
Mbunge wa
Muleba Kusini (CCM), Prof. Anna Tibaijuka, ametangaza kung’atuka nafasi ya
ubunge kwa kutogombea tena kwenye uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020.
Prof.
Tibaijuka alitangaza msimamo huo jana mkoani Kagera, wakati wakizungumzia miaka
miwili ya serikali ya Rais John Magufuli ambaye hivi sasa yuko mkoani humo kwa
ziara za kikazi.
Jumatatu ya
wiki iliyopita, Lazaro Nyalandu, ambaye alikuwa Mbunge wa Jimbo la Singida
Kaskazini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), alitangaza kujiuzulu ubunge
na pia kujivua uanachama wa CCM kutokana na kile alichoeleza kuwa ni
kutoridhishwa na mwenendo wa chama hicho.
Baadaye
Nyalandu alionekana akikaribishwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Kisheria, kuhama chama humpotezea mbunge sifa ya kuendelea kuwa mwakilishi wa
jimbo lake na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) huandaa uchaguzi mwingine mdogo
kwa ajili ya kumpata mbunge mwingine kwenye jimbo husika.
Wakati
akifafanua kuhusu uamuzi wake wa kutogombea tena ubunge mwaka 2020, Tibaijuka
aliyewahi kuwa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, aliiambia Televisheni ya
Taifa (TBC), kuwa ameamua kujing’atua ili kutoa nafasi kwa vijana.
“Sisi ni
watu wazima… kizazi chetu tumeshamaliza kazi. Tumeshastaafu na mimi nikimaliza
ubunge muhula huu nastaafu, nakwenda Muleba,” alisema Tibaijuka na kuongeza:
“Na kuaga
nimeshaaga na wananchi wameniamini. Napenda tuwape nafasi vijana. Kuzeeka
haimaanishi kwamba maarifa yangu yaondoke kwa sababu nimestaafu, tunawapa
nafasi vijana washike nchi.
“Baba wa
Taifa Mwalimu Julius Nyerere alisema tung’atuke… na mimi nang’atuka ili maarifa
yetu yaweze kutumika kushauri, jamani tufanye hivi ili tuende mbele.”
Akizungumzia
utendaji wa serikali ya Rais Magufuli katika kipindi cha miaka miwili tangu
aingie madarakani Novemba 5, 2015, Tibaijuka alisema amefanya mengi mazuri na
lazima Watanzania waendelee kumuamini.
“Hii nchi
ilikuwa inasubiri kiongozi si Rais. Rais lazima awe pia kiongozi… sasa
tujifunze kujua tofauti, mtu anaweza kukalia nafasi, lakini anaongoza?
Anaonyesha njia? Ni jasiri? Kwa maana ujasiri unatokana na ukweli,” alisema.
Tibaijuka
aliondolewa katika nafasi ya uwaziri kwenye serikali ya awamu ya nne ya Rais
(mstaafu) Jakaya Kikwete wakati baadhi ya wabunge walipomhusisha na kashfa ya
uchotwaji wa mabilioni ya shilingi kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa
Benki Kuu (BoT).





No comments:
Post a Comment