Waasi
wanaodaiwa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wamewateka madereva 21,
wakiwamo Watanzania 18 wanaofanya kazi kwenye kampuni ya malori ya mizigo ya
Alistair ya nchini.
Meneja
usimamizi wa Tanzania na DRC wa kampuni ya Alistair , Anna Joyce Mbise
aliliambia gazaeti la Mwananchi jana
kuwa madereva hao walitekwa asubuhi ya
Juni 29, baada ya mapambano kati ya askari wa Serikali ya Congo na waasi hao.
“Kwa mujibu
wa maelezo ya madereva hao ni kwamba askari wa Serikali waliokuwa
wanawasindikiza kabla ya msafara kuvamiwa, walizidiwa kwenye mashambulizi hayo
ndipo wakatekwa,” alisema Mbise na kuongeza:
“Wametueleza
kuwa hakuna aliyejeruhiwa katika tukio hilo, waasi wamekuwa wakizungumza nao
vyema, lakini gari zetu tatu zimeharibika kwa risasi kutokana na mashambulizi
hayo,” alisema.
Alisema
kampuni hiyo imewasiliana na viongozi husika wa Serikali kwa kuandika barua
Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ili wasaidie
madereva hao kuachiwa huru wakiwa salama.
“Tumejawa na
hofu kuhusu usalama wao, kwani tunaamini kwamba askari wa jeshi la Serikali
lazima wanajipanga kurejea kupambana ili kulikomboa eneo hilo, hapo tuna
wasiwasi na usalama wa madereva hao ,” alisema.
Mratibu wa
Shirikisho la Wasafirishaji Afrika Mashariki (FEARTA), Emmanuel Kakuyu alisema
taarifa walizonazo ni kwamba madereva hao wamekumbwa na mkasa huo katika eneo
la kijiji cha Lulimba kilichopo kati ya Ziwa Tanganyika na Kindu Manyema.
Alisema
waasi hawa hawajawadhuru madereva hao, lakini alifafanua kuwa madereva watatu
kati ya 21 wanatoka Uganda.
“Watekaji
wamekuwa wakizungumza nao vizuri ikiwamo kuwahakikishia usalama wao wakidai
kwamba hawana ugomvi nao, bali wana ugomvi na Serikali ya Congo,” alisema.
Umbali kati
ya Lulimba na Kigoma ni kilomita 448, lakini ili ufike Lulimba ni lazima
ulizunguke Ziwa Tanganyika upande wa mashariki mwa DRC.
Kaimu
Mkurugenzi wa dawati la Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Suleiman Saleh alijibu kwa kifupi kwamba
wamepokea taarifa za utekaji huo na tayari wameanza kushughulikia.
|
No comments:
Post a Comment