Serikali
imepanga kuajiri walimu 11,000 wa shule za msingi na sekondari katika mwaka wa
fedha wa 2017/18.
Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Suleiman Jafo alisema
katika mpango huo, walimu 7, 000 watakuwa wa shule za msingi na 4,000 wa
sekondari.
“Hadi
kufikia Desemba 31, walimu 2,700 watakuwa wameshaajiriwa,” alisema Jaffo
Akizungumza
na waandishi wa habari mjini Dodoma wakati wa kurekodi kipindi cha Tujadiliane
kinachoandaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) na kurushwa
kwenye vyombo mbalimbali vya habari, Jafo alisema ajira hizo zitapunguza upungufu
wa walimu unaotokana na ongezeko la wanafunzi tangu Sera ya Elimu Bure ya
Msingi ianze kutekelezwa.
Tangu mwaka
jana, Serikali inatekeleza sera hiyo inayoligharimu Taifa zaidi ya Sh20 bilioni
kila mwezi, huku idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa katika shule za msingi na
wale wanaojiunga na za sekondari ikiongezeka kwa zaidi ya wanafunzi milioni
moja.
Kuhusu
miundombinu shuleni alisema kwamba Serikali imetenga zaidi ya Sh37 bilioni za
ujenzi wa mabweni katika shule za sekondari za umma 148.
Akifafanua,
Jafo alisema zaidi ya Sh21 bilioni zimetumika kujenga mabweni 85 katika awamu
ya kwanza ya mpango huo, huku awamu ya pili ya kujenga mabweni 65 iliyoanza
kutekelezwa Agosti ikitarajiwa kugharimu Sh16 bilioni.
Kuhusu
matundu ya vyoo na vyumba vya madarasa, Waziri Jafo alisema Serikali imetenga
zaidi ya Sh246 bilioni kukabiliana na upungufu wa matundu ya vyoo na vyumba vya
madarasa katika shule za umma.
“Theluthi
moja ya fedha hizo, sawa na Sh82 bilioni zitatumika kukamilisha miradi ya
ujenzi wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo inayotekelezwa kwa nguvu za
wananchi,” alisema.
Waziri Jafo
alisema kuwa Serikali imepanga kujenga vituo vya afya 172 kwa fedha kutoka
Benki ya Dunia (WB), Serikali ya Canada na wadau wengine kupitia mfuko wa
pamoja wa kuendeleza Sekta ya Afya (Basket Fund).
“Lengo ni
kutekeleza sera ya zahanati kila kijiji na kituo cha afya katika kila kata ili
kuwahakikishia wananchi upatikanaji wa huduma za afya,” alisema Jafo.
Alifafanua
kuwa hivi sasa ni kata 530 pekee kati ya 3,900 zilizopo nchini ndizo zenye
vituo vya afya.
Kuhusu
upatikanaji wa dawa na vifaatiba, alisema Serikali imeongeza bajeti hadi
kufikia Sh269 bilioni kwa ajili hiyo.
“Tunazo pia
zaidi ya Sh127 bilioni za Basket Fund zitakazoelekezwa kwenye utatuzi wa
changamoto ya upungufu wa dawa na vifaa tiba kwenye zahanati, vituo vya afya na
hospitali za umma,” alisema.
Akizungumzia
upungufu wa watumishi katika sekta ya afya iliyochangiwa na uhakiki wa vyeti
feki, Waziri Jafo alisema tayari Serikali imeajiri watumishi 2,058 huku wengine
zaidi wakitarajiwa kuajiriwa.
Suala la
uhakiki wa vyeti lililoendeshwa na Serikali mwaka jana liliwanasa zaidi ya
watumishi 19, 000 ambao ajira zao zilisitishwa, huku sekta ya afya na elimu
zikiathirika zaidi.
|
No comments:
Post a Comment