandishi wa habari ambapo nilitangaza ilani yangu ya
uchaguzi.
Lengo la ilani ilikuwa ni kuwaeleza wadau na wapenzi wa mpira
wa miguu Tanzania dira ambayo ingeongoza mpira wetu iwapo ningechaguliwa kuwa
Rais wa TFF.
Aidha niliahidi iwapo ningechaguliwa tungekutana katika
chumba hiki hiki baada ya siku 100.
Ninapenda nichukue fursa hii
kuwashukuru na kuwapongeza wajumbe wote wa Mkutano Mkuu wa TFF, walionipa
kura na ambao hawakunipa kura, kwa kukamilisha vyema zoezi la uchaguzi
huo.
Uchaguzi umekamilika kazi iliyobakia mbele yetu ni kutekeleza
majukumu yetu kama viongozi wa mpira miguu Tanzania.
Ilani na Utekelezaji wake
Ilani yangu ya uchaguzi iliainisha
maeneo kadhaa ya kupewa vipaumbele. Nitakumbushia maeneo haya na kueleza
hatua tulizofikia katika utekelezaji wake:
1.
Idara ya Ufundi
1.1
Kikao cha Kamati ya Utendaji
kilichokaa tarehe 23 Novemba, 2013 pamoja na mambo mengine kilipitisha muundo
mpya wa Sekretariati ya TFF. Muundo huo unaelezwa katika chati hii hapa
chini:
Katika muundo huu Idara ya
Ufundi imepanuliwa kwa kuundwa vitengo vya Ufundi,Elimu na Maendeleo ya mpira.
Aidha katika kutekeleza azma ya
kuboresha usimamizi wa mpira wa vijana (Youth Football) Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania limeamua kuajiri Desk Officer wa vijana yaani msimamizi maalum
wa mpira wa vijana na tayari ameajiriwa.
Zoezi la kuimarisha Idara ya Ufundi
kwa kuajiri Mkurugenzi wa Ufundi pamoja na Wakurugenzi wake Wasaidizi
linaendelea.
1.2
Ujenzi wa Kituo cha Mpira (Football
Centre of Excellency)
Limekuwa ni jambo la kufurahisha na
kutia moyo kuwa mara baada ya kuingia madarakani Serikali kupitia Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ilitufahamisha juu ya uamuzi wa Serikali,
kwa kushirikiana na Kampuni ya SYMBION ya Marekani na Klabu ya Mpira ya
SUNDERLAND ya Uingereza, wa kujenga kituo cha michezo (Sports Centre) Kidongo
Chekundu , Ilala na kujenga kituo cha kulea na kukuza vipaji vya vijana (Elite
Academy) Wilayani Kinondoni.
Wizara ilinikutanisha na Uongozi wa SYMBION
na mazungumzo yanaendela kuona ni jinsi gani mradi huu utashirikisha Serikali,
Mshirika wetu SYMBION, Klabu ya SUNDERLAND na TFF ambao kwa mujibu wa katiba
yetu ndio waratibu na wasimamizi wa maendeleo ya mpira wa miguu
Tanzania. Vikao kadhaa vimefanyika na mwelekeo ni mzuri sana.
Tunaamini mradi huu utatoa mchango mkubwa sana katika kuendeleza mpira wa
vijana (Youth Football).
Aidha kamati ya utendaji ya TFF
imeviagiza vyama vyote vya mpira vya mikoa kuomba kumilikishwa viwanja vikubwa
katika maeneo mapya yanayopimwa, TFF italipia malipo yote yatakayotakiwa.
Mkoa wa Tanga tayari wametekeleza agizo hili na hati imekwisha toka.Msanifu
tayari anaanda michoro ya awali kwa ajili ya kujenga kituo cha michezo katika
ardhi hii. Mfano wa mchoro wa kituo hiki ndio utakaotumika nchi nzima iwapo
utapitishwa na kamati ya utendaji.
1.3
Timu Kupanda Daraja
TFF tayari imeunda Kamati ya dharura
(Adhoc) ya kuangalia mapungufu yaliyopo katika utaratibu wa sasa wa kuwa na
timu 14 za Ligi Kuu na 24 za Ligi Daraja la Kwanza ili tuone ni kwa jinsi gani
tutaweza kuboresha Ligi yetu.
Ripoti ya Kamati ikikamilika italetwa mbele
ya Kamati ya Utendaji kwa ajili ya maamuzi ya mwisho.
1.4
Kuanzisha Mashindano Mapya na
Kufufua ya Zamani
Juhudi zinaendelea kuhakikisha
mashindano ya Kombe la Taifa yanafufuliwa. Aidha taratibu za kuanzisha
upya Kombe la Shirikisho (Federation Cup) ambalo litakuwa ni la mtoano nchi
nzima zimefikia hatua nzuri na muda si mrefu taratibu zake zitatangazwa
pindi mshirika wetu atakapokuwa amemaliza maandalizi upande wake.
1.5
Mpira wa Wanawake
1.5.1
Katika kuhakikisha mpira wa wanawake
unatengenezwa mkakati maalum wa maendeleo matayarisho ya mpango wa maendeleo ya
mpira wa wanawake (women football development plan) yamekamilika na
yatawasilishwa katika kikao kijacho cha Kamati ya Utendaji kwa ajili ya maamuzi
ya mwisho. Mpango huu utatoa dira ya maendeleo ya mpira wa miguu kwa
miaka mitano ijayo na utakuwa ni sehemu ya mpango kazi wa TFF wa miaka
mitano.
1.5.2
TFF inayo furaha pia kuufahamisha
umma wa wapenda mpira wa Tanzania kuwa shula ya kukuza na kuendeleza vipaji ya
Alliance Mwanza kwa kutambua mapungufu yaliyopo katika kuendeleza mpira wa
wanawake kuanzia mwaka huu imeanzisha mafunzo maalum ya mpira wa watoto wa kike
umri chini ya miaka 10. Matunda yake tutayaona baadaye. Hawa watakuzwa na
kulelewa pamoja.
1.5.3
Jitihada zinafanyika kuanza
mashindano ya kitaifa ya wanawake na muda si mrefu utaratibu wake utatangazwa
baada ya mshirika wetu kumaliza maandalizi yake.
1.5.4
TFF kwa kushirikiana na Wizara ya
Wanawake na Jinsia ipo katika kuandaa mpango kazi wa kushirikiana na vyuo
55 vya Ustawi wa Jamii Tanzania katika kuanzisha masomo maalum kwa wasichana
katika vyuo nchini, masomo ambayo yatahusisha ufundishaji wa mpira wa wanawake,
urefa, ukocha na utawala wa mpira. Lengo ni kutoa fursa kwa wasichana
kujifunza stadi hizi kama sehemu ya masomo yao katika vyuo vya maendeleo ya
jamii. Utaratibu wa mpango huu unasimamiwa na chama cha mpira wa migu wa
wanawake (TWFA) na taasisi nyingine husika.
1.5.5
Pamoja na ufinyu wa bajeti tulionao
na timu zetu za wanawake kutokuwa na udhamini TFF bado inahakikisha timu zetu
za wanawake zinashiriki michuano yote ya kimataifa.Wiki iliyopita timu yetu ya
Taifa ya wanawake imesajiliwa kushiriki mtoano wa kushiriki fainali za All
Africa games Congo Brazzavile 2015.
1.6
Maandalizi ya Vijana
(Grassroot Football)
Mpango kazi wa maendeleo ya mpira wa
miguu wa vijana Tanzania (Tanzania youth development plan)
maandalizi yake yamekamilika na utazinduliwa muda si mrefu.
Vipaumbele vikuu vya mpango huu ni pamoja na:
1.6.1
Kuhakikisha shule zote za msingi
16,000 za Tanzania zinakuwa na viwanja vya kuchezea mpira,
mwalimu mmoja wa mpira na zinapata kwa mwaka angalau mipira 10 ya
size 3 na 4 pamoja na jozi angalau 30 za viatu.
