Afisa
Muuguzi Kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Flora Kasembe akimpima shiniko
la damu mwandishi wa habari Manuel Kaminyoge katika hospitali ya Vwawa-Mbozi.
|
Daktari
Bingwa wa Magonjwa ya Moyo George Lyego Longopa Kutoka Taasisi ya Magonjwa ya
Moyo ya Jakaya Kikwete akichukua maelezo ya mgonjwa wa moyo katika hospitali ya
Vwawa-Mbozi.
Wagonjwa 467
wenye matatizo ya moyo wamebainishwa na kupatiwa huduma ya ushauri na matibabu
kutoka kwa madaktari bingwa waliotoa huduma kwenye kambi maalumu ya siku 4
katika hospitali ya Vwawa-Mbozi Mkoani Songwe.
Timu ya
Madaktari Bingwa na wauguzi 5 wameeleza kuwa wagonjwa 18 kati ya hao
waliowahudumia wamepewa rufaa ya kufika hospitali za Rufaa kwa ajili ya
matibabu Zaidi.
Daktari
Bingwa wa Magonjwa ya Moyo George Lyego Longopa Kutoka Taasisi ya Magonjwa ya
Moyo ya Jakaya Kikwete amesema wameanza matibabu siku ya Jumanne na kila
Daktari amekuwa akiona zaidi ya wagonjwa 60 kutokana na hamasa ya wagonjwa
waliojitokeza kupata matibabu ya magonjwa ya moyo.
“Tumeona
wagonjwa wengi na tumeamini kuwa Songwe tatizo la Magonjwa ya moyo bado ni
kubwa, wagonjwa wengi wamekutwa na matatizo ya shinikizo la damu, moyo
kushindwa kufanya kazi vizuri pamoja na matatizo ya mishipa ya damu kuziba”,
amesema Dkt Longopa.
Afisa
Muuguzi Kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Flora Kasembe ameeleza kuwa
mtindo wa maisha ya wananchi wa Songwe unaweza kuwa ni chanzo cha magonjwa ya
moyo hasa kutokana na uwepo vyakula vingi lakini wananchi hawali mlo kamili.
Kasembe
amefafanua kuwa, “tumekuwa tukitoa elimu ya kuzingatia mlo kamili ili hivi
vyakula vingi vilivyopo huku visaidie kuimarisha afya na sio waishie kuuza tu
bila wao kutumia, pia wananchi wajenge mazoea ya kufanya mazoezi na endapo
watabainika na matatizo na wakaanzishiwa dawa wazitumie kwa usahihi waiache”.
Baadhi ya
wagonjwa waliohudhuria kupata matibabu ya moyo wameishukuru serikali kwa
kusogeza huduma karibu na utaratibu huo ufanyike mara kwa mara ili wananchi
wengi wapate huduma ya madaktari bingwa.
Brigita
Haule ambaye amepata matibabu ya moyo ameeleza kunufaika na huduma hiyo kwani
hakuwa akifahamu kama ana tatizo la moyo mpaka alipofika katika huduma hiyo.
“Wengi
tunajiamini ni wazima kwakuwa hatusikii kuumwa sana ila tunatembea na magonjwa
mbalimbali ambayo tunakuja kuyafahamu yakiwa katika hali mbaya, mimi pia
sikufahamu kama nina tatizo hivyo nawashauri wote tuwe na utaratibu wa kupima
afya zetu”, amefafanua Bi Haule.
Kwa upande
wake Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt Kheri Kagya amesema utaratibu wa kuwaalika
madaktari bingwa wa moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete uliangaliwa
na uongozi wa Mkoa baada ya kubaini kuwa kuna wagonjwa 210 wa moyo.
Dkt Kagya
ameongeza kuwa wagonjwa waliojitokeza wamekuwa wengi kuliko matarajio ya awali
huku akieleza kuwa hayo ni mafanikio kwakuwa wameweza kuwabaini wagonjwa ambao
hawakutambulika hapo awali.
|
No comments:
Post a Comment