Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Dk Emmanuel Nchimbi
|
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi
amesema Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) litakabidhiwa iliyokuwa kambi ya kuhifadhi
wakimbizi ya Mtabila mkoani Kigoma.
Pia amesema hivi sasa Tanzania ina jumla ya wakimbizi zaidi ya 60,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) walioko katika Kambi ya Nyarugusu mkoani humo.
Dk Nchimbi aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kufungwa kwa kambi hiyo iliyokuwa ikiwahifadhi wakimbizi kutoka Burundi tangu mwaka 1994.
Alisema
kambi hiyo iliyokuwa na zaidi ya wakimbizi 36,000 ilifunguliwa rasmi mwaka
1994, ikiwapokea kutoka nchini Burundi walipokimbia vita vya wenyewe kwa
wenyewe kufuatia kuuawa kwa Rais wa nchi hiyo, Melkior Ndadaye mwaka 1993.
“Baada ya
kuifunga rasmi kambi hiyo kwa wakimbizi kurejeshwa nchini kwao, tutawakabidhi
JKT kambi hiyo ili kuweza kuendeleza eneo hilo kwa shughuli mbalimbali zikiwemo
za kilimo,” alisema Dk Nchimbi.
“Yaliyokuwa
majemgo ya shule na zahanati yatakarabatiwa na kukabidhiwa kwa Serikali ya mkoa
huo na huduma husika zitaanza kutolewa,” alisema.
Alisema hadi
kufikia Desemba 12 mwaka huu, raia wa Burundi 35,354 waliokuwa wakimbizi
walikuwa tayari wamerejeshwa katika nchi yao.
“Jumla ya
wakimbizi 2,400 ambao wana sababu za msingi za kuendelea kubaki nchini wamepewa
hifadhi katika Kambi ya Nyarugusu wakisubiri suluhisho jingine la kudumu,”
alisema Dk Nchimbi.
Alisema kuwarudisha wakimbizi hao kwa kushirikiana na Serikali ya Burundi na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) imehitimisha safari ya muda mrefu kuwarudisha nchini kwao.
Dk Nchimbi
alizitaja kambi nane za wakimbizi zilizokuwa zimefungwa kabla ya Mtabila kuwa
ni Karago, Mtendeli, Kanembwa na Nduta zilizokuwa wilayani Kibondo mkoani Kigoma.
Nyingine ni Muyovosi iliyokuwa Wilayani Kasulu mkoani Kigoma, Lukole A na B wilayani Ngara mkoani Kagera, Mkungwa wilayani Kibondo mkoani Kigoma na Kitali iliyokuwa wilayani Biharamulo mkoani Kagera.
No comments:
Post a Comment