Serikali kujenga soko la mazao katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Kigoma ili kurahisisha uuzaji na ununuzi wa mazao ya wakulima. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Tuesday, April 23, 2013

Serikali kujenga soko la mazao katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Kigoma ili kurahisisha uuzaji na ununuzi wa mazao ya wakulima.


Kigoma
Serikali  inatarajia kujenga soko la mazao katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Kigoma ili kurahisisha uuzaji na ununuzi wa mazao ya wakulima wilayani humo.



Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima, alibainisha hayo bungeni jana(April 22,2013) alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kasulu Vijijini, Agripina Buyogera, aliyetaka kujua ni lini serikali itajenga soko la uhakika kwa ajili ya wakulima wa Kasulu.




Waziri Malima alisema hatua iliyofikiwa na serikali katika kujenga soko hilo ni halmashauri kusaini Mkataba wa Maelewano (MoU) na Benki ya Rasilimali (TIB) Mei mwaka 2012 ambayo imekubali kuchangia asilimia 80 ya gharama za ujenzi huku Kasulu itachangia asilimia 20.




Kwa mujibu wa naibu waziri huyo, soko kuu la mazao wilayani humo linatarajiwa kujengwa kwenye eneo lililopo katikati ya vijiji vya Mgombe na Nyachenda.




Kuhusu kuondoa migogoro ya ardhi hususan katika eneo litakalojengwa soko hilo, serikali wilayani Kasulu imekamilisha uwekezaji wa maeneo hayo kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji hivyo kabla ya ujenzi huo kuanza.




Pia Malima alitolea ufafanuzi kuhusu tuhuma za baadhi ya watendaji kutokuwa waaminifu katika ukusanyaji wa ushuru ambapo alisema wizara kwa kushirikiana na idara na taasisi, itafanya jitihada zote kupambana nao.




Alikiri kuwa watendaji hao wamekuwa wakiwatoza ushuru wakulima mara mbili kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kuuza mazao yao bila ya kudai au kupewa stakabadhi za malipo au kulipa ushuru sehemu ndogo ya mazao hivyo kulipishwa mara mbili.




Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu inatoza ushuru kwa kuzingatia Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Na. 9, kifungu cha 7(1) (g) ya mwaka 1982 ambayo ushuru unaotozwa ni kati ya asilimia 3 na 5 ya bei ya shambani,” alisema.




Chanzo:Tanzania Daima.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad