Ripoti mpya
ya utafiti imebainisha kuwa mishahara mikubwa wanayolipwa viongozi wa juu
serikalini na wanasiasa hailingani na utendaji wao wa kazi.
Ripoti hiyo
iliyozinduliwa jana jijini Dar es Salaam, imeeleza kuwa viongozi hao wanalipwa
mishahara inayotofautiana kwa kiwango kikubwa na pato la mwananchi wa kawaida.
Huku ikitaja
mapato ya mishahara ya marais wa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki ikiwamo Tanzania,
imesema kuwa hali hiyo ni kuibebesha jamii mzigo wa kugharimia malipo ya
viongozi.
Akizindua
ripoti hiyo iliyochunguza gharama za kuwalipa viongozi wa Serikali na
wanasiasa, Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti kuhusu Kuondoa Umaskini (Repoa),
Dk Theodore Valentine, alisema kuwa viongozi wa Afrika Mashariki ndio
wanaoongoza kwa kulipwa mishahara mikubwa zaidi chini ya Jangwa la Sahara.
"Kama
viongozi wakuu watakuwa wanalipwa mishahara mikubwa, nchi za Kusini mwa Jangwa
la Sahara zitaweza kugharimia demokrasia?" alihoji Valentine.
Utafiti huo
uliofanyika kati ya mwaka 2009 na 2012, umebainisha kuwa Rais wa Tanzania
analipwa mshahara dola 172,014 kwa mwaka (Sh275 milioni) sawa na Sh22.9 milioni
kwa mwezi, huku Rais wa Kenya, akiongoza kwa kulipwa dola 515,021 kwa mwaka
(Sh824 milioni) kwa mwaka sawa na Sh68.6 milioni kwa mwezi.
Rais wa Rwanda
analipwa dola 199,000 kwa mwaka (Sh124 milioni) sawa na Sh10 milioni kwa mwezi,
wakati rais wa Nigeria akipokea dola 161,902 (Sh259 milioni) ambazo ni sawa na
Sh21 milioni kwa mwezi.
Pia umeeleza
kuwa Rais wa Kenya analipwa mara 320 zaidi ya pato la mwananchi wa kawaida wa
nchi hiyo, wakati rais wa Afrika Kusini anapata mara 46 na Rwanda mara 150
zaidi ya mwananchi wa kawaida.
Ripoti hiyo
imeendelea kubainisha kuwa rais wa Tanzania analipwa mara 8.2 ya mshahara wa
hakimu, huku rais wa Kenya akipokea mara 13.1 na kumpita rais wa Rwanda anayechukua
mara 12 zaidi ya mshahara wa hakimu.
Kwa upande
wa wabunge, utafiti huo umeeleza kuwa wabunge wa Tanzania wanalipwa mara 3.0 ya
mshahara anaolipwa hakimu, Kenya (5.5) na Rwanda (3.0).
Viwango hivyo vimetajwa
kuwa vikubwa kuliko vya wabunge wa Nigeria na Afrika Kusini.
Naibu Spika
anena
Naye Naibu
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai alisema kuwa umefika wakati ambapo
mishahara ya viongozi wa umma inabidi iwekwe wazi kwa wananchi.
"Ningependa
mishahara ifahamike kama ilivyo kwa nchi nyingine, hii itaondoa uongo kwa
wabunge," alisema.
Alisema
mishahara wanayolipwa wabunge siyo mikubwa na kwamba inapaswa kuongezwa zaidi
kwa kuwa hivi sasa imetofautiana kidogo na ya wakuu wa wilaya.
"Mshahara
wangu mimi kama Naibu Spika ni mdogo..., hata wa Waziri Mkuu siyo mkubwa. Siku
zote mtu anapoongezewa mshahara inamwongezea motisha ya kufanya kazi,"
alisema Ndugai.
Serikali
yajibu.
Naibu Waziri
wa Kazi na Ajira, Dk Makongoro Mahanga, alisema viongozi wanalipwa mshahara
kutokana na nyadhifa walizonazo, hivyo haoni sababu ya jambo hilo kujadiliwa.
