Waganga Mkoani KAGERA watakiwa kuzingatia usafi wa vifaa wanavyovitumia katika kutoa tiba kwa Wananchi . - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Wednesday, April 17, 2013

Waganga Mkoani KAGERA watakiwa kuzingatia usafi wa vifaa wanavyovitumia katika kutoa tiba kwa Wananchi .



Waganga na wakunga wa tiba asilia katika Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, wametakiwa kuzingatia usafi wa vifaa wanavyovitumia katika kutoa tiba kwa wananchi, ili kuepuka kueneza magonjwa kutokana na uchafu wa vifaa hivyo.




Mkuu wa wilaya ya Bukoba mkoani Kagera Bw.Zipporah Pangani  ametoa wito huo wakati wa mkutano wa kukabidhi vyeti vya Serikali kwa waganga 13, ambavyo vinawaruhusu kufanya kazi ya kutoa tiba kwa jamii kisheria,katika katika Uwanja wa Uhuru mjini Bukoba. 




Amesema waganga hao wasipozingatia usafi wa vifaa vyao  wanaweza kusababisha kuenea kwa magonjwa kama Ukimwi na kuharisha. 




Bw. Pangani  amewataka waganga kuongeza  ujuzi na kuboresha shughuli zao kwa kutumia dawa hizo kutengeneza vidonge na kuitaka jamii kutambua kazi zinazofanywa na waganga hao, maana zipo kwa mujibu wa sheria namba 23 ya mwaka 2002.




Naye  Mwenyekiti wa Chama cha Waganga na Wakunga wa Tiba Asilia (STAMATA) Manispaa ya Bukoba,Bw. Habibu Mahyoro  amesema watu wanaoishi kwa kutegemea viungo vya binadamu si waganga  bali ni matapeli na ni wachawi. 




Ameiomba Serikali kuwawezesha kupata vitendea kazi, ikiwamo vyombo vya usafiri ambavyo vitatumika kutoa elimu kwa jamii kwa lengo la kupunguza matukio ya wanaojihusisha na matendo maovu ikiwamo mauaji ya albino na vikongwe. 



Awali akisoma risala kwa mgeni rasmi Katibu wa kamati ya maandalizi, Bi.Veidiana Lukeisa  amesema waganga wana umuhimu mkubwa, kwani yapo baadhi ya magonjwa ndani ya jamii ambayo hutibiwa na dawa za asili pekee. 




Ameiomba Serikali kuwashirikisha ili kukabiliana na changamoto mbalimbali  ikiwamo kupambana na magonjwa kama malaria na Ukimwi  kwa kutumia tiba asilia na kutoa ushauri. 




Pia ameiomba Serikali kuweka utaratibu utakaosaidia hospitali kuwapokea wagonjwa kutoka kwa waganga na wakunga wa tiba asilia, ili kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika.




Aidha  STAMATA mkoani Kagera  ilianzishwa mwaka 2011 ikiwa na wanachama 47  ambapo  mpaka sasa ina wanachama 89 kutoka wilaya za Misenyi na  Bukoba.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad