Wataalamu na wachambuzi wa masuala ya kijinsi wameasa matokeo ya sensa ya
watu na makazi yanayoonesha idadi ya wanawake ni kubwa kuliko wanaume
yasitafsiriwe kwa mtazamo wa kwamba suluhu ni wanaume kuoa wake wengi.
Matokeo yaliyotangazwa na Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka
2012, Amina Mrisho yanaonesha wastani wa uwiano wa idadi ya watu kijinsi
Tanzania Bara, ni wanaume 95 kwa kila wanawake 100.
Zanzibar ni wanaume 94 kwa kila wanawake 100 huku mikoa mingi uwiano
ukiwa kati ya wanaume 92 na 95.
Mkoa wa Manyara ndio pekee una wanaume wengi kuliko wanawake kwa uwiano
wa wanaume 101 kwa kila wanawake 100 huku Mkoa wa Njombe, ukiwa na wanawake
wengi zaidi kwa uwiano wa wanaume 88 kwa kila wanawake 100.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wachambuzi wanasema dhana kwamba
wanawake wanazaliwa wengi kuliko wanaume ni dhaifu badala yake, takwimu hizo
zichambuliwe kitaalamu kuwezesha mipango sahihi ya kisera na kiuchumi kwenye
kipengere hicho.
Wamesema tafsiri yake lazima izingatie sababu mbalimbali zikiwemo za
kibaiolojia na shughuli za mwanamume ili watunga sera na wanaotoa uamuzi katika
masuala ya maendeleo kuja na suluhu sahihi.
“Unaweza ukachukulia mzaha kwamba wanawake ndiyo wanapaswa kusaidiwa kwa
kuwaoa lakini kumbe wanaume wakawa ndiyo wanaohitaji kusaidiwa kwa kukabili
mambo yanayochangia idadi yao kuwa ndogo,” alisema mwanaharakati wa masuala ya
jinsia, Remmy Magesa.
Meneja wa Idara ya Takwimu za Jamii, Vifo, Uzazi na Maradhi ya Ofisi ya
Taifa ya Takwimu (NBS), Aldegunda Komba alisema kibaiolojia, uwezo wa wanaume
kuishi wanapofikia utu uzima, ni mdogo kuliko wa wanawake.
Katika mafunzo yaliyoandaliwa na NBS kwa waandishi wa habari kuwaelimisha
juu ya uandishi wa habari za matokeo ya sensa, Komba sanjari na Mratibu wa
Sensa, Irenius Ruyobya, walikiri kuwepo watu wanaochukulia wingi wa wanawake
kuwa ni tatizo ambalo suluhisho lake linapaswa kuwa ndoa za wake wengi.
Wataalamu hao walifafanua kwamba idadi ya wanawake kuzidi wanaume ni
suala la kidunia siyo tu kwa Tanzania. Licha ya sababu za kibaiolojia, pia
wingi wa majukumu ya kifamilia na kimaisha yakiwemo majanga, vinatajwa kuwa
chanzo cha kupungua umri wa kuishi wa wanaume.
Akizungumza na mwandishi mwishoni wa wiki baada ya matokeo hayo
kuzinduliwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, pia alisisitiza mantiki ya takwimu hizo akisema
haimaanishi kwamba idadi ya wanawake wanaozaliwa ni wachache.
“Hapa haina maana wanawake ndiyo tunazaliwa wengi, sote tunazaliwa sawa…
Wanaume wengi hufariki wakifikia utu uzima kuliko wanawake,” alisema Profesa
Tibaijuka.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba katika
kuzungumzia wanawake kuwa wengi kuliko wanaume, alisema inatoa changamoto kwa
Serikali kutoa nafasi sawa kwa jinsi zote.
Chuo Kikuu cha Liverpool John Moores cha Uingereza, kiliwahi kutoa
matokeo ya utafiti uliofanywa na jopo la wanasayansi yaliyoonesha kwamba
wanawake wana uwezo wa kuishi miaka mingi zaidi ya wanaume.
Ilibainika kwamba nguvu ya moyo wa mwanamume hupungua kwa asilimia 20 –
25 kutoka miaka 18 hadi 70, lakini nguvu ya moyo wa wanawake wenye umri wa
miaka 70 haitofautiani na ya vijana wenye umri wa miaka 20.






No comments:
Post a Comment