TFF tayari inawasiliana na Mashirika
mbalimbali yasiyo ya kiserikali ili yatukusanyie vifaa vya mpira vilivyotumika
(has viatu) ili viweze kuletwa na kugawiwa kwa watoto wetu kwenye shule za
msingi na academies. Kwa sasa tayari kontena mbili za vifaa hivi
zimekwisha kusanywa nchini Uingereza na utaratibu wa kuzileta
unafanyika. Lengo ni kuingiza nchini jozi za viatu 500,000 kwa mwaka na
mipira 160,000 ya size 3 na 4 kwa mwaka. TFF inaomba ushirikiano wa
Serikalini, Taasisi za Umma, Makampuni Binafsi na Taasisi zisizo za kiserikali
katika kuhitimisha azma hii.
1.6.2
TFF ilipata fursa ya kukutana na
Balozi wa Uholanzi hapa nchini na kufanya naye mazungumzo. Nia na lengo
ilikuwa ni kuangalia ni kwa jinsi gani Uholanzi inaweza kutusaidia kufundisha
walimu wa walimu (trainer of trainers). Matumaini yetu ni kuwa walimu
hawa wakishafuzu watakuwa na jukumu la kuwafundisha walimu wa michezo wa
shule za msingi kwa kushirikisha vyuo vya walimu vinavyotoa taaluma hii kama
Malya, Murutunguru na Butimba.
1.6.3
TFF kwa kushirikiana na taasisi
isiyo ya kiserikali inaangalia uwezekano wa kujenga vituo vya michezo 169
katika Wilaya zote 169 Tanzania. Vituo hivi pamoja na kufundisha mpira
vitakuwa pia ni vituo maalum vya kuwafundisha vijana juu ya athari za matumizi
ya dawa za kulevya.
1.6.4
TFF kupitia Idara yake ya Ufundi na
Kamati ya Vijana iko mbioni kufanya sensa ya vituo vya kukuza na kulea vipaji
vya vijana (Academies) pamoja na vituo vya mpira (Sports Centres) nchini kote
Tanzania. Utaratibu unafanywa wa kuweka vigezo vya kutambuliwa vituo hivi
na TFF itaanzisha utaratibu wa kusajili na kutoa vyeti vya usajili kwa vituo
vitakavyokidhi vigezo. Lengo ni kuweka utaratibu nchini wa kusimamia na
kuendeleza vituo hivi kitaifa.
1.6.5
Mpango wa muda mfupi wa TFF ni
kuandaa timu ya Taifa ya vijana itakayoshiriki mashindano ya Fainali za Afrika
umri chini ya miaka 17 mwaka 2019. Tanzania tumeomba uenyeji wa Fainali
hizi. Mwaka huu wa 2014 TFF itafanya mashindano maalum ya vijana chini ya
umri wa miaka 12 ili kuunda timu ya Taifa ya kuanzia ya U12, timu ambayo itakua
pamoja kuelekea 2019. Malengo ni kuiboresha timu hii kila mwaka kwa
kuongeza vijana U13 mwaka 2015, U14 mwaka 2016, U15 mwaka 2017 na mwishowe U16
mwaka 2018.TFF imekwisha pata mshirika wa mpango huu na akimaliza maandalizi
yake atatangazwa rasmi.
1.6.6
Ili Tanzania ifundishe mpira
unaofanana nchini kote, utaratibu unafanyika wa kuandaa mtaala wa kufundisha
mpira (National football curricullum). Mtaala huu unaandaliwa na Idara ya
Ufundi ya TFF kwa kusaidiana na Mtaalam wa mpira toka Uholanzi. Mtaala
huu ukikamilika utakuwa nyenzo muhimu ya kufundishia mpira mashuleni na kwenye
Academies.
1.7
Tiba, Waalimu na Makocha
TFF imeandaa mpango wa kukutana na
wenyeviti wa vyama vya Tiba, Waamuzi na Makocha ili kupanga nao mikakati ya
maendeleo ya kitaaluma. Mikakati hii ikiwa tayari itajumuishwa katika
mpango mama wa maendeleo wa TFF (TFF National Business Plan), mpango
ambao maandalizi yake yatakamilika ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa.
