Shirikisho
la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limelitaka Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) kuanza upya mchakato wa uchaguzi baada ya kubaini kasoro
iliyotokana na ukosefu wa kutokuwepo vyombo vya kushughulikia ukiukwaji wa
maadili.
FIFA ambayo
ilituma ujumbe wake katikati ya mwezi uliopita kufanya utafiti kuhusu mchakato
wa Uchaguzi Mkuu wa TFF ambao ulisimamishwa baada ya baadhi ya wagombea
kulalamika, imetaka uchaguzi ufanyike kabla ya tarehe 30 Oktoba 2013, lakini
ukitanguliwa na mabadiliko ya katiba ambayo yatahusisha uundwaji wa vyombo vya
kushughulikia ukiukwaji wa maadili.
Raiswa TFF,
Leodegar Tenga aliwaambia waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano wa
shirikisho hilo kuwa suala la Tanzania lilijadiliwa kwenye kikao cha Kamati ya
Dharura ya FIFA kilichofanyika tarehe 28 Aprili 2013 na maamuzi yake kutumwa
juzi kwa barua iliyosainiwa na KatibuMkuuwa FIFA, Jerome Valcke.
Baada ya
kupokea barua hiyo, Rais wa TFF alifunga safari kwenda Dodoma jana kukutana na
Mheshimiwa Waziri na Naibu wake pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la
Taifa (BMT).
“Matarajio
yetu sote yalikuwa kupokea majina ya waliopitishwa ili tufanye uchaguzi.
Kinyume chake tumepokea maagizo hayo.Hata hivyo tumeona kuwa hili ni jambo la
kheri kwa vile siyo tu haki itatendeka bali pia itaonekana imetendeka.” alisema
Tenga, ambaye alishatangaza kuwa hatagombea tena urais baada ya kuliongoza
Shirikisho kwa vipindi viwili vya miaka minne kila kimoja.
“Lengo letu
ni kuhakikisha maagizo hayo yanatekelezwa na uchaguzi kufanyika mapema iwezekanvyo
kabla ya tarehe iliyotolewa. Yale mambo nayoweza kufanyika kwa pamoja
yatafanyika ili tuharakishe utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na FIFA.”
Uchaguzi wa
TFF ulipangwa kufanyik tarehe 23 na 24 Februari 2013 na ulikuwa ukielekea
ukingoni, lakini baadhi ya wagombea walienguliwa katika hatua ya mwisho na
Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF na ndipo walipo andika barua FIFA kuomba
iingilie kati.
Rais Tenga
alisema kuwa ujumbe wa FIFA ulikutana na pande zote zilizoathiriwa na mchakato
wa uchaguzi na kwamba baada ya kukusanya taarifa hizo, maagizohayo ya FIFA sasa
yatakuwa ni suluhisho la matatizo ya muda mrefu katika uendeshaji wa mpira wa
miguu nchini.
Katika barua
hiyo, FIFA imeiagizaTFF:
1. Kuunda vyombo sahihi (Kamati ya Maadili
itakayokuwa na vyombo viwili ambavyo ni cha kutoa maamuzi ya awali na cha
rufaa) ambavyo mamlaka yake yatakuwa ni kushughulikia masuala ya ukiukwaji wa
maadili.
2. Kufanya mabadiliko ya katiba kwa kuzingatia
uundwaji wa vyombo hivyo.
3. Kuanza upya kwa mchakato wa uchaguzi wa
Kamati ya Utendaji kwa kufungua milango kwa wagombea ambao walishachukua fomu
na wagombea wapya.
4. Shughuli hiyo ikamilike ifikapo tarehe 30
Oktoba 2013.
Katika
kutekeleza hayo, TFF inatakiwa iitishe Mkutano Mkuu wa Dharura kwa ajili ya
kufanya mabadiliko ya Katiba kwa ajili ya kuunda kamati hizo za maadili na
Kanuni za Uchaguzi kabla ya kuendelea na Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Kamati
Mpya ya Utendaji.
Katika maoni
yake FIFA imeeleza kuwa katika mchakato, Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliwaengua
au kupitisha baadhi ya wagombea kwa kubaini kuwa walikiuka Ibara ya 9 (7) ya
Kanuni za Uchaguzi na pia Ibaray a 29 (7) ya Katiba ya TFF ambavyo vinahusisha
suala la kufungua kesi mahakamani, kufuja fedha za shirikisho na ukosefu wa
uwajibikaji wa pamoja.
Hata hivyo,
FIFA ilisema kuwa watu hao walitakiwa waadhibiwe kwanza na kamati husika
(kamati za maadili) kabla ya kuenguliwa na kamati za uchaguzi za TFF.
“Kutokana na
ukosefu wa kamati za maadili matokeo yake, mmoja wa wagombea amekuwa
akienguliwa kwenye uchaguzi kila anapombea bila ya kujua adhabu yake ni ya muda
gani,” inasema barua hiyo ya FIFA.
Rais Tenga
ameagiza kuitishwa kwa kikao cha dharura cha Kamati ya Utendaji ya TFF kupokea
maagizo ya FIFA na kupanga ratiba ya utekelezaji wake kwa lengo la kuhakikisha
kuwa mchakato huu unatekelezwa mapema iwezekanavyo.
Boniface
Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment