|
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amewataka Madiwani
wasio na Shughuli ya kuwaingizia Pesa binafsi kujiuzulu, kwani Serikali yake
haiwezi kuwaongezea posho wanayohitaji.
Akizungumza
kwenye uzinduzi wa mkutano wa 33 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT)
uliofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere Dar es salaam, amesema kwamba
Madiwani hao walifahamu masharti ya kugombea nafasi hiyo, hivyo kama
wameshindwa kuyatimiza ni vyema wakajiuzulu.
“Ndio
maana diwani masharti tunapojaza fomu tunaambiwa lazima uwe na kazi maalum
inayokupa kipato, sasa kama wapo madiwani waliojaza hiyo nafasi na hawana kazi
ya kuwapa kipato, wajiuzulu udiwani”, amesema Rais Magufuli.
Leo katika
hotuba iliyowasilishwa kwa Rais Magufuli ikisomwa na Mwenyekiti wa Jumuiya Ya
Tawala za Mitaa (ALAT) Bwana Gulam Mkadam, waliomba kuongezewa posho za madiwani,
kutoka Tsh. 300,000 hadi Tsh. 800,000 jambo ambalo Rais amelipinga.
Katika hatua
nyingine,Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameahidi kuwafukuza kazi Wakurugenzi wa
halmashauri wanne kwa ulevi wa pombe pindi wawapo makazini.
"Nimepata
taarifa ya Wakurugenzi kama wawili watatu hivi ni walevi sana, nawaambia hao
wataondoka kama upo hapa Mkurugenzi halafu ni mlevi ukajirekebishe haraka sana,
kabla sijaja huko ili angalau uonekane umebadilika" alisema Rais
Magufuli.
Mbali na
hilo Rais Magufuli aliwataka viongozi hao kwenda kumaliza migogoro mbalimbali
ndani ya halmashauri zao na mivutano isiyokuwa na msingi na kusema kuwa vyama
vya siasa si adui bali adui wa kwanza wa serikali yake ni watu wanaokuja kuiba
maliasili za Tanzania.
"Haipendezi
kuwa na makundi, muyamalize makundu hayo kwenye manispaa, tunajenga nyumba moja
adui yetu siyo vyama tunachelewa sana, adui yetu ni wale wanaotuibia nasema
mkamalize hayo makundi huko, najua tofauti lazima zitakuwepo lakini kwenye
masuala ya kazi lazima tushikamane kwa maslahi ya Watanzania, mkawaimize
Watanzania kufanya mambo ya maendeleo" alisisitiza Rais Magufuli
|
No comments:
Post a Comment