UFAFANUZI
WA TAARIFA MBALIMBALI ZILIZOTOLEWA
KWENYE VYOMBO VYA HABARI DHIDI YA DAWA BANDIA YA KUPUNGUZA MAKALI YA UKIMWI YENYE JINA LA
BIASHARA TT-VIR 30 TOLEO NAMBA 0C.01.85.
Tarehe
9 Mei, 2013, Mhe. Dkt. Hussein A. Mwinyi (Mb) Waziri wa Afya na Ustawi wa
Jamii, katika kuhitimisha hoja ya bajeti
ya Wizara alitolea ufafanuzi suala la dawa bandia ya ARV kufuatia hoja zilizokuwa imetolewa na Mhe. Zarina S. Madabida (Mb)
kuhusu kuhusika kwa kiwanda cha dawa cha
Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd (TPI) katika sakata la dawa bandia ya
ARV.
Baada
ya ufafanuzi huo wa Mhe. Waziri kutolewa, kumekuwa na taarifa mbalimbali kupitia vyombo vya habari zinazoleta
mkanganyiko kwa wananchi kuhusu suala
hili.
Ili kuondoa mkanganyiko ambao umeanza kujitokeza,
Wizara inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu
tamko lililotolewa na Mhe. Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii.
Aidha,
kama ilivyoelezwa katika taarifa mbalimbali za umma zilizokwisha kutolewa na
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na TFDA kuhusiana na suala hili,bado inasisitizwa
kwamba kampuni ya TPI Ltd iliiuzia Bohari
ya Dawa (MSD) dawa bandia aina ya TT-VIR 30 toleo Na. 0C.01.85, kwa
mujibu wa nyaraka zilizopo.
Tunapenda
kusisitiza kwamba, Mhe. Waziri katika hotuba yake hakukanusha kuwa kampuni
ya TPI Ltd iliiuzia MSD dawa bandia bali
alieleza kwamba uchunguzi wa awali katika
kiwanda cha kampuni hiyo haukuonesha dawa hiyo ilizalishwa na TPI
Ltd bali vifungashio ni vya TPI Ltd na
nyaraka zinaonesha TPI Ltd kuiuzia MSD
dawa hizo bandia.
Aidha,
alieleza kuwa vyombo vya usalama bado
vinaendelea kulichunguza suala hilo ili kubaini chanzo na wahusika wakuu wa
dawa hizo bandia.
Kwa
kuzingatia unyeti wa suala hili, Wizara inatoa wito kwa vyombo vya habari
kusubiri hatma ya uchunguzi unaofanywa na vyombo vya usalama na kuepuka kutoa taarifa ambazo zinaweza kupotosha umma
na jitihada kubwa za Serikali katika
kupambana na dawa bandia nchini.
N. Mwamwaja
MSEMAJI
16
Mei, 2013.
No comments:
Post a Comment