Na Phinias
Bashaya-Mwananchi.
Pambano hili
linafanana na msemo wa panya waliosafiri katika boti la muhogo ambao kwa ujinga
wao walianza kutafuna kifaa walichopanda. Kilichofuata ni ukoo mzima wa kizazi
cha panya kuzama na kuangamia.
Vigogo hawa
wawili walikuwa na ndoto moja juu ya maendeleo ya mji wa Bukoba lakini baadaye
wakatofautiana katika utekelezaji wa miradi ya manispaa.
Balozi
Kagasheki alilalamika jukwaani akidai anaogopa kuumbuliwa na Dk Willbrod Slaa
siku akinusa ufisadi katika eneo lake.
Wote
walitumia madiwani na wapambe wengine kujenga makundi ya uhasama ili kuwasaidia
kusukuma ajenda zao.
Kabla ya
ripoti ya CAG, Kagasheki alionekana kama mwanasiasa mwoga anayetafuta huruma ya
wapigakura, kwa kutozoea ushindi usio na shaka.
Wapo
waliomwona Dk Amani kama mwanasiasa aliyeficha makucha yake na asiyeaminika,
ambaye yuko tayari kufa na tai shingoni akitetea anachokiamini hata kama kwa
kufanya hivyo kungewaumiza wengine
Makovu ya
mgogoro.
Bila kujali
ushindi alioupata Kagasheki baada ya CAG kuthibitisha madai yake dhidi ya meya
na hatimaye Dk Amani kujiuzulu, mgogoro wao umeacha athari kubwa za kiuchumi na
kijamii kwa wananchi wa Bukoba.
Hata hivyo,
Kagasheki ambaye inawezekana mvuto wake kwa wananchi umeongezeka, atalazimika
kujipa muda akisubiri kupima ‘Matokeo Makubwa Sasa’ ya ushindi wake kama
yatasomeka kwenye sanduku la kura.
Baada ya
mgomo wa madiwani kususia vikao kama njia ya kushinikiza kung’olewa kwa meya
wao, huduma muhimu za wananchi ambazo upatikanaji wake ulitegemea baraka za
Baraza la Madiwani ziliathirika kwa kiwango kikubwa.
Madiwani
waliona bora kususia vikao kuliko aibu ya kukaa na mtuhumiwa kujadili bajeti ya
kununua dawa kwa ajili ya wapiga kura wao wanaohitaji tiba katika vituo vya
Rwamishenye, Zamuzamu na Kashai.
Manispaa
haikuwa tena na watia saini wa kuhidhinisha malipo baada ya wale wa zamani muda
wao kumalizika. Hivyo isingeweza kuchukua fedha za kununua dawa kwa ajili ya
vituo vyake, achilia mbali huduma nyingine zilizokwama.
Kwa hali
ilivyokuwa, huwezi kupuuza uwezekano wa watoto kupoteza maisha baada ya
kudorora kwa huduma za afya kutokana na mgomo wa madiwani.
Wapo
wawekezaji waliojengewa hofu na kufuta mipango ya uwekezaji katika mji wa
Bukoba ambapo waombaji saba wamekwama kupata vibali vya ujenzi kwa zaidi ya
mwaka mmoja.
Kwa mujibu
wa Ofisa Maendeleo ya Jamii, Kitengo cha Vijana, Murshid Issa, mikopo kwa ajili
ya vijana imekwama kwa kuwa vikao vya madiwani vyenye mamlaka ya kujadili na
kupitisha suala hilo havifanyiki.
Mwenyekiti
wa mtaa wa Kalelabana, Imelda Kyaishozi anasema madiwani ambao ni wawakilishi
wa wananchi wamepoteza fursa muhimu ambayo ingetumika kuwainua vijana,
huku Respicius Muchunguzi kutoka Mtaa wa Kafuti akitaka yafanyike
maandamano kulaani ukatili huo dhidi ya vijana.
Katika
pambano hili ilikuwa ni lazima mshindi apatikane hata kwa gharama ya damu ya
wapiga kura.
Utawala
bora.
Kwa wagonjwa
waliokosa huduma na hata wengine kupoteza maisha, kwao madiwani sio lolote
zaidi ya malaika waliobadilika kuwa shetani.
Katika
mgogoro huo wananchi wa Kata ya Nyanga wamepoteza mradi wa maji kutoka
serikalini kwa ufadhili wa Benki ya Dunia baada ya diwani wao kutumia muda
mwingi katika malumbano kuliko kuhamaisha uchangiaji wa Sh6 milioni kama nguvu
ya jamii ili wapate mradi huo.
