![]() |
Jeneza lenye mwili wa Albert Mangweha
likishushwa kaburini.
|
Aidha Mazishi
ya msanii huyo maarufu wa muziki wa kizazi kipya, Albert
Mangwair, yaliyofanyika makaburi ya Kihonda-Kanisani, jana(Juni 06,2013)
yaliutikisa mji wa Morogoro mbele ya Mkuu wa Mkoa huo, Joel Bendera.
Shughuli
hiyo ilitanguliwa na kuaga mwili na ilifanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri
kutokana na wingi wa maelfu ya watu.
Wingi wa
watu ndio uliifanya Kamati ya Mazishi chini ya Adam Juma, ihamishie hafla hiyo
Uwanja wa Jamhuri badala ya nyumbani kwa usalama zaidi.
Mji wa
Morogoro ulianza kuzizima tangu asubuhi, baada ya kushuhudia vikundi vya watu
wengi vikielekea Jamhuri wakiwa kwa miguu, pikipiki, baiskeli na wengine kwenye
magari vikienda na kurudi.
Wasanii na
viongozi mbalimbali, akiwamo Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, nao
walikuwapo kwenye tukio la kuaga mwili wa Ngwair na baadaye kwenye mazishi yake
ambayo yalizua mkanyagano wa aina yake.
Idadi kubwa
ya watu ilijitokeza katika shughuli ya kumuaga marehemu, ambapo pia ilikimbilia
makaburini kwa ajili ya kushuhudia mwili wake ukiingia kaburini.
Awali, Mkuu
wa Mkoa Morogoro, Joel Bendera, alifika nyumbani kwa mama wa marehemu saa nne
za asubuhi na kupata fursa ya kuwapa pole wafiwa.
Akizungumza
na wanafamilia na baadaye Uwanja wa Jamhuri, Bendera alisema Tanzania imepoteza
msanii nyota na mwenye bahati ya kupendwa na watu wengi.
“Hii ni
hatari kubwa maana Ngwair ameonyesha ni kiasi gani alikuwa nyota katika tasnia
ya muziki wa Hip Hop kwa umahiri wake, sambamba na kuishi na watu vizuri.
“Hii leo ni
historia katika mkoa wa Morogoro, hususan kwa kushuhudia watu wengi wakiwa na
huzuni katika kumuaga msanii wao mpendwa kwa namna moja au nyingine, hivyo serikali
itaendelea kufanyia kazi changamoto zinazowakabili vijana hawa,” alisema
Bendera.
Naye Mbunge
wa Mbeya Mjini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, alisema wasanii wamechoka kuishi kimaskini wakati watu
wengi wanaheshimu kazi zao.
“Inaumiza
kuona tunazikwa kwa mtindo huu wakati maisha yetu ni magumu mno, hivyo hatuwezi
kuona hali hii inaendelea kuota mizizi, hivyo wasanii tuendelee kuwa makini
katika hili.
“Matatizo
yaliyompata Ngwair katika maisha yake ni sehemu ya changamoto zilizopo katika
tasnia hii ya muziki wa kizazi kipya, ingawa tukifa mazishi yetu yanakuwa ya
heshima mno,” alisema.
Pamoja na
kukusanya watu wengi, watu wengi walionekana kwenda uwanjani kuwaona wasanii
wengine, hivyo kusababisha mkanyagano kila anapoingia au kutoka msanii nyota.
Hata hivyo,
matatizo yalianza kujitokeza wakati wa kuaga mwili kutokana na askari kushindwa
kukabiliana na wingi wa watu katika kuwadhibiti.
M 2 The P. |
Wakati wa
shughuli ya kuaga, ghafla, rafiki wa Ngwair, aliyopata matatizo naye Afrika
Kusini, Mgaza Pembe, M 2 The P, aliletwa uwanjani hapo kumuaga Ngwair.
Barabara
zilizopitiwa na msafara wa mwili wa Ngwair, zilikuwa zimejaa watu wakiwa na nia
ya kumungalia nyota wao akielekea nyumba yake ya milele baada ya kufariki
Afrika Kusini, Jumanne ya wiki iliyopita.
Kufika
makaburini, umati mkubwa wa watu ulikuwapo, hivyo ndugu wa marehemu kukosa muda
wa kutia mchanga katika kaburi, hasa pale watu waliposhindwa kusogea.
Kaka wa
marehemu, Kenneth Mangwea, aliwashukuru Watanzania kwa moyo wao wa upendo kiasi
cha kushirikiana na wao kuhakikisha kuwa mwili wa Ngwair unazikwa Tanzania.
“Nashukuru
sana, natumia muda huu kuwatakia upendo zaidi na zaidi Watanzania wenzetu,
sambamba na kumtakia mapumziko mema huko mbinguni Ngwair,” alisema Kenneth.
Mwili wa
Mangwair ulizikwa majira ya saa tisa za mchana, ikiwa ni siku moja tangu aagwe
kwenye Viwanja vya Leaders, jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment