Padre
Anselmo Mwang'amba wa kanisa katoliki visiwani Zanzibar nchini Tanzania
amemwagiwa tindikali na watu wasiofahamika akiwa katika eneo la Ngome Kongwe
siku ya ijumaa. Kwa mujibu wa mashuhuda ni kuwa Padre huyo wa Parokia ya Machui
alitokea kwenye internet cafe moja mjini hapo na dakika chache alirejea huku
akipiga yowe kwa lengo la kuomba msaada.
Rukia
Abbasi ambaye ni mmoja wa wafanyakazi wa cafe hiyo amesema walimpatia Padre
huyo huduma ya kwanza kwa kumwagia maji na kisha kumkimbiza hospitali kwa ajili
ya kupatiwa matibabu.
Madaktari
wamesema wanaendelea kumtibu majeraha aliyopata maeneo ya usoni, kifuani na
mikononi na endapo hakutakuwa na mabadiliko chanya basi watamsafirisha kwa
matibabu zaidi.
Akizungumza
na Idhaa ya Kiswahili ya Radio France International, Afisa Habari Mkuu wa Jeshi
la Polisi visiwani humo Inspekta Mohammed Mhina amesema wanaendelea kuchunguza
ili kuwabaini waliohusika na tukio hilo na kuwaomba wananchi kushirikiana nao
katika kuwasaka wahalifu hao.
Hili
sio shambulio la kwanza kwa viongozi wa dini visiwani humo, mwezi Februari
mwaka huu Padre Evarist Mushi alipigwa risasi na kuuawa na watu wasiofahamika,
wakati mwezi desemba mwaka jana Padri Ambrose Mkenda alinusurika kifo baada ya
kupigwa risasi na kujeruhiwa vibaya wakati akitoka kanisani kuhudhuria misa.
Aidha
kiongozi wa dini ya kiislamu, Msaidizi wa Mufti wa Zanzibar Shekh Fadhil
Suleiman Soraga alimwagiwa tindikali mwezi Novemba mwaka jana na Sheha wa
Shehia ya Tomondo Wilaya ya Magharibi Unguja Mohammed Omar Said alimwagiwa
tindikali mwezi Mei mwaka huu.
Tukio
la karibuni ni lile la wasichana wawili raia wa Uingereza waliokuwa wafanyakazi
wa kujitolea visiwani humo kuvamiwa na kumwagiwa tindikali, mpaka hivi sasa
watuhumiwa wa tukio hilo bado hawajatiwa nguvuni licha ya kutangazwa donge nono
la euro 4500 kwa yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwao.
Serikali
ya Tanzania imekuwa ikilaani vitendo hivyo ambavyo vinatia doa Taifa hilo la
Mashariki mwa Afrika.





No comments:
Post a Comment