Taarifa ya
CAG iliwaumbua kwa kuweka wazi kuwa wananchi wa Kata ya Nyanga hawana haki ya
kulalamikia Kata ya Kagondo waliokamilisha sharti muhimu la mchango wa jamii na
kupewa mradi huo, bali wanatakiwa kujililia wenyewe.
Ni dharau na
kuwakejeli wananchi kuwaeleza kuwa Benki ya Dunia imefuta ufadhili wake wa
kiasi cha Sh18.5 bilioni kwa kuwa Manispaa ilishindwa kukamilisha kigezo muhimu
cha kuwapo mihtasari ya vikao vya Baraza la Madiwani.
Kwenye macho
ya wafadhili hali hiyo ilitafsili kutokuwapo kwa utawala bora kwenye Manispaa
ya Bukoba.
Kutokana na
hilo, barabara za manispaa zitaendelea kuwa na mahandaki na busara ya
madiwani iliwaonyesha eti bora kukosa kiasi hicho kuliko kikao kuendeshwa na
mtuhumiwa.
Kwa mujibu
wa CAG, Manispaa ya Bukoba kwa miaka miwili ya mgogoro imepoteza kiasi cha
zaidi ya Shilingi 250 milioni kutokana na kutokusanywa kwa ushuru sokoni,
ingawa mkaguzi mkuu huyo hakujua kuwa idadi kubwa ya madiwani wanamiliki
vibanda kinyemela katika soko hilo, hivyo wamenufaika wenyewe kwa kutokusanywa
ushuru huo.
Ufa
kwenye chama.
Kwa vyovyote
vile makundi yenye uhasama yanaendelea kuweka ufa na kutoaminiana kwenye chama
kuanzia ngazi ya wilaya hadi mkoa kutokana na ukweli kuwa ngazi hizo
zimeshiriki kutafuta suluhu bila mafanikio.
Hatua ya
Kamati Kuu ya CCM kutengua uamuzi wa kuwafukuza madiwani ‘waasi’ waliodaiwa
kuungwa mkono na Balozi Kagasheki unaongeza mashaka ya makundi hayo kuongea
lugha moja ya chama, baada ya kung’oka kwa Dk Amani.
Wanachama
waliokunywa maji ya bendera wanaamini kwamba pamoja na ukweli wa tuhuma za
Kagasheki dhidi ya Meya, bado mbunge huyo ameshiriki kukiumiza chama na ukweli
uko wazi kuwa amepoteza baadhi ya viongozi waliomuunga mkono.
Hawa
wanaamini chama chao hakina utaratibu wa kulalamika majukwaani kama vyama
vingine, bali kinatakiwa kupelekewa taarifa kupitia vikao halali na hatimaye
hatua kuchukuliwa kwa kuwa kinamiliki dola.
Hata hivyo,
kundi jingine linamuona Kagasheki kama nguzo ya chama ambaye yuko tayari
kutofautiana na kiongozi yeyote hata kama hatua hiyo itamgharimu.
Hii ndiyo
sababu ya kuwatuhumu hadharani viongozi wenzake majukwaani bila kujali matokeo
yake.
Vilevile
baada ya kumdhoofisha Dk Amani kupitia taarifa ya CAG, hata kama hakuwahi
kutangaza kukitamani kiti cha ubunge, Kagasheki anaweza kupata mpinzani mpya
atakayetishia nafasi yake ya ubunge kwa kutegemea kuungwa mkono na wapambe wa
Dk Amani.
Pengine
mtihani mkubwa kwa CCM ni jinsi ya kuwashawishi wapigakura wa Bukoba hadi ipate
sababu ya kuaminika.
Kutokana na
mgogoro huu kuna uwezekano mkubwa wa ahadi walizotoa kutokamilika kabla ya
uchaguzi mkuu.
Wakati wa
uchaguzi mkuu hakuna mwananchi atakayehangaika kujikumbusha jinsi Mkaguzi Mkuu
na Serikali walivyoshughulikia watuhumiwa wa ubadhilifu wa miradi bali watahoji
hesabu ya yale waliyohaidi kutekeleza.
Kwa jinsi taswira ya Baraza la Madiwani ilivyo hakutakuwa na mawazo mapya yatakayoibuliwa, na idadi kubwa ya madiwani hawana la kupoteza kutokana na ukweli kuwa wengi wao hata kwa kukosea hawawezi kuchukua fomu ya kutetea nafasi zao.
No comments:
Post a Comment