Alisema
mshahara ni siri ya mfanyakazi husika, na kwamba iwapo itawekwa wazi baadhi ya
watu wataacha kujadili mambo ya maendeleo na badala yake wataanza kuzungumzia
malipo hayo.
"Tujadili
kuhusu namna ambavyo gesi itatuletea maendeleo kwenye uchumi wa nchi yetu na
siyo mishahara," alisema.
Alipopigiwa
simu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi), Hawa Ghasia, alihoji kuwa anazungumza na nani, mwandishi
alipojitambulisha alitaka apewe muda hadi baadaye kwa madai kuwa hakuwa sehemu
nzuri.
Rais Kikwete
na OGP.
Akinukuliwa
na gazeti la Serikali, Rais Jakaya Kikwete, ambaye Oktoba 31 hadi Novemba Mosi
2013, alihudhuria Mpango wa Pamoja wa Uendeshaji wa Serikali kwa Uwazi (OGP)
uliofanyika London, Uingereza, ambapo alizungumzia uwazi kwenye Serikali yake
likiwemo suala la mishahara.
Mkutano huo
ulihudhuriwa na washiriki 1,000 kutoka nchi 60 wanachama na Rais Kikwete
alipata nafasi ya kuuelezea mkutano huo, namna Tanzania ilivyoanza utekelezaji
wa masharti ya mpango huo.
Rais Kikwete
alisema kuwa mshahara wa mtumishi wa umma hauwezi kuwa siri na ndiyo maana
unawekwa katika bajeti ya serikali.
"Mishahara
haiwezi kuwa siri. Si ipo kwenye bajeti za Serikali?" Alijibu Rais Kikwete
alipoulizwa kama suala la mishahara litaendelea kuwa siri katika utekelezaji wa
mpango huo.
Rais Kikwete
alisema: "Changamoto iliyopo ni kwamba mpango huu unabadili mazoea yetu ya
kufanya kazi. Sisi katika kila Serikali kila kitu kilikuwa siri. Sasa OGP
inataka mambo haya yawe wazi, ifike hatua mtu aone kutoa habari ni
wajibu."
TUCTA yatoa
kauli.
Katibu Mkuu
wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Nicolas Mgaya alisema wabunge
wanalipwa mishahara mikubwa lakini baadhi yao hawaonekani kwenye vikao.
Alitaka
mishahara yao iwekwe wazi kwa wananchi kwa kile alichokieleza kuwa kwa sababu
wanalipwa kwa kutumia kodi za wananchi.
Anavyosema
Profesa Wangwe.
Akizungumzia
matokeo ya utafiti huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa, Profesa Samuel Wangwe
alisema kuna haja ya kuangalia gharama za kuwalipia viongozi.
"Tuangalie
gharama ya demokrasia, lakini jambo la msingi ni kuwa kama wabunge wanalipwa
kiasi kinachotajwa basi wafanye kazi yao wanayostahili na wasisahau kwamba
wanawawakilisha wananchi ambao ni maskini," alisema.
Profesa
Lipumba.
Kwa upande
wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi - CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye
ni mchumi kitaaluma alisema kuwa hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa viongozi
wakilipwa mishahara mikubwa wanafanya kazi zaidi.
"Hakuna
ushahidi wowote kwamba kwa kuwalipa wabunge mishahara mikubwa basi wanafanya
kazi vizuri zaidi," alisema.
Akitolea
mfano wabunge wa Kenya alisema: "Katika kipindi cha miaka mitano mbunge wa
Kenya analipwa dola za Marekani dola 1milioni (sawa wa Sh1.6 bilioni) kiasi ambacho
ni sawa na Sh26 milioni kwa mwezi."
Aliongeza
kuwa mishahara ya wabunge wa Tanzania ni zaidi ya mara 40 ya pato la kawaida la
mwananchi.
Alipendekeza
kuanzishwa kwa taasisi ambayo itapewa jukumu la kusimamia mapato ya viongozi wa
umma, na kwamba ni vyema katiba izungumze kuwa mishahara na marupurupu ya
wabunge itapangwa na taasisi ambayo ipo huru itakayozingatia mapato ya nchi
yalivyo.
Chanzo:Mwananchi






No comments:
Post a Comment