![]() |
Kiongozi wa
kijeshi wa kundi la M23, Sultani Makenga
REUTERS/James
Akena.
|
Duru sahihi
kutoka katika jeshi la Uganda zimearifu kwamba Makenga amejisalimisha akiwa na
wapiganaji zaidi ya 1500 katika eneo la mpaka wa DRC na Uganda.
Msemaji wa
jeshi la serikali ya Uganda Paddy Ankunda hapo awali alifahamisha kuwa
wapiganaji 1500 wa kundi la M23 wamejisalimisha mikononi mwa jeshi lao pamoja
na Sultani Makenga, ingawa hakusema lolote juu ya hatma ya kamanda huyo.
Kujisalimisha
kwa wapiganaji hao kunakuja wakati huu ambapo Umoja wa Mataifa UN umeahidi
kuendelea kuisaidia serikali ya DRC kuimarisha usalama wa mipaka yake baada ya
kufanikiwa kusambaratisha ngome zote za waasi wa M23 mashariki mwa nchi hiyo.
Mkuu wa
vikosi vya Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO, Martin Kobler amethibitisha
vikosi vyao vitaendelea kuweka kambi karibu na mpaka ili kudhibiti upitishwaji
wa silaha na kukabiliana na wapiganaji wa Kihutu wa FDLR wanaingia nchini
Rwanda.
Majeshi ya
serikali ya DRCongo yakiungwa mkono na brigedi maalumu ya UN juma hili
yalifanikiwa kuwazidi nguvu waasi wa M23 ambao walianza harakati zao mwanzoni
mwa mwaka 2012.
Wakati hayo
yakijiri serikali ya Jamhuri ya Kinshasa imesema kuwa itatia saini azimio la
amani na kundi la waasi wa M23 na si mkataba wa kusitisha vita dhidi ya kundi
hilo iwapo litaendelea na uasi mashariki mwa nchi hiyo.
Kauli hiyo
imetolewa na msemaji wa serikali, Lambert Mende ambaye amesisitiza kuwa azimio
litakalotiwa saini ni la kusitisha vita kwa muda.
Kwa upande
wao kundi la waasi wa M23 kupitia kwa mpatanishi wake kwenye mazungumzo ya
kampala, Roger Lumbala anasema kuwa kwa sasa kundi lao litageuzwa na kuwa chama
cha siasa na kwamba serikali lazima itekeleze maazimio ya jumuiya ya kimataifa.
Naye
mwakilishi maalumu wa UN, Mary Robinson ameliambia Baraza la Usalama la Umoja
wa Mataifa UNSC kuwa ushindi dhidi ya M23 ni muhimu katika wakati huu ambapo
jitihada za kutokomeza uasi mashariki mwa DRC zikizendelea.
Chonzo:-rfi.






No comments:
Post a Comment