Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) |
Kocha wa
timu ya taifa ya vijana, Jacob Michelsen amesema kuwa anajivunia vijana wake
licha ya kuondolewa na Congo kwenye mashindano ya kuwania nafasi ya kucheza
fainali za Mataifa ya Afrika na kulaumu uamuzi kuwa ulichangia kwa kiasi
kikubwa Serengeti Boys kulala kwa mabao 2-0 mjini Brazaville.
Kwa matokeo
hayo, Serengeti Boys imeondolewa kwenye mashindano ya Afrika kwa vijana walio
na umri chini ya miaka 17 kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya mechi ya kwanza
iliyofanyika jijini Dar es salaam kuisha kwa Tanzania kuibuka na ushindi wa bao
1-0 kwenye Uwanja wa Taifa. Timu hiyo itarejea nchini siku ya Jumanne saa 1:00
jioni kwa ndege ya Kenya Airways.
Serengeti Boys |
“Vijana
walicheza vizuri sana na walicheza kwa juhudi wakati wote wa mchezo na safari
hii wacheza dhidi ya vijana ambao ni wakubwa zaidi,” alisema kocha huyo kutoka
Denmark. “Lakini waliangushwa na uamuzi kwa sababu walipata penati ambayo
haikustahili.
“Kwa kweli
hata tukio lenyewe lilitokea nje ya penati na beki wetu alilala kuchukua mpira
na alifanikiwa kuufikia bila ya kumgusa mshambuliaji wa Congo. Lakini wakati
beki wetu akiwa ameshauchukua mpira na yule aliyejiangusha akiwa
ameshanyanyuka, mwamuzi alipiga filimbi kuamuru penati.”
Kocha huyo
alisema pamoja na bao hilo Serengeti Boys iliendelea kucheza vizuri na nusura
mchezo huo uamuliwe kwa penati tano, lakini wenyeji wakapata bao la pili
lililoinyima Tanzania nafasi ya kufuzu kwa mara ya kwanza kucheza fainali hizo.
“Lilikuwa ni
bao lilitokana na shambulizi la kushtukiza na walikimbia vizuri na mpira na
baadaye kupiga krosi iliyounganishwa kwa kichwa,” alisema Michelsen.
“Najivunia
vijana wangu kwa sababu walicheza kwa kujituma na kujiamini; walifanya juhudi
kubwa, lakini uamuzi ulituangusha. Nina imani na timu hii na natumaini kama
vijana watano walitoka kwenye timu ya U-20 na kuingia timu ya taifa, basi kuna
vijana wengine wanaoweza kutoka kwenye timu hii na kuingia timu ya taifa. Ni
vizuri tukaendelea na programu za vijana tuweze kujenga timu nzuri baadaye.”
Afisa wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Salum Madadi ambaye aliambatana na
timu hiyo Congo, alisema mechi hiyo ilizingirwa na mizengwe kabla na baada ya
mechi na kwamba wamesharipoti matukio yote kwa kamisaa wa mechi hiyo baada ya
kocha msaidizi, Jamhuri Kihwelo, mtunza vifaa Juma Kizwezwe na mkalimani wa
timu kushambuliwa na polisi na mashabiki kabla ya mechi hiyo.
“Hatukupewa
gari la polisi wakati wa kwenda uwanjani na hivyo hatukujua tuingilie wapi.
Tulipofika uwanjani, walituelekeza mlango ambao tuliona wanaumwagia maji ambayo
Julio aliona yangeathiri wachezaji na kuwaagiza wasitumie mlango huo na ndipo
polisi walipomvamia,” alisema Madadi.
“Kizwezwe
alishambuliwa na mashabiki baada ya kamisaa kumuagiza arejee hotelini kufuata
jezi zaidi kutokana na Congo kuwasilisha pingamizi kabla ya mechi kuwa jezi za
Tanzania hazikuwa kwenye mlolongo uliokuwa kwenye orodha iliyowasilishwa.
“Alipotaka
kutoka uwanjani, alizuiwa na askari na tukalazimika kumuita kamisaa ambaye
aliagiza polisi wamruhusu atoke uwanjani. Alipotoka mashabiki walimzuia
asiondoke na mzozo ulipokuwa mkubwa mashabiki walimvamia na ndipo tulipomwita
tena kamisaa ambaye aliagiza Kizwezwe asiondoke na badala yake jezi zilizokuwa
na matatizo zibandikwe plasta. Hata hivyo, polisi walimzuia Kizwezwe asiende
kukaa kwenye benchi hadi mchezo ulipoisha.”
Madadi
alisema kuwa kutokana na vurugu hizo, kamisaa huyo kutoka Afrika Kusini aliomba
majina ya walioshambuliwa na akaahidi kuyaweka matukio hayo kwenye ripoti yake.
Katibu Mkuu
wa TFF, Angetile Osiah alisema Shirikisho limeyapokea matokeo hayo kwa
masikitiko kutokana na ukweli kwamba TFF ilifanya juhudi kubwa katika
kuhakikisha safari hii timu za vijana zinapata maandalizi mazuri na ya muda
mrefu, lakini juhudi hizo zimekwamishwa na mazingira mabaya kama
yalivyoripotiwa na viongozi wa msafara wetu.
“Katika
kutafuta mafanikio hakuna njia ya mkato. Ni lazima tuamini katika program
tunazozitekeleza na kuboresha pale tunapoona pana udhaifu. Tunaamini kuwa
itafika wakati juhudi hizi zitazaa matunda na Watanzania watanufaika na mipango
hii ya muda mrefu,” alisema katibu huyo.
No comments:
Post a Comment