1.8
Utawala
TFF imeanza kwa kuboresha mazingara
ya utendaji wa kazi. Vyama shiriki TAFCA, FRAT, TASMA, TWFA na SPUTANZA
tayari vimepatiwa ofisi za kisasa katika eneo la Ilala. Ofisi kuu za TFF
nazo ziko mbioni kuhamia katika jengo la kisasa la PPF Tower,nia ikiwa ni
kuiwekea sekretariet ya TFF mazingira ya kisasa ya kufanyia kazi na pia kupisha
ujenzi wa kitega uchumi eneo letu la Uwanja wa Karume.
Aidha TFF imeunda kamati maalum
(Adhoc) ya kupitia Muundo wa Bodi ya Ligi lengo likiwa ni kutekeleza maagizo ya
Mkutano Mkuu wa TFF ulioagiza Bodi ya Ligi iundwe ikiwa ni ya mpito kuelekea
uundwaji wa Kampuni ya kuendesha Ligi Kuu ya mpira wa miguu.
1.9
Mahusiano na Zanzibar
Mahusiano kati ya TFF na Chama cha
mpira Zanzibar (ZFA) yamezidi kuimarishwa kufuatia ziara kadhaa ambazo
tumezifanya kati ya maeneo yetu mawili. Mipango ya kuimarisha timu zetu
za Taifa za wakubwa, za vijana na za wanawake inafanywa kwa pamoja.
Juhudi za kuhakikisha Zanzibar inajiunga na FIFA pia zinaendelea kupitia
mazungumzo na wahusika.
1.10
Vilabu vya Mpira
Mara baada ya kuingia madarakani Uongozi wa TFF ulikutana na viongozi wa vilabu
vyote vya Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza. Kikao hiki kilifanyika kama
sehemu ya kuangalia ni maboresho gani yafanyike ili kuongeza ufanisi katika
uendeshaji wa Ligi zetu. Utekelezaji wa maazimio ya kikao hicho
unaendelea kupitia wahusika mbalimbali.
1.11
Wachezaji
SPUTANZA wameleta TFF mapendekezo yao ya jinsi ya kuboresha maslahi ya
wachezaji wa mpira wawapo mpirani na baada ya kustaafu kucheza soka. TFF
inayafanyia kazi mapendekezo hayo. Lakini kubwa litakuwa ni kuanzisha
Mfuko Maalum (Trust Fund) utakaochangiwa na wachezaji wakiwa bado wanacheza
pamoja na TFF na taasisi nyingine ili mfuko huu uwasaidie pindi wakistaafu.
1.12
Masoko na Uwekezaji
Kama nilivyoeleza hapo juu TFF iko mbioni kuwekeza katika Kiwanja cha Karume,
lakni pia njia nyingine za kuiongezea TFF mapato ziko mbioni kuanzishwa ikiwa
ni pamoja na kuanzisha utaratibu maalum wa kuuza jezi za Timu ya Taifa (replica
shirts).
1.13
Kitengo cha Habari
TFF imeandaa utaratibu wa kuboresha kitengo hiki kwa kukiongezea nguvu kazi ili
upashanaji wa habari uwe ni wa haraka zaidi ikiwa ni pamoja na TFF kuanzisha
Blog yake,kuboresha Tovuti yake, na kuwa na kurasa kwenye mitandao ya
kijamii kama Instagram, Facebook, Twitter, n.k. Press officer ataajiriwa punde
ili kuimarisha kitengo hiki.
1.14
Viwanja
Wakati tunaingia madarakani FIFA kupitia mpango wake wa maendeleo ilikuwa
imekwisha tenga pesa kwa ajili ya kuweza nyasi bandia uwanja wa kihistora
wa Nyamagana jijini Mwanza. Uongozi wetu kwa kushirikiana na Wizara
ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Mwanza na Meya wa Manispaa ya Mwanza tulifuatilia kwa karibu na kufanikiwa
kuondoa dosari zilizokuwa zimekwamisha mradi huu. Utandazaji wa nyasi
bandia utaanza mara moja kuanzia sasa.
Kwa mafanikio haya Tanzania tuna viwanja vyenye/ vitakavyokuwa na nyasi bandia
baadae ambavyo ni Gombani Pemba, Amani Zanzibar,Uwanja wa Uhuru, Uwanja wa Karume,
Uwanja wa Azam Chamazi na Uwanja wa Nyamagana.
TFF iko mbioni kuanza mazungumzo na baadhi ya vyama vya siasa ambavyo ni
wamiliki wa viwanja kadhaa vya mpira ili kuangalia uwezekano wa kuingia ubia
kwa nia ya kuviendeleza.
1.15
Timu ya Taifa (Taifa Stars)
Ili kuandaa mkakati maalum wa kuboresha timu ya Taifa TFF iliitisha kikao
maalum cha walimu wa mpira waandamizi. Kikao hiki kilifanyika Zanzibar
kati ya tarehe 06-07 Desemba, 2013 na kilitoka na maamuzi kadhaa. Tarehe
18-19 Januari, 2014 TFF iliitisha kikao kingine maalum cha Makatibu 30 wa vyama
vya mpira vya mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar ajenda ikiwa ni
uboreshaji wa Timu ya Taifa (Taifa Stars). Matunda ya vikao hivi ni mpango kazi
maalum ulioandaliwa wa kuboresha timu ya Taifa kwa kushirikiana na
washirika wetu Tanzania Breweries ltd kupitia bia yao ya Kilimanjaro Lager.
Mpango huu utatangazwa rasmi wiki ya pili ya mwezi February 2014.
CHANGAMOTO.
Uongozi
mpya tangia umeingia madarakani umekutana na changamoto kadhaa. Baadhi yake ni
kama hizi zifuatazo:
1.Tiketi
za Elektronik.
Uongozi
mpya ulipoingia madarakani ulikuta awamu iliyopita ilikwisha saini mkataba wa
mradi huu.Jukumu la uongozi wangu ni kutekeleza masharti ya mkataba. Changamoto
nyingi zimejitokeza ikiwa ni pamoja na mitambo kuzima mara kwa mara,mitambo
kufanya kazi kwa spidi ndogo , mageti yaliyofungwa mashine hizi kuwa machache
(mfano Mkwakwani yamefungwa mitambo miwili katika uwanja unaoingiza watu zaidi
ya elfu kumi,uwanja wa Taifa mitambo 48 wakati unaingiza watu 60,000,linganisha
na uwanja wa Emirates London unaoingiza watu 60,000 mitambo imefungwa
125,karibia mara tatu ya uwanja wetu wa Taifa). Pia uelewa mdogo wa wadau
kuhusu taratibu za utumiaji tiketi hizi nao ni tatizo na mkataba wa TFF na CRDB
unaitaka TFF ibebe jukumu la kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi ya tiketi
hizi na bajeti yake haipungui shilingi milioni 500 ikijumuisha gharama za
matangazo kwenye radio,magazeti,televisheni,roadshows,mabango,vipeperushi n.k.
Matokeo yake yalikuwa ni vurugu katika baadhi ya viwanja, vurugu ambazo kama si
busara za TFF zingeweza kusababisha maafa.Mazungumzo yanaendelea kati ya TFF na
mzabuni CRDB ili kutafuta namna ya kuboresha utaratibu wa mfumo wa tiketi
za elektronik,lakini pia ni kuangalia ni kwa jinsi gani tiketi hizi hazigeuki
kuwa mzigo kwa mlaji maana licha ya watazamaji kulipia gharama ya tiketi
yenyewe lakini bado kuna asilimia inakatwa kama kamisheni ya uwakala jambo
ambalo pia ni mzigo kwa vilabu.TFF ina nia thabiti ya kutumia utaratibu huu,ni
mzuri iwapo utatekelezwa kwa taratibu stahili.
2. Ufinyu wa bajeti
TFF katika kutimiza majukumu yake
inahitaji pesa nyingi hasa kuendeleza mpira wa vijana, kukidhi gharama za
kuendesha ofisi, kuvipa nguvu vyama wanachama na kusimamia timu zake nane za
Taifa (Za wakubwa mbili wanawake/wanaume,U17 mbili,U20 mbili na za olimpiki
mbili).Eneo lenye ufadhili mkubwa ni timu ya Taifa ya wanaume tu.Hivyo ni
dhahiri mahitaji ya fedha TFF ni makubwa sana na vyanzo havikidhi.Jitihada
zinafanyika kuhakikisha tunaongeza vyanzo mbadala wa mapato.
3. Madeni
Madeni ambayo uongozi mpya
ulipoingia madarakani uliyakuta ni makubwa na yamelielemea shirikisho. Juhudi
za kuongea na wanaotudai ili aidha watupunguzie madai yao au tuyalipe kwa
masharti nafuu yanaendelea.Wale wote wanaotudai ambao wametuelewa katika hili
tunawashukuru sana. Kwa sasa kesi zote za madai dhidi ya TFF zilizokuwa
mahakamani zimeondolewa baada ya mapatano.
4. Nidhamu
Nidhamu bado ni tatizo si kwa
wachezaji bali hata kwa viongozi wetu.Yupo mchezaji amediriki kupigana na
walinzi wa raia na wengine wakadiriki kumpiga mwamuzi,hili halikubaliki na
hatua kali zitakuwa zinatolewa dhidi ya watovu wa nidhamu bila kujali wao ni
kina nani kwenye mpira wa nchi hii.
5. Maadili
Wizi mdogo mdogo hasa wa mapato ya
milangoni umeendelea.TFF tumekuta kesi za wizi wa aina hii zaidi ya hamsini
zilizoripotiwa polisi Chang’ombe na watuhumiwa hawakuwahi kupelekwa mahakamani
kwa kuwa mlalamikaji (TFF) hakujitokeza kuandika taarifa (statement). Uongozi
wangu umeamua utakuwa unafuatilia kwa karibu kesi hizi ili kukomesha tabia
iliyozoeleka ya udokozi.Pesa ya mpira itumike kwenye mpira.
6. Maamuzi uwanjani (Refeering)
Wapo waamuzi wanaokosea kwa makosa
ya kibanadamu, hao tunawaelewa.Lakini zinapotokea tetesi au tuhuma za haki
kutotendeka kiwanjani kwa sababu nyingine zaidi ya hii shirikisho linashtuka
sana na kamwe halitakubali lidhalilike kwa tuhuma kama hizi.Shirikisho kwa sasa
linafuatilia kwa karibu kinachoendelea uwanjani ili kuhakikisha haki inatendeka
kwa timu zote. Tayari mitihani imekwisha fanyika kupandisha madaraja waamuzi
mbali mbali ili kuongeza uwigo wa kupata waamuzi.Kozi za waamuzi zitaendelea
kutolewa ili kuzidi kunoa uwezo wao.
Aidha vituo vya kuendeleza waamuzi
vijana vya kambi ya Jenerali Twalipo na Alliance academy Mwanza viko mbioni
kuimarishwa ili viwe na nguvu zaidi ya kufundisha waamuzi vijana.
HITIMISHO
Ndugu
zangu nihitimishe kwa kutoa wito kwa wadau wote wa Mpira wa Miguu Tanzania
wakiongozwa na Serikali, CAF, FIFA, CECAFA, vyombo vya habari, Mashirika
ya Umma, Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Makampuni na watu binafsi wote kwa
pamoja tushikamane kwa pamoja tukiwa na nia moja tu, kuinua kiwango cha mpira
Tanzania na kuzifanya timu zetu za mpira ziwe za wakubwa, za wanawake na
za vijana ziwike, sio tu barani Afrika, bali duniani pote.
Kwa pamoja tunaweza.
Tukijaliwa tutakutana tena ndani ya
chumba hiki hiki baada ya siku 365 tangia nimechaguliwa kuongoza TFF ili
tufanye tathmini ya mwaka mmoja wa uongozi wangu.
Mungu ibariki TFF, Mungu
Ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika,"
Jamal Malinzi, Rais wa
TFF, 07 Januari, 2014.






No comments:
Post